Saturday 27 December 2008

Uaminifu Posta TZ ni kiduchu!!

Serikali inafanya nini kuhusu wizi katika posta nchini Tanzania? Hata barua za kawaida zinaibiwa na kufunguliwa na wafanyakazi wa posta.

Nimewaandikia ndugu zangu mara nyingi na, kila mmoja wao, wamesema barua pamoja na picha nilizowatumia hazikuwafikia. Na wote wameniambia nisithubutu kuwatumia kitu chochote kupitia posta nchini Tanzania. Na mmoja wao amesema wananchi wengi wanasema itakuwa ni vizuri posta zikifungwa kwa sababu ya wizi huo ambao unaendelea kwa kasi.

Malalamiko hayo yanatoka sehemu zote za Tanzania. Ndugu zangu niliowaandikia wanaishi sehemu mbali mbali - Dar es Salaam, Mtwara, Iringa, Mbozi, Mwanza, Bukoba, Tabora, na Arusha.

Hakuna posta nchini ambayo haina wafanyakazi wanaoiba vitu mbali mbali - barua, vifurushi - vinavyotumwa kutoka n'gambo. Pia wana akili pungufu wanapofikiri kwamba kuna fedha katika barua hizo wanazozifungua.

Labda wananchi wakigoma kutumia posta, hatua zitachukuliwa kupambana na wizi huo.

Nimeishi n'gambo miaka michache (au mingi?) - zaidi ya kumi - na ni jambo la kukatisha tamaa kwa watu kama mimi tunaotaka kurudi nyumbani tunapoona serikali haifanyi chochote kurekebisha mambo - wizi, rushwa, mahongo, ufisadi na kadhalika.

Tutajengaje taifa letu? Kama Mwalimu alivyosema, "Tanzania itajengwa na wenye moyo."

Haitajengwa na wezi. Haitajengwa na wala rushwa au mahongo, na haitajengwa na mafisadi. Wamejaa serikalini na katika kila wizara na idara na sehemu mbali mbali kazini.

Halafu kuna viongozi wanashangaa kwa nini wananchi wengi hawataki kurudi nyumbani? Si Tanzania tu bali nchi zote katika bara letu. (chanzo: jamii-forum)

No comments: