Tuesday 10 November 2009

Mikosi safarini

Nikiwa njiani na wenzangu toka Kigoma, baada ya kuupita kidogo mji wa Urambo tulipata ajali baada ya gari yetu kupasuka tairi (tyubu ya tairi) ya mbele upande wa dereva. Gari ilikuwa na mwendokasi wa kama 100km/hr na tulikuwa kwenye kona ndipo gurudumu hilo likapasuka. Tukaanza kuyumba kwa umbali mrefu kidogo huku dereva akijitahidi kurekebisha mambo yasiwe mabaya zaidi! Ndipo baadae kidogo likaserereka na kuingia mtaroni na kuegemea ukuta wa nje wa mtaro kwa kishindo. Wanakijiji wa eneo lile walisikia mlio wa tairi (tyubu) kupasuka na kishindo cha gari kugonga gema la barabara na mara moja wakakimbia kuja eneo la tukio na walishangaa kukuta tuko nje ya gari tayari na tuko salama!

Ilikuwa ajali mbaya na tunamshukuru Aliye Juu kwa kutuepushia madhara makubwa. Gari ilibondeka upande wa dereva mbele hadi nyuma.

Wanakijiji walitusaidia kuinyanyua gari na kuisukuma nje ya mtaro mkubwa wa barabara. Shughuli yote hii ilidumu kwa saa 3 na ushee. Ni nguvu za binadamu tu zilitumika hapa kuiondoa gari mtaroni, wenye magari wote walipiata bila msaada wowote, sana sana labda wale walioulizia kama wamesalimika wasafiri wa hilo gari!

Tukabadili gurudumu (tulikuta ile tyubu iliyosababisha ajali imechanika vipandevipande!! Imetengenezwa China!!!!!!!!!!!!!!!!!!!! Yaogopeni magurudumu (tubes)ya China kama ukoma).

Mafuta ya gari yalimwagika karibu robotatu ya tenki -kutokana na gari kulala kwenye tuta). Lilipotengamaa matengenezo madogo tukapumzika kidogo na baadae tukaianza safari kulekea Tabora.

Kwa bahati mbaya tena tairi iliyowekwa nayo ilipata pancha tukiwa eneo la Shelui mpakani mwa Tabora na Singida, ila safari hii tulisimama salama na kulibadili na kisha kuelekea Singida.

Mikasa na mikosi ilikuwa mingi. Hapa nimesimulia kidogo tu!

Ama kweli ilikuwa ni safari yenye mkosi*.
.................................................

*kichwa cha habari cha kitabu cha 'tujifunze lugha yetu' (kiswahili) cha darasa la tano, enzi zangu!

No comments: