Saturday 15 September 2007

Msuya 'bosi' Chuo Kikuu cha Ardhi

Rais awateua Mwinyi, Msuya wakuu wa vyuo
NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete, amemteua Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Muhimbili.
Sambamba na uteuzi huo, Rais pia amemteua Waziri Mkuu mstaafu Cleopa Msuya, kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi.
Taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla, ilisema viongozi hao wameteuliwa kuongoza vyuo vikuu hivyo vipya ambavyo kabla ya Julai, mwaka huu vilikuwa vyuo vikuu vishiriki vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Msolla alisema, mbali na Mwinyi na Msuya, Rais pia amewateua Waziri wa zamani wa Elimu, THabitha Siwale kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Ardhi na Deogratius Ntukamazina kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Muhimbili.
Kwa upande wa makamu wakuu wa vyuo, Profesa Kisali Pallangyo ataongoza Muhimbili wakati Profesa Idrisa Mshoro ataongoza Ardhi. Kabla ya uteuzi, Profesa Pallangyo alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Afya Muhimbili na Profesa Mshoro alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Uhandisi na Teknlolojia cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Katika uteuzi huo pia, Rais amewateuwa Profesa David Ngassapa kuwa Naibu Makamu Mkuu (Taaluma, Utafiti na Ushauri) na Profesa Bakari Lembariti kuwa Naibu Makamu Mkuu (Mipango, Fedha na Utawala) katika Chuo Kikuu cha Muhimbili.
Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Ardhi walioteuliwa kuwa manaibu makamu wakuu wa vyuo ni Profesa Mengiseny Kaseva (Taaluma, Utafiti na Ushauri) na Profesa Eleuther Mwageni (Mipango, Fedha na Utawala).
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Ngassapa alikuwa Mkurugenzi wa Mipango katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Muhimbili na Profesa Lembariti alikuwa Mrajisi wa Chuo hicho.
Naye Profesa Kaseva alikuwa Kaimu Mkuu wa kilichokuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi na Usanifu Majengo, na Profesa Mwageni alikuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma ya Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Morogoro.
Uteuzi wa viongozi hao, kwa mujibu wa taarifa ya Profesa Msolla, unaanza Septemba 11, mwaka huu.
source: Uhuru

No comments: