Monday 20 August 2007

Kujiajiri: Napenda watu wenye ubunifu kimaisha

Mimi binafsi nina kiu kujikita katika maisha ya kujiajiri na ninafurahi sana ninapowaona watu wengine ktk nafasi zao wakifanya shughuli zao binafsi kujiletea kipato kimaisha.
Mhe Ditto amenipa changamoto kwa mawazo yake hapa chini. Pia mzee Reginald Mengi nae ni mfano wa kuiga. Alianza maisha kwa kujaza wino ktk mirija ya kalamu za wini maarufu kama 'Epica' pale Pugu Road (siku hizi ni Nyerere Road) enzi hizo nikiwa nasoma elimu ya msingi, miaka ya 1980. Leo hii Mzee Mengi amepiga hatua kubwa sana kimaisha na kibiashara.
Na Mosonga.


Dito sasa muuza asali
20 Aug 2007By Lucas Raphael, PST Tabora
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, ameamua kuwa mfanyabiashara wa asali, baada ya kupoteza nafasi ya ukuu wa mkoa kutokana na kukabiliwa na kesi ya mauaji.
Hivi sasa Bw. Ditopile yupo mjini hapa akiishi katika nyumba ya kulala wageni, ambapo inaelezwa kuwa ananunua asali na kuisafirisha jijini Dar es Salaam na kisha kuiuza.
Bw. Ditopile alimweleza Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Bw. Reginald Mengi aliyetembelea mkoani hapa mwishoni mwa wiki kwamba ameamua kuwa mfanyabiashara ili kukabiliana na ukali wa maisha.
Alisema baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kujishughulisha na kazi yoyote ameona ni bora afanye biashara hiyo ili aweze kujipatia kipato yeye na familia yake.
`Mhe. Mengi karibu sana Tabora kwenye mito ya asali, iliyojaa neema. Kama unasikia nchi ile ya ahadi nchi ya Kanani ndio Tabora kwa hiyo karibu sana,` alisema Bw. Ditopile.
Aidha Bw. Ditopile aliwataka vijana kuwa wabunifu wa biashara kabla ya kwenda katika taasisi zinazojishughulisha na kazi ya kutoa fedha ya mikopo kwa wajisiriamali kwa ajili ya kuanzisha biashara.
Hata hivyo haikuweza kufahamika mara moja iwapo, Bw. Ditopile ameamua kurejea Tabora kufanya makazi yake ya kudumu au la. Baadhi ya watu, hususani vijana mjini hapa wamekuwa wakimshangilia huku kila mmoja akitaka ashikane naye mkono wakati akiwa katika matembezi yake.
* SOURCE: Nipashe


Vyuo vya juu vyatakiwa kubuni mitaala ya ajira
20 Aug 2007By Mariam Samiji, PST Dodoma
Waziri wa Sayansi , Teknolojia na Elimu ya Juu, Profesa Peter Msolla, amevitaka vyuo vya elimu ya juu kubuni mitaala inayokidhi soko la ajira la ndani na nje ya nchi. Kadhalika amesema iwapo wataanza mitaala na kuona kuwa haina manufaa kwa ajira za wanafunzi hakuna haja ya kuendelea kufundisha kozi zake. Alitoa ushauri huo kwa wanajumuiya wa vyuo vya elimu ya juu vya Mkoa wa Dodoma alipovitembelea mwishoni mwa wiki iliyopita. Aliongeza kuwa changamoto kwa vyuo vya elimu ya juu ni kubuni mitaala ambayo itakidhi mahitaji ya jamii katika soko la kazi na sio wanafunzi kuhitimu na kuhangaika mitaani bila kuwa na cha kufanya. Alisema itakuwa haileti picha nzuri maana wanafunzi wanahitimu kozi waliyosomea lakini inakuwa ni vigumu kupata ajira ndani na nje ya nchi. Aliwashauri wakuu wa vyuo kufuatilia mwenendo wa wanafunzi mara wanapomaliza vyuo ili kuona wameishia wapi na endapo wamepata ajira ni muhimu zaidi kufuatilia utendaji wao na kufahamu jinsi wanavyofanya kazi. Waziri huyo alitembelea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini na Chuo cha Mtakatifu Johns. Akiwa UDOM alipongeza uongozi na kusema ameridhishwa na hali ya ujenzi inayoendelea chuoni hapo kwani hatua iliyoofikiwa ni kubwa pamoja kwamba imeanza kwa muda mfupi. Kwa wanajumuiya wa Chuo cha Mipango, Waziri alisema asasi za elimu ya juu kwa sasa zinakabiliwa na changamoto kubwa na kuwataka wahadhiri kufanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu.
* SOURCE: Nipashe

No comments: