Tuesday, 10 November 2009

Kigoma ni kiboko

Nakumbuka wakati nikiwa JKT Luwa, watani wangu Waha walikuwa wakitaniwa kwa ushamba wao:
1. Mwanza ni mji lakini Kighoma ni kibhoko!!
2. Kighoma taa zinawaka kwenye chupa! (yaani Bulb)

Kwa mara ya kwanza nimefika na kukaa kidogo mji wa Kigoma! Kumbe mji huu uko juu ya milima na mabonde ya huku na huko. Uwapo juu ya kilima (hasa Milimani Lodge waweza kuliona vema ziwa Tanganyika na eneo la Kinyirizi). Pia kuna hoteli nzuri sana ya kitalii inaitwa Lake Tanganyika (Beach). Hotel hii ni kiboko. Nasikia ni mali ya mwekezaji mzalendo toka mkoa wa Mbeya! Hongera sana 'Mnyaki' kwa hicho kitu!!!

Hotel au nyumba nyingi za wageni zinatumia jina la Zanzibar; Zanzibar Lodge, Zanzidar Inn, Zanzibar ya Chini, Z'bar ya Juu n.k.

Ardhi ya Kigoma ina rutuba na kwa kweli ni pazuri kimandhari, na hata maendeleo nayo si haba -yapo. Nguo za kina mama hasa vitenge vinatoka nchi jiarani ya DR Congo. Vipande 3 vinaanzia sh. 13,300/=, na vya 'phoenix' (Trade Mark) viko kwenye sh. 25,000/= au zaidi.

Upatapo nafasi tembelea mji wa Kigoma na ikiwezekana jitahidi ufike Lake Tanganyika Beach Hotel. Chumba ni sh 70,000 hadi 80,000 kwa siku. Pia tembelea soko lao maarufu pale karibu na stesheni ya treni na lile liitwalo Mwanga (hili liko juu kidogo ya kilima kabla hujatelemka kuingia mwisho wa reli).

Hongereni sana wana-Kigoma.

No comments: