Monday 18 February 2008

George Bush ndani ya TZ

Rais wa Marekani, Bw. George Bush, amepongeza utawala wa Rais Jakaya Kikwete kwamba umeonyesha kwa dhati na kwa vitendo kupambana na ufisadi nchini.

``Wewe ni mtu mzuri Bw. Rais, ninajisikia furaja kukuita rafiki,`` Bush alimwambia Kikwete, huku ndege aina ya tausi wakionekana kukonga nyoyo za wageni wengi waliohudhuria sherehe hiyo mbele ya ofisi za Ikulu jijini Dar es Salaam.

Ilikuwa ni muda mfupi baada ya kutia saini mkataba wa dola za Marekani milioni 698 kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo barabara, afya na umeme nchini.

Pesa hizo zinatoka kwenye mfuko uitwao Millenium Challenge Corporation (MCC) ambao ulianzishwa na uongozi wa Rais Bush mwaka 2002.

Nchi zinazopewa pesa kutoka katika mfuko huo ni zile zinazoonekana kuendesha utawala bora, kuwekeza katika elimu, kuendeleza ujasiriamali, mazingira pamoja na sera nzuri za kiuchumi.

Kiasi kilichosainiwa jana kinaelezwa kuwa ndicho kikubwa zaidi kutolewa na mfuko huo.

``Matumaini yangu ni kwamba msaada huu utakuwa sehemu muhimu katika juhudi za kuendeleza baadhi ya maeneo ya nchi hii,`` alisema Rais Bush.

Alisema Rais Kikwete ni mtawala mzuri na shupavu na ameweza kupambana na rushwa na akaahidi kuwa Marekani mbali ya kuendeleza uhusiano na nchi za Afrika, lakini Tanzania itakuwa rafiki mkubwa.

Kwa mujibu wa Bw. Bush, chini ya utawala wake alifanikisha mara mbili kwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kufutiwa madeni ikiwa ni pamoja na kuongeza misaada kwa nchi hizo.

Rais Kikwete kwa upande wake alimuomba Rais Bush kuwa hata kipindi chake cha urais kikimalizika, atakayempokea aendeleze mahusiano mazuri na Tanzania.

Ombi ambalo lilikubaliwa na Rais Bush na kueleza kuwa Marekani ina mapenzi ya dhati na nchi za Afrika.

Kuhusu msaada huo wa dola milioni 698, Rais Bush alisema wanakusudia kuanzisha programu maalum ya miaka minne ya kutoa misaada kwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.

Rais Kikwete alisema maelfu ya Watanzania wangekuwa wamekufa kama si mpango ulioanzishwa na Rais Bush katika kupambana na malaria na Ukimwi duniani kote.

"Utakumbukwa sana kwa vizazi vingi vijavyo kwa mambo mazuri ambayo umeifanyia Tanzania na mengi mazuri ambayo umeifanyia Afrika," alisema Rais Kikwete.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kiongozi wa chama Democrat nchini Marekani, Barack Obama, ambaye baba yake anatokea Kenya kushinda urais wa nchi hiyo, Rais Kikwete alisema: ``Ni kweli watu wanaongea kwa matumaini kuhusu Obama, lakini kikubwa kwetu ni kwamba Rais Bush yuko katika kumalizia muda wake na Marekani itapata rais mwingine, yeyote yule watakayempata.``

``Kwetu sisi, kitu muhimu zaidi ni, kama yeye (Obama ama mwingine atakayechaguliwa) atakuwa rafiki wa Bara la Afrika kama Rais Bush.``

Wakati akianza kuzungumza na waandishi wa habari, jana, Rais Bush aliwasalimia kwa Kiswahili: ``mambo`` salamu ambayo iliangua vicheko kwa watu waliohudhuria hafla hiyo ambao waliitikia, `poa``

Rais Bush na mkewe Laura pia jana walitembelea hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam ambayo inapata msaada wa Marekani.

Rais Bush pia jana alikutana na familia zilizoathirika na shambulizi la mabomu ya al Qaeda katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam mwaka 1998.

Jana, kama kawaida, makachero wa Marekani walitawala kila kona ya Ikulu na ndiyo yaliyokuwa yakiendesha upekuzi kwa watu waliokuwa wakiingia.

Rais Bush aliingia nchini juzi saa 12:35 jioni na kufanya eneo la uwanja wa ndege wa zamani kutawaliwa na makachero wake ambao walisheheni vifaa vya usalama na mawasiliano kila kona ya uwanja huo.

Makachero hao wakiwa na mbwa, walionekana hata juu ya majengo ya uwanja huo na hata ulinzi wa polisi wa Tanzania ulikuwa mdogo kwani walionekana wachache sana uwanjani hapo na badala yake walijazwa kwenye barabara alizopita Rais huyo.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Bush kuzuru bara la Afrika toka aingie madarakani.
Agosti, 2000 aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Bw. Bill Clinton alitembelea Tanzania ambapo alifikia mkoani Arusha kwa ajili ya kusaini mkataba wa amani kati ya vikundi vilivyokuwa vikipingana serikali ya Burundi ambayo kwa wakati huo ilikuwa madarakani.

Rais Bush anatarajiwa kuondoka nchini kesho kuelekea nchini Rwanda na baadaye ataelekea nchi za Ghana na Liberia kwa ziara kama ya Tanzania.

* SOURCE: Nipashe, 18 Feb 2008
By Dunstan Bahai

No comments: