Thursday 8 May 2008

'Ruti' zaidi za daladala Dar

Njia mpya za daladala zaongezwa D`salaam
(Nipashe, 2008-05-08 10:31:51. Na Anneth Kagenda)
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi kavu (SUMATRA) imetangaza kuanzishwa safari mpya za daladala jijini Dar es Salaam. Mfumo huo mpya utahusisha njia ndefu, fupi na zile za kati na kwamba nyongeza hiyo imezifanya ruti za daladala jijini kufikia 130. Lengo la kuongeza njia mpya za daladala ni kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji.

Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki Bw. Walukani Luhamba, alisema jana kuwa kuanzia sasa kutakuwa na daladala zinazosafiri kati ya:

1. Kimara na Buguruni kupitia barabara za Morogoro na Mandela.
2. Kimara hadi Kawe kwa kupitia barabara ya Morogoro na Sam Nujoma.
3. Ukonga hadi Stesheni kupitia barabara za Nyerere na Uhuru.
4. Ukonga hadi Mbagala kupitia barabara ya Nyerere,
5. Mwananyamala na Mabibo.
6. Tegeta hadi Kawe kupitia barabara ya Bagamoyo na
7. Kawe hadi Buguruni kupitia barabara ya Kawawa.

Bw. Luhamba alisema zoezi hilo linakwenda pamoja na usajili wa magari madogo ya abiria Hiace maarufu kama 'vipanya' ambayo yatakuwa na ruti fupi fupi.

Alisema magari yatakayosajiliwa katika njia ndefu ni yale mabasi makubwa yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 25 ambayo yatafika hadi pembezoni mwa jiji.

Bw. Luhamba alisema njia hizo mpya zitaanza kufanyakazi kuanzia wiki ijayo na tayari baadhi ya magari yameshasajiliwa kwa kutumia njia hizo.

No comments: