Tuesday, 9 December 2008

Reginald Mengi vs. 'Vitisho'

Hivi karibuni, Reginald Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), alikaririwa akisema, ameanza kuandamwa na vitisho dhidi ya maisha yake.

Kwa mujibu wa Mengi, kuandamwa huko kumetokea baada ya watu wasiojulikana, kumtumia ujumbe wa maandishi kwa njia ya simu, ukimtaja kuwa kinara wa mapambano dhidi ya ufisadi nchini.

Mengi alishatoa taarifa za vitisho hivyo katika kituo cha polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, alisema vitisho hivyo haviwezi kamwe kumkatisha tamaa na kumfanya aache kutetea haki na kupambana na vitendo ya ufisadi.

Vitisho dhidi ya Mengi, vilitumwa kwa ujumbe wa maneno kupitia simu ya mkononi, yenye namba 0768 373967.

Ulisomeka hivi: ``Ni afadhali kunyofoa roho yako ipotee kuliko kuendelea kukuachia uchafue amani na utulivu wa nchi kwa tamaa zako za kutaka urais.``

Ujumbe mwingine alisomeka, "Unachafua sana amani ya nchi kwa uchochezi wako. Tunajua unawahonga wahariri wote na kukusujudia kama Mungu mtu.
Unapenyeza sumu kali ya uzandiki watu waichukie serikali.
Hivi yakitokea machafuko wewe utasalimika?"


``Wewe ni mnafiki mkubwa, unajifanya upo karibu na `Government` (serikali) kumbe ni mnafiki wa kutisha. Jihadhari lazima tukumalize!``

Pia, Mengi alisema kuna waziri mmoja kijana katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ameshaanza kuandaa mikakati ya kumhujumu kibiashara.

Ingawa hakumtaja kwa jina, lakini Mengi alisema waziri huyo anaongoza wizara nyeti na kwamba alitoa pendekezo hilo katika kikao kinachotambulika, akitaka kuona (Mengi) anafilisiwa kama alivyofanyiwa tajiri mmoja mkubwa nchini Urusi.

Siku chache baadaye, Masha alijitokeza hadharani na kupitia waandishi wa habari, alimtaka Mengi kuthibitisha madai ya kuwepo waziri anayefanya njama za kutaka kummaliza kibiashara, kwa kumbambikizia kodi kubwa, ili ashindwe kulipa na baadaye afilisiwe.

Masha ambaye ni mmoja wa mawaziri vijana katika Baraza la Mawaziri wa serikali ya awamu ya nne, alijitokeza na kumpa Mengi siku saba kutoa ushahidi wa madai yake na kusema akishindwa kuthibitisha, atachukuliwa hatua.

SOURCE: Nipashe, 09/12/2008

No comments: