Saturday 16 February 2008

Mama Salma Kikwete (hotuba)

HOTUBA YA MHE. MAMA SALMA KIKWETE, MWENYEKITI WA TAASISI YA WANAWAKE NA MAENDELEO (WAMA), KATIKA UZINDUZI WA
MRADI WA UJANA ULIOFANYIKA HOTELI YA GOLDEN TULIP DESEMBA 11, 2006

Mheshimiwa Balozi wa Marekani, Michael Ritzier,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Abbas Kandoro,
Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Mej. Jen. (Mstaafu) Herman Lupogo,
Mkurugenzi wa Mradi wa YouthNet (Family Health International), Bi Tonya Nyagiro
Viongozi wa Serikali,
Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na Asasi Mbalimbali,
Vijana,
Waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa tukiwa wazima na wenye afya njema. Aidha nawashukuru sana Family Health International kwa heshima kubwa mliyonipa kwa kunialika nishirikiane nanyi kuchambua mafanikio ya mradi wa vijana wa YouthNet na hatimaye kuufunga na pia kufungua mradi mpya wa UJANA.

Ndugu wageni waalikwa,
Nimefurahi sana kushirikishwa katika mkutano huu muhimu. Hivi leo tunahitimisha Mradi wa YouthNet/Tanzania, na wakati huo huo tunasherehekea uzinduzi wa Mradi wa UJANA, hii inathibitisha kuwa kazi nzuri iliyokuwa inafanywa chini ya Mradi wa YouthNet/Tanzania, sasa itaendelea. Nafarijika sana kuona kuwa bado kuna msukumo mkubwa unaoelekezwa katika kuboresha afya ya uzazi kwa vijana wa Tanzania. Napongeza sana juhudi zinazofanywa na Serikali yetu, asasi za kiraia na wadau wengine wa maendeleo.

Ndugu wageni waalikwa,
Vijana wenye umri kati ya mika 10 na 24 wanafikia asilimia 60% ya idadi ya watu wote Tanzania. Na tunaarifiwa na tafiti za kuaminika kwamba, ingawa viwango vya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) miongoni mwa vijana viko chini kuliko kiwango cha wastani cha kitaifa, bado takribani theluthi mbili ya maambukizi mapya ya VVU hutokea miongoni mwa vijana wetu walio na umri wa chini ya miaka 45.

Takwimu hizi zinanisukuma kumtaka kila raia, kijana na mtu mzima, mwanamke na mwanaume, kutafakari upya madhara ya kutisha ya janga la UKIMWI. Kila mmoja wetu anawajibu wa kuhakikisha tunadhibiti maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI katika familia zetu, jamii yetu na taifa letu. UKIMWI unaathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wetu hivyo endapo hatua madhubuti za kuudhibiti hazitachukuliwa sasa, ni wazi kuwa nchi yetu itazidi kuzama kwenye dimbwi la umasikini.

Kila mtu anao wajibu wake wa kutekeleza ili kusaidia katika kuzuia hili janga. Sisi kama jamii, tunapaswa kujikinga wenyewe na kuwakinga vijana wetu ? na hii ndiyo sababu siku zote nasema mtoto wa mwenzio ni mwanao, mkinge na UKIMWI.

Ndugu wageni waalikwa
Kiwango cha maambukizi ya VVU ni kikubwa zaidi kwa wasichana ukilinganisha na wavulana kwa sababu za kibaiolojia, na kubwa zaidi ni kutokana na elimu duni na uwezo mdogo wa kiuchumi unaowakabili wanawake na wasichana. Ni muhimu sasa kuboresha hali ya maisha ya wanawake na watoto wa Tanzania kwa kutoa fursa za elimu, stadi na kuwawezesha kujijenga na kujitegemea kiuchumi.

Tusaidie elimu haswa kwa mtoto wa kike, tusaidie vikundi na asasi zinazolenga kuboresha usawa wa kijinsia, na pia tusaidie vikundi vya wanawake na vijana vya kujiinua kiuchumi ili kuwawezesha vijana kujiepusha na hatari ya kuambikizwa VVU.

Mheshimiwa Balozi ametueleza kuwa Serikali ya Marekani itafadhili Mradi wa UJANA kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 25 kwa miaka mitano ijayo. Uhisani huu wa watu wa Marekani kwa Tanzania, unalenga kushughulikia masuala yote muhimu niliyoyagusia yanayowezesha kumkinga kijana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Kwa niaba ya Watanzania, napenda kukushukuru sana Mheshimiwa Balozi, kwa msaada huo mkubwa uliotolewa na serikali yako kwa lengo la kuhakikisha kuwa tunaongeza juhudi na uwezo wa kuwakinga vijana na janga hili la UKIMWI.

Aidha, msaada huu mkubwa unadhihirisha kushamiri kwa uhusiano kati ya Serikali ya Marekani na Tanzania. Nimearifiwa kuwa Serikali ya Marekani, kupitia mfuko wa Rais wa Kupunguza Makali ya UKIMWI (PEPFAR), umekuwa ukifadhili mradi wa YouthNet wa shirika la Family Health International ili kutoa msaada wa kitaalam na rasilimali kwa mashirika yanayofanya vizuri katika juhudi za kuzuia maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI miongoni mwa vijana wa Tanzania.

Waalikwa mabibi na mabwana, Nina imani kuwa Watanzania, na hususan wafanyakazi na walengwa watakaofaidika na mradi huu mpya wa UJANA, watajitahidi kutekeleza majukumu yao kwa umahiri, ufanisi na uaminifu mkubwa ili kufikia lengo tulilojiwekea katika kupunguza maambukizi ya virusi kwa VIJANA. Hii ndiyo njia pekee ya kuuenzi msaada huu adhimu tuliopewa na ndugu zetu wa Marekani.

Nimefurahi kuona kuwa malengo ya Mradi wa UJANA yanashabihiana sana na malengo ya Taasisi yangu ya WANAWAKE NA MAENDELEO (WAMA) ambayo nimeizindua hivi karibuni. WAMA inalenga katika kuboresha maisha ya watoto, hususan watoto wa kike, pamoja na kudhibiti kasi ya maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI kwa vijana. Kwa sababu hiyo, napenda kusema kuwa milango ya WAMA iko wazi kwa ajili ya ushirikiano. Naahidi kuunga mkono juhudi za mradi huu mpya wakati wowote nitakapotakiwa kufanya hivyo.

Nawapongeza sana Shirika la Misaada la Marekani (USAID), uongozi na wafanyakazi wa FHI na wadau mbalimbali kwa kuendesha vizuri mradi YouthNet/Tanzania. Tuzo ya Mradi wa UJANA kwa Family Health International (FHI) ni ushahidi tosha wa mafanikio mazuri ambayo timu ya FHI imeyapata. Nawatakia mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Mradi huu mpya unaovutia. Natarajia kuwa nitakuwa napata taarifa za maendeleo ya mradi huu mara kwa mara.

Vijana wangu, UJANA ni kipindi muhimu sana katika maisha ya mwanadamu na kinapopita huwa hakirudi. Kijana aliyeutumia vibaya ujana wake hujuta sana uzeeni. Nawaomba vijana, kila mnapokumbuka na kujivunia UJANA wenu, basi mjivunie pia na mradi wa UJANA na kuhakikisha mmefaidika nao ili msije kujuta baadaye.


Nawashukuruni sana kwa kunisikiliza, Ahsateni sana


kutoka: www.jakayakikwete.com

No comments: