Saturday 15 September 2007

Mudhihir akatwa mkono


Mudhihir akatwa mkono

*Ni kutokana na ajali ya gari iliyotokea Lindi
*Ahamishiwa kitengo cha MOI kwa matibabu
*Lowassa, mawaziri na wabunge wamjulia hali

Na Reuben Kagaruki
MBUNGE wa Mchinga, Bw. Mudhihir Mudhihir (CCM), amekatwa mkono wa kulia uliosagwa na gari alilokuwa akiendesha na kupinduka.
Ajali hiyo ilitokea juzi jioni eneo la SIDO mkoani Lindi ambapo inadawa Mbunge huyo alikuwa akijaribu kumkwepa mwendesha baiskeli.

Katika gari hilo inadaiwa alikuwa na mdogo wake aliyetajwa kwa jina moja la Ramadhan lakini yeye hakupata majeraha.
Bw. Mudhihir alisafirishwa kwenda Dar es Salaam jana kwa ndege ya kukodi, akitokea hospitali ya Misheni ya Nyangao, Lindi Vijijini na kukimbizwa moja kwa moja kwa matibabu zaidi katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) ambako amelezwa akiendelea na matibabu.

Akizungumza jana na gazeti hili Ofisa Muuguzi Daraja la Pili wa MOI, Bw. Francis Chilumba, ambaye alimsindikiza Bw. Mudhihir kutoka Nyangao hadi Dar es Salaam, alisema alipokewa katika hospitali yao saa mbili usiku akitokea hospitali ya mkoa wa Lindi ya Sokoine ambako alipewa matibabu ya awali.
"Baada ya kufikishwa hospitalini kwetu alionekana mkono wake umesagika na baada ya kupigwa X-ray ulionekana umeumia mno," alisema Bw. Chilumba.

Alisema madaktari wa hospitali hiyo walijadiliana kwa muda mrefu na kuafikiana kuukata ili kuokoa maisha yake. "Madaktari waliamua kuuondoa mkono wote, ili kuokoa maisha ya mgonjwa," alisisitiza Bw. Chilumba kuhusu mkono huo ambao umekatiwa juu ya kiwiko.
Alipoulizwa kuhusiana na hali ya Bw. Mudhihir tangu walipotoka Lindi hadi kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K. Nyerere, Bw. Chilumba alisema haikuwa mbaya, isipokuwa mara kwa mara alikuwa akilalamikia maumivu.

Akizungumza na watu waliokwenda kumjulia hali akiwamo Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa, ambaye alifika MOI saa 9 alasiri, Bw. Mudhihir alisema kwa wakati huo hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri.
"Msihofu kwa kuwa niko hapa, basi nimepona," alisema Bw. Mudhihir na kuongeza: "Hii ni kazi ya Mungu." Alisema viungo vyote viko salama isipokuwa anasikia maumivu makali kwenye mkono uliokatwa.
Alimwambia Bw. Lowassa kuwa anaishukuru Serikali kwa kutuma ndege haraka ili kumchukua kutoka Lindi na kumleta Dar es Salaam kwa matibabu muhimu.

Kwa upande wake, Bw. Lowassa aliwaambia mawaziri na wabunge waliofika hospitalini kumjulia hali: "Nimemwona na anatia moyo."

Wengine waliofika hospitalini hapo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Hawa Ghasia na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Bw. Emmanuel Nchimbi.

Wengine ni Mbunge wa Kinondoni, Bw. Idd Azzan, Mbunge wa Mafia, Bw. Abdulkarim Shah, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Bw. Mohamed Sinani na Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Anna Abdallah.

Jina la Mudhihir limekuwa kwenye 'midomo' ya wapinzani katika siku za karibuni, baada ya kutoa mapendekezo ya kumsimamisha kazi Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), kwa tuhuma za kusema uongo bungeni dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Nazir Karamagi. Bw. Zitto alisimamishwa kazi kwa miezi sita.

Hatua hiyo ilifikiwa kutokana na Bw. Kabwe kutoa hoja binafsi bungeni akitaka iundwe Kamati Teule ya kuchunguza hatua ya Waziri Karamagi kusaini mkataba wa mgodi wa Buzwagi nje ya nchi.

Hata hivtyo baada ya Bw. Kabwe kusimamishwa kazi, yeye na wapinzani wenzake wamekuwa wakizunguka sehemu mbalimbali nchini kuelezea sababu za kusimamishwa kwake huku wakimlaumu Bw. Mudhihir kwa kutoa mapendekezo yaliyomfikisha katika adhabu hiyo.

source; majira

No comments: