Friday 15 February 2008

mjadala wa richmond waendelea bungeni

Mjadala wa Richmond moto
Mjadala kuhusu Tume ya Bunge ya kuchunguza mkataba tata wa kampuni ya uzalishaji umeme wa dharura, Richmond, ulirejelewa tena bungeni jana huku wabunge wakielezwa kushangazwa kwao na mambo yalivyokwenda katika mkataba huo.

Wabunge pia walimchachamalia mbunge mwenzao wa Jimbo la Igunga, Bw. Rostam Aziz (CCM) wakidai kuwa ndiye `mmiliki` wa kampuni hiyo na kutaka awajibishwe.

Aidha walilitaka bunge limchukulie hatua mbunge huyo kwa kulikaidi kutokana na kuigomea kamati teule ilipomwita kumhoji.

Mbunge wa Sikonge Bw. Said Nkumba(CCM)jana alimkalia kooni Bw. Aziz alipokuwa akichangia taarifa ya kamati ya Bunge iliyoanza kujadiliwa tangu Alhamisi iliyopita.

``Nimeisoma ripoti safi haina fitina, haina majungu wala haikuwa na nia ya kuwaharibia watu majina. Naipongeza kamati,`` alisema.

Aliongeza kuwa alisoma ripoti ya kamati ya Richmond na ukweli ni kwamba wale wote waliohakikisha kwamba Richmond wanapata mkataba ule, hao ndiyo Richmond na hakuna wengine.

Aliongeza kuwa TANESCO iliundwa kwa madhumuni makubwa ya kuwapa unafuu wananchi kwenye nishati ya umeme, lakini mkataba huo mbovu uliojaa mizengwe na harufu ya rushwa umewabebesha Watanzania mzigo wa kulipa fedha nyingi.

``Juni 23, 2006 waliweka mkataba na Richmond na baadaye Dowans ambayo mmoja wa wabunge wenzetu hapa, Rostam Aziz ametajwa kwenye ukurasa wa 9 wa ripoti kuwa na uhusiano nayo, ndiyo ambayo inaendelea kupokea hizo fedha Sh. 152 milioni kila mwezi kila siku.``

Akizungumza kwa uchungu mbunge huyo alisema: ``Hii ni aibu, fedheha kubwa. Mimi niombe wale wote waliohusika pamoja ambao hawakuwa katika madaraka ya serikali, wengine wana madaraka ya chama, wengine ubunge, lazima hatua za kinidhamu zichukuliwe. Jambo hili hatuwezi tukaliacha hivi hivi.``

``Nimpongeze sana Mheshimiwa Dk. Harrison Mwakyembe ameiwasilisha ripoti kwa mbwembwe, hata mimi kama ningepata nafasi hiyo ningeiwasilisha kwa mbwembwe kwani nina uhakika na kile nilichokifanya,`` alisema.

Alisema anasimama kwa maslahi ya wapiga kura wake wanaoteseka na bei kubwa ya umeme, kwa maslahi ya taifa ambalo limedhulumiwa na watu wachache waliokabidhiwa dhamana za kuongoza umma lakini hawana uadilifu na wamevunja uaminifu wa viapo vya kuwatumikia Watanzania.

``Tumeibiwa, badala ya fedha hizi zijenge barabara vijijini, zinunue madawa kwenye zahanati zetu, wananchi wapate maji safi na salama, tuongeze uwezo wa kupeleka pembejeo na ruzuku kwa wakulima. Badala ya fedha hizi tuwalipe walimu wanaodai malimbikizo na ujenzi wa madarasa, watu wachache wanaliibia taifa,`` alieleza.

Alisema kujiuzulu hakutoshi na akataka hatua za kinidhamu, za dharura za kuhakikisha kwamba Watanzania wanaridhishwa na hatua sahihi zinachukuliwa.

Aliwashambulia watuhumiwa kwa kuidharau kamati wakati ikichunguza ufisadi wa Richmond, Mheshimiwa Rostam Aziz na ndugu yetu Daniel Yona waliitwa kwenye kamati, hawakufika.

``Na Kamati katika maelezo yake mwishoni, haikutoa maelezo ni hatua gani zinachukuliwa dhidi ya hawa watu. Sasa naomba waongeze pendekezo la kuchukuliwa hatua wakati wanamaliza kujibu hoja yao hapa,`` alishauri
Alisema kuwachukuliwa hatua wote waliodharau kazi ya Bunge ni muhimu kwa kuwa kutotii mamlaka hiyo ni kumdharau Spika, Bunge na Watanzania.

Alisisitiza kuwa jambo hili haliwezi likaruhusiwa liendelee na kuomba hatua zichukuliwe na mapendekezo ya kamati mwishoni yaonyeshe.

Alisema uadilifu kwa viongozi ni suala muhimu pia ni lazima wawe mfano kwa wananchi kwa maisha yao.

``Nataka niseme hapa, kuna hii hoja ya biashara na siasa. Nasema kwamba si wafanya biashara wote si waaminifu.

Lakini wapo ambao si waaminifu na wanatafuta kila namna ya kuingia kwenye siasa wanayoiona kama kinga... Wanaona wakiwa kwenye siasa watapata kila kitu,`` alisema.
Alitaka wana siasa hao wabainishwe na huu ni mfano uliojionyesha kwenye Richmond.

``Leo ukienda katika maeneo mengine yote, utaona zabuni kubwa kubwa zina watu maalum, mwingine lazima ukapige magoti kwao ndiyo upate zabuni hata wafanya biashara wengine nafikiri watakuwa wananiunga mkono. Lazima ukapige magoti kwao ndiyo upate kazi,`` alisema na kushangiliwa sana.

Alisema kuwasaidia wananchi kwa kwapelekea maji na misaada wasiojiweza si mpaka mtu uwe mbunge au diwani.

``Unaweza ukafanya hivyo bila ya kuingia kwenye ubunge wala udiwani. Wako watu wengi tu tunawaona hapa, hawajawa na hisia hata siku moja za kuingia kwenye siasa. Kina Reginald Mengi hao, tunawaona kila siku wako wanasaidia watu hatujawasikia wanataka kugombea hizi nafasi,`` alisema na kushangiliwa.

Alionya kuwa kama watu wameingia kwenye siasa kwa ajili ya kuhakikisha biashara zao zinakwenda kwenye utaratibu ambao utapeleka nchi kwenye masuala ya Richmond safari hii watakuwa wakali kweli kweli na hakuna kuoneana haya humu bungeni.

Baada ya kutoa mchango wake Spika Bw. Samuel Sitta, alisema ``Loo! ahsante Mheshimiwa Said Nkumba``
Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Grace Kiwelu (CHADEMA) alisema wahusika wa sakata hilo wanaweza kutorokea nje ya nchi ili kukwepa mkono wa sheria na kwamba njia pekee ya kuwazuia ni kuwanyang’anya hati za kusafiria.

``Kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri peke yake haitoshi, waliohusika wachukuliwe hatua na labda nitoe tu angalizo kwamba pasipoti zao zizuiliwe, wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili na haki ijulikane,`` alisisitiza.

Alifafanua kuwa haki inaweza kupatikana mahakamani hivyo wale wanaodhani wanasingiziwa wanapaswa kufuata mkondo wa sheria badala ya kulalamika.

Aidha, mbunge wa Ubungo, Bw. Charles Keenja (CCM) alisema njia pekee itakayoonyesha kiwango cha utekelezaji wa mapandekezo ya kamati teule ni serikali kutoa taarifa yake kwa Bunge.

``Mkataba wa Richmond haukufanyika kwa bahati mbaya, yalikuwa ni makusudi kwa ajili ya kuwaneemesha wachache. Hivyo pamoja na kupendekeza wahusika wachukuliwe hatua kali kwelikweli naomba serikali iyafanyie kazi mapendekezo ya tume na kuleta taarifa ya utekelezaji hapa Bungeni, mheshimiwa Spika hatuwezi kusamehe jambo linaloudhi namna hii`` alisema.

Aliongeza kuwa mkataba tata wa Richmond ulifanywa na serikali chini ya shinikizo la viongozi na hivyo kutokana na hali hiyo inapaswa kulipa kampuni hiyo na si suala la TANESCO kulipa Sh. milioni 152 kila siku.

``Serikali itafute fedha hizo zilipo na si kuiwajibisha TANESCO na wananchi,`` aliongeza.

Bw. Keenja alisema uchunguzi zaidi unahitajika ili kubaini `mchawi` aliyeishinikiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuudanganya umma katika suala nyeti kama la Richmond.

Alibainisha kuwa ni vyema vyombo kama TAKUKURU na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwajibika kwa bunge.

``Lazima tumjue aliyeishinikiza PCCB kutoa ripoti chafu kiasi kile na tunaweza kupendekeza vyombo kama TAKUKURU na CAG viwajibike kwetu,`` alisistiza.

Kwa upande wake, mbunge wa viti maalum (CUF) Bi. Magdalena Sakaya alitaka TAKUKURU ipanguliwe na Mkurugenzi wake Mkuu Bw. Edward Hosea achukuliwe hatua za kisheria.

Alifafanua kuwa kutokana na uzembe wa uwajibikaji uliofanywa na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali, mamlaka hiyo ‘ipigwe chini’ na kupangwa upya.

``Tumethibitisha kuwa uwezo wa TAKUKURU ni kula dagaa na si samaki pamoja na kwamba tulipitisha sheria ya kuiongezea meno. Napendekeza tuipige chini pamoja na Mwanasheria Mkuu wa serikali ili tuweze kujipanga upya. Lakini pia kila kiongozi aliyehusika kwa namna yoyote ile awajibishwe ili kutoa fundisho kwa vizazi zijavyo`` alisema.

Bi. Sakaya alibainisha kuwa kupanda kwa gharama za umeme kunazidi kuhatarisha uhai wa mazingira kunakosababishwa na ukataji miti kwa matumizi ya nishati.

Naye mbunge wa Igalula (CCM) Bi. Tatu Ntimizi aliitaka serikali kuvunja mikataba yote inayoliangamiza taifa bila kuogopa kushitakiwa ili kuikomboa nchi.

Aliongeza kuwa, utafiti wake unaonyesha kuwa makusanyo ya kila mwezi ya TANESCO ni takribani Sh. biloni 30 ambapo Sh. bilioni 21 zinaenda kwa makampuni matano yanayozalisha umeme hapa nchini.

Makampuni hayo ni IPTL, Richmond, Songas, Aggreko na Artumas.

Awali Kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni Bw. Hamad Rashid Mohamed ambaye alikuwa mchangiaji wa kwanza wa mjadala huo alisema wafuasi wake wanahitaji maelezo ya kina kutoka serikalini juu ya kukiuka sheria za nchi kwa kuingia mikataba tata inayoliangamiza taifa.

Alisema mipango ya taifa ni kuwafikishia wananchi wa vijijini umeme kwa haraka zaidi jambo linaloelezwa katika sera ya taifa ya umeme na kueleza kuwa makampuni yanayozalisha nishati hiyo hapa nchini hayajafanya hivyo hadi sasa.

``Tunataka serikali itueleze kwa nini inaingia mikataba inayokinzana na sera zetu... Kwa nini imekuwa kinara wa kuvunja sheria mfano kama ilivyokiuka sheria ya manunuzi ya umma hasa katika sakata la Richmond kama ilivyoelezwa katika ripoti ya kamati teule`` alisema.

Kwa mujibu wa Bw. Mohamed, TANESCO imekuwa ikilipa Sh. bilioni 444.4 kila mwaka kwa makampuni matano yanayozalisha umeme hapa nchini jambo linalozidi kuliangamiza.

Aliongeza kuwa utata wa Richmond umedhihirisha jinsi serikali ilivyokiuka sheria kwa makusudi hivyo ili kutokomeza jambo hilo ni kuwachukulia hatua kali wahusika wote.

Alisema kuna vipengele vitano katika mkataba wa Richmond vinaruhusu kuvunja mkataba na kuongeza kuwa serikali inaweza kutumia mwanya huo kuutupilia mbali.

``Naomba Bunge lako tukufu lipitishe azimio la kuona mikataba ili tusiendelee kuporwa rasilimali zetu maana tumeomba mikataba kwa muda mrefu bila mafanikio,`` alisema na kuongeza: ``Hili tunalofanya hapa ni rasharasha, tunayo mikataba chungu nzima, tuende mbele zaidi, tuangalie madini, majengo ya BoT `twin tower` na kwingineko`` alisistiza.

Kwa upande wake, Mgana Msindai Iramba Mashariki (CCM) aliongeza kuwa hakuna sababu ya kuilipa Richmond ikiwa haipo Marekani wala hapa nchini.

Kwa upande wake, mbunge wa Busanda (CCM) Bw. Kabuzi Rwilomba aliwataka wanasheria watumie taaluma yao kulinasua taifa katika mikataba tata na kwamba sio lazima kuendelea nayo hadi mwisho.

* SOURCE: Nipashe, 15 Feb 2008
By Gaudensia Mngumi, Dodoma

No comments: