Monday 17 September 2007

Serikali yafanya kweli

Naipongeza serikali ya JK kwa hili!
By Mosonga.

Marufuku `supermarket` kuuza mboga za nje-Wasira

17 Sep 2007
By Richard Makore

Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imepiga marufuku maduka makubwa ya bidhaa mbalimbali maarufu kama supermarkets, kuagiza mboga za majani kutoka nje na kuuza nchini.

Waziri wa wizara hiyo, Bw. Stephen Wasira, alitangaza hatua hiyo jana jijini Dar es Salaam na kuwataka wenye maduka hayo kuuza mboga za majani zinazozalishwa na wakulima wa hapa nchini.

`Wanunue zinazolimwa na wakulima wa ndani ili kuinua kipato chao.` Aliagiza Bw. Wassira alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Bw. Wasira alisema, baadhi ya wawekezaji wenye maduka makubwa wamekuwa wakiagiza vitu mbalimbali kutoka nje kwa ajili ya matumizi ya kawaida hata vile vinavyopatikana kwa wingi humu nchini.

Aidha, Waziri alisema, serikali iko mbioni kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo inakuwa ya kibiashara zaidi na yenye manufaa kwa wakulima .

Alisema katika hatua za awali za kufikia lengo hilo watalaamu 2,500 wanatarajiwa kuajiriwa na kusambazwa vijijini ili kuwaelekeza wakulima mbinu za kilimo cha kisasa.

Alisema kilimo hakiwezi kuboreka ikiwa hakutakuwa na mipango maalumu ya kukiboresha ikiwa ni pamoja na kutumia watalaamu, mbolea ,mbegu bora , zana za kilimo na wanyama kazi.

`Kilimo hapa nchini hakiwezi kumsaidia mkulima kama ataendelea kutumia njia za kizamani katika kulima`, alisema.

Bw. Wasira aliwahimiza wakulima kutumia mbolea ili wapate mavuno mengi.

Alisema serikali itawatumia wananchi waliopo vijijini kama mawakala wa kuuza mbolea badala ya utaratibu wa sasa ambapo kazi hiyo inafanywa na makampuni makubwa.

Bw. Wasira alifafanua kuwa licha ya serikali kuyalipa makampuni hayo gharama za usafirishaji wa pembejeo kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani bado yameshindwa kuziuza kwa bei ya nafuu ili kuwawezesha wakulima kuzinunua.

Aliongeza kuwa, serikali imetenga Shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuwapatia mafunzo mawakala wa kuuza pembejeo vijijini.

Aliendelea kusema kuwa makampuni hayo yameshindwa kazi kwa kuwa maeneo mengi wakulima wanalalamikia suala la kucheleweshewa pembejeo.

Ili kuondoa usumbufu huo kila mkulima atapewa kadi maalumu itakayomwezesha kununua mbolea na pembejeo kwa bei nafuu na kwa wakati.

Alisisitiza kuwa, kama mipango ya wizara yake itasimamiwa ipasavyo itaweza kumsaidia mkulima kujikomboa kutoka katika umasikini na kuingia kwenye maisha bora.

* SOURCE: Nipashe

No comments: