Tuesday 18 September 2007

Hizi hela zifanye kazi yake jamani!

Marekani yatoa sh. bilioni 890
NA LEON BAHATI
BODI ya Wakurugenzi ya Ushirika wa Malengo ya Milenia (MCC) chini ya serikali ya Marekani imeidhinisha msaada wa dola za Marekani milioni 698 (sawa na sh. bilioni 890) kwa ajili ya kuharakisha Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini Tanzania (MKUKUTA) ili kufikia malengo ya milenia.
Taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam jana, ilisema azimio hilo lilifikiwa na MCC katika kikao kilichofanyika mjini Washington, Marekani.
“Makubaliano haya (ya MCC) ni uthibitisho wa juhudi za Tanzania katika kuwajengea maisha bora wananchi wake,” Mtendaji Mkuu wa MCC, Balozi John Danilovich alinukuliwa kwenye taarifa hiyo.
Danilovich ambaye aliwahi kutembelea miradi ya MKUKUTA hapa nchini Januari mwaka huu, alisisitiza umuhimu wa Tanzania kupatiwa msaada mkubwa wa kifedha ili kufanikisha malengo thabiti iliyojiwekea.
Aliwapongeza Watanzania kwa kuwa na mpango makini na endelevu katika kukuza uchumi kama vile kuimarisha miundombinu, upatikanaji wa nishati ya kudumu na maji salama.
“Kipaumbele cha Tanzania kuwekeza katika sekta ya miundombinu, nishati na maji, itakuwa ni kichocheo cha kupunguza umasikini na kusababisha uchumi kukua,” alisema Balozi Danilovich.
Alisema lengo la MCC la kutoa msaada wa fedha kwa Tanzania kutafanikisha mikakati ya ukarabati wa barabara na kuwezesha mawasiliano mazuri ya kwenda kwenye masoko, shule, hospitali, vituo vya afya, zahanati na hivyo kuongeza fursa za kibiashara na kilimo.
“Kupitia kwenye haya malengo ya milenia, Wamarekani wanaona fahari kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za kupunguza umasikini na kuboresha maisha ya wananchi,” alifafanua Danilovich.
Alisema kuidhinishwa kwa msaada huo ni sehemu ya makadirio kwa mwaka wa fedha 2008 wa MCC katika kutekeleza mikakati yake.
Balozi Danilivich alisema Tanzania ni nchi pekee iliyopewa sehemu kubwa ya misaada ya MCC kuliko nchi nyingine 16, wanachama wa ushirika huo.
Nchi nyingine wanachama wa MCC ni Madagascar, Cape Verde, Honduras, Nicaragua, Georgia, Armenia, Vanuatu, Benin, Ghana, Mali, El Salvador, Msumbiji, Lesotho, Morocco na Mongolia.
MCC ni ushirika ulioundwa na serikali ya Marekani kwa ajili ya kuzisaidia nchi masikini duniani, kuimarisha uongozi bora, uwezo wa kujitegemea kiuchumi na uwekezaji ambao unaimarisha uchumi na uondoaji umasikini.
Wakati huohuo, serikali ya Japan imetia saini makubaliano ya kutoa msaada wa sh. bilioni 25.6 kwa Tanzania ili kufanikisha MKUKUTA na kupambana na ugonjwa wa ukimwi.
Makubaliono hayo kwa niaba ya serikali ya Japan, yalitiwa saini jana jijini Dar es Salaam na Balozi wa nchi hiyo hapa nchini, Makoto Ito na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Grey Mgonja.
Ito alitaja moja ya mambo yaliyoshawishi utoaji wa msaada huo kuwa ni juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kupambana na ukimwi na kuondoa umasikini.
“Julai mwaka huu nilifurahi sana nilipohudhuria hafla ya kitaifa ya kupima virusi vya ukimwi iliyozinduliwa na Rais Kikwete,” alisema Ito.
Aliongeza kuwa kitendo cha Rais Kikwete kupima ukimwi katika uzinduzi huo kinaonyesha jinsi alivyokusudia kupambana nao na kinadhihirisha kwa vitendo umahiri wake katika kuongoza.
Ito alisema ana imani kuwa serikali ya Tanzania itatumia fedha hizo kulingana na makubaliano ili kutekeleza lengo la kuimarisha uchumi na kuondoa umasikini.
Kwa upande wake, Mgonja alifafanua kuwa kati ya sh. bilioni 25.6 zitakazotolewa na Japan, sh. bilioni 21.8 ni kwa ajili ya kutekeleza MKUKUTA wakati sh. bilioni 3.8 zitachangia kwenye vita dhidi ya ukimwi.
Mgonja alisema miradi yote itaelekezwa katika maeneo ya vijijini kwa kuwa ndiko kwenye hali mbaya.

Uhuru

No comments: