Saturday 8 March 2008

Rais wa Marekani awashukuru Watanzania

Rais George W. Bush wa Marekani, ameahidi kuendelea kufanya kazi na Rais Jakaya Kikwete pamoja na viongozi wengine, ili kuisaidia Tanzania kushughulikia changamoto zinazoikabili.

Katika barua yake kwa Rais Jakaya Kikwete na Watanzania wote iliyotolewa jana na ofisi ya ubalozi wa Marekani nchini, Bw. Bush alisema serikali yake itaendelea kutoa misaada kwa Tanzania.

``Tunashukuru kwa urafiki wake na urafiki wenu, tutaendelea kutoa misaada yetu wakati mnapozidi kusonga mbele,`` ilisema sehemu ya barua hiyo.

Bw. Bush ameandika barua hiyo akitoa shukrani kwa Watanzania kufuatia ziara ya siku nne aliyoifanya mwezi uliopita nchini pamoja na mkewe Bi. Laura na akaahidi kutembelea tena nchini miaka ijayo.

``Laura na mimi tunapenda kuwashukuru sana kwa kutukaribisha katika nchi yenu nzuri wiki chache zilizopita. Tanzania inafahamika kwa ukarimu wake mkubwa, na ziara yetu inathibitisha kuwa kweli mnastahili sifa hiyo. Kuanzia maelfu ya wananchi mliojipanga barabarani kutukaribisha, hadi kwa watoto walioimba na kucheza kwenye sehemu mbalimbali kama vile Ukumbi wa Karimjee, Taasisi ya WAMA, pamoja na Shule ya Wasichana wa Kimasai kule Arusha.
Kwa kweli mmegusa mioyo yetu sana,`` alisema.

Alisema anajua kwamba kuwa mwenyeji wa ugeni wa Rais ni jukumu kubwa, na anatambua kwamba kulikuwa na wakati ambapo ziara yao ilileta matatizo ya usafiri, pamoja na usumbufu mwingine, na kutokana na hali hiyo anawashukuru wote kwa uvumilivu waliouonyesha wakati wa ziara yao.

``Kama mnavyojua, hii ilikuwa ni ziara rasmi ya kwanza kufanywa na Rais wa Marekani aliye madarakani. Ziara hii si tu kwamba ilikuwa na tija na mafanikio kwa upande wa mazungumzo ya serikali kwa serikali, bali pia ilikuwa ni fursa muhimu kwa Wamarekani wa kawaida kujifunza mengi kuhusu taifa lenu,`` alisema.

Alisema kupitia picha zilizopelekwa Marekani, waliweza kuona nchi inayopendeza iliyojaa watu wazuri.

Alisema Wamarekani waliwaona Watanzania wa ngazi zote wakifanya kazi kwa bidii kujenga mustakabali bora wenye mafanikio mazuri na pia waliona vijana waliodhamiria kuendeleza dira ya Mwalimu Nyerere ya kujenga Tanzania yenye amani na umoja.

* SOURCE: Nipashe, 08 Mar 2008
By Mwandishi Wetu

No comments: