Tuesday 7 August 2007

Dar: Gharama za vyakula zapanda

Gharama za vyakula Jijini zapanda
07 Aug 2007
By Valery Kiyungu
Wakati wananchi wakilia na kupandishwa kwa nauli za mabasi kote nchini, wafanyabiashara katika masoko mbali mbali Jijini Dar es Salaam, pia wamelalamikia ongezeko la gharama za usafirishaji wa bidhaa kutoka mikoani. Kwa nyakati tofauti wamesema ongezeko hilo linatishia kuongezeka kwa bei ya bidhaa mbalimbali sokoni.
Mfanyabiashara wa mchele Bw. Saidi Ngalawa amesema, kupanda huko kwa gharama za usafirishaji wa bidhaa kutoka mikoani, kulianza kujitokeza wiki iliyopita, mara baada ya kutangazwa kwa ongezeko la nauli za mabasi kwa nchi zima. Akasema, kabla ya kupanda kwa nauli za mabasi alikuwa akilipia shilingi 60,000 kwa ajili ya kusafirisha tani moja ya nafaka kutoka Mbeya hadi Dar, lakini sasa kiwango hicho hicho cha mzigo husafirishwa kwa shilingi 75,000.
`Gharama zimepanda kwa kiasi kikubwa kwani awali haikuwa hivyo,` alisema Bw.Ngalawa ambaye pia ni Katibu Mkuu Msaidizi wa soko la Tandale. Bw. Ngalawa amesema kutokana na kupanda kwa gharama za kusafirisha nafaka, hivi sasa anafanya biashara kwa hasara, na kwamba upo uwezekano mkubwa wa kupandisha bei za nafaka. `Tunafanyabiashara kwa hasara hivyo tunakusudia kupandisha bei ya mchele ili twende sambamba na makali ya bei za nauli,` akasema.
Mfanyabiashara mwingine katika soko la Manzese, Bw. Saadi Kinyogoli alisema, ongezeko la gharama za usafirishaji limepanda kwa kiasi kikubwa, ambacho hakijawahi kutokea kwa muda mrefu.
Naye Bw.Denis Mbele wa soko la Mabibo amewaomba wenye magari ya kusafirisha bidhaa toka mikoani wapunguze bei ya nauli wanazotoza hivi sasa, kwa maelezo kuwa zinawaumiza mno wafanyabiashara masokoni. `Wamepandisha kwa kiasi kikubwa mno, watupunguzie ili nasi tuweze kuuza kwa bei ambayo walaji wataimudu,` akasema Bwana Mbele. Wafanyabiashara wengine waliolalamikia ongezeko hilo la gharama za usafirishaji ni Bi. Aisha Omari wa soko la Kinondoni na Bwana Hussein Nassoro wa soko la Ilala.
* SOURCE: Alasiri

No comments: