Friday 14 September 2007

Tutembelee mbuga za wanyama

Changamoto kwa Watanzania kutembelea mbuga za wanyama

13 Sep 2007
By Richard Makore

Unapofika katika mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro mbali na kuwakuta wanyama lakini kivutio kikubwa kuwakuta Wamasai wakiishi ndani ya mbuga hizo na hivyo na wao kuwa sehemu ya kivutio cha kitalii.

Wamasai katika mbuga hizo wameruhusiwa kuishi huko tofauti na mbuga zingine ambazo watu hawaruhusiwa kuwa na makazi yao ya kudumu.

Jamii ya kiamsai inaishi pamoja na wanyama wakali kama vile Simba, Faru, Chui na Tembo siku zote katika maisha yao bila wasiwasi.

Kila familia inaishi pamoja katika vibanda vya nyasi ambapo mtalii mmoja analazimika kulipa Sh. 20,000 kwa ajili ya kwenda kutembelea familia moja kwa ajili ya kuwaangalia ambapo huimbiwa nyimbo mbalimbali kama sehemu ya kumburudisha.

Aidha, serikali inatambua Wamasai kama jamii ya watu wanaopenda kuishi na wanyama pamoja na kuwalinda.

Mamlaka ya hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro zinawapatia huduma zote zikiwemo za maji na chakula kwa kuwa maeneo wanayoishi ni makavu na hayaruhusiwi kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Aidha, mbuga za Serengeti na Ngorongoro ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato ya serikali.

Mhifadhi Mkuu wa hifadhi ya Serengeti Bw. Martin Loibooki anasema, hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 1951 na ina ukubwa wa kilomita za mraba 14,763.

Anasema wanapokea watalii kutoka nje ya nchi kati ya 120,000 hadi 130,000 kwa mwaka ambapo kila mtalii wa nje analipa dola 50 za Marekani kama kiingilio cha kuona wanyama.

Anaongeza kuwa eneo la Serengeti mwaka 1981 lilitangazwa na serikali kama eneo la urithi na kuanzia hapo mikakati mbalimbali ya kuhifadhi wanyama ilianza kuchukuliwa kwa kasi kubwa.

Bw. Loibooki anasema, Serengeti ni eneo lenye maajabu mengi yakiwemo ya wanyama wa kila aina,wadudu, ndege pamoja na vilima na mabonde.

Anasema hivi wanyama aina ya Nyumbu wanafikiazaidi ya milioni moja jambo ambalo linawafanya watalii kuvutiwa na makundi makubwa ya wanyama hao.

Mhifadhi huyo anaongeza kuwa idadi ya watalii nayo imeongezeka lakini anawahimiza Watanzania kwenda kutembelea huko mara kwa mara.

Anasema Mtanzania anatozwa Sh.1,500 tu kama kiingilio jambo ambalo anaamini wengi wanamudu kutembelea huko mara kwa mara.

Anawataka Watanzania kuachana na imani kwamba kazi ya utalii inapaswa kufanywa na wageni na wao wabakie kuwa watazamaji na wasikilizaji.

Anafafanua kuwa Mbuga hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kwa kutoa ajira kwa wananchi katika hoteli mbalimbali za kitalii zilizojengwa ndani ya mbuga hiyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Bi. Zubein Mhita anasema, Tanzania inapata watalii wengi kutokana na amani iliyopo pamoja na demokrasia.

Anasema misingi hiyo ndiyo inasababisha watalii kwenda kutembelea visiwa vya Zanzibar. mlima Kilimanjaro, mito pamoja na maziwa mbalimbali yaliyopo hapa nchini.

Anaongeza kuwa sekta ya utalii inachangia asilimia 16 ya pato la taifa na kwamba idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Bi. Mhita anasema mwaka 1995 Tanzania ilipata watalii 295,312 ambao waliingiza dola za Marekani milioni 259 na kwamba mwaka jana kiasi hicho kiliongezeka na kufikia dola za Marekani milioni 862.

Anasema serikali itaendelea kutangaza vivutio vya kitalii kupitia magazeti makubwa, Televisheni za ndani na nje ya nchi pamoja na viwanja vya ndege 54 vilivyopo nchini Marekani.

Anafafana kuwa mipango ya serikali ni kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya watalii wa nje na ndani.

Aidha, Bi. Mhita anasema sambamba na kuongeza idadi ya watalii lakini pia serikali inatarajia kuongeza idadi ya hoteli za kitalii na kwamba uwanja wa ndege wa kimataifa unaojengwa mji wa Mugumu wilayani Serengeti utasaidia kupeleka watalii wengi zaidi.

Naibu waziri huyo anasema,utalii sio lazima ufanywe na wageni peke yake bali hata wananchi wanatakiwa kutembelea huko kwani bei ya kiingilio kidogo cha Sh. 1,500.

Kwa upande wake Kaimu Mhifadhi Mkuu wa hifadhi ya Ngorongoro Bw. Bernard Malunya anasema, mikakati yao ni kuhakikisha kwamba wanafanya utalii wa kisasa na wenye tija.

Bw. Malunya anasema, hifadhi yake nayo ina maajabu mengi ikiwemo ya bonde la Ngorongoro Crater ambalo huwavutia watalii wengi wanaopenda kuteremka chini umbali mrefu kwenda kuangalia wanyama wa kila aina.

Anasema hifadhi yake licha ya kuwa na wanyama wazuri wa kila aina lakini pia imezungukwa na milima mizuri pamoja wamasai.

Bw.Malunya anawahimiza Watanzania kutembelea mbuga za hifadhi kwa kuwa ni mali zao na zinamilikiwa na serikali yao.


* SOURCE: Nipashe

No comments: