Saturday 12 July 2008

Ze Komedy

Sakata hili baina ya 'ze komedi' na eatv/itv linaweza kuamliwa kisheria kwa kuzingatia mkataba kati ya pande hizo mbili.

Kama eatv/itv iliwaalika waigizaji hao kivyaovyao (bila kuwa kikundi rasmi kinachojulikana) na kuwapa kazi ya kuigiza na kisha kuanzisha jina la 'ze komedi' wakiwa tayari ndani ya eatv/itv, basi haki miliki ya jina hilo linabaki kuwa la eatv/itv.

Lakini kama itv/eatv iliwaita waigizaji wakiwa tayari kama kikundi kinachojulikana kama 'ze komedi', basi wanakikundi wana haki kuhama na kuigiza ktk kituo kingine cha tv kwa kutumia jina lao la 'ze komedi'.

Hayo ndio mawazo yangu.

Kuna mifano mitatu napenda kuitoa hapa (imetokea Uingereza);
1. Mchekeshaji Paul O'grady alikuwa na shoo ktk kituo cha itv, Paul O'grady Show, kutokana na sababu fulani fulani Paul alihamia Channel4 miaka miwili iliyopita. Ktk Channel4 alitumia jina jipya The new Paul O'grady show. Kwa hiyo jina lilibadilika, japo kidogo.

2. Dada mmoja, mwendesha kipindi cha watu na maisha, alikuwa na shoo yake ktk tv (itv) ikiitwa Trisha. Nae kwa sababu zisizozuilika ilibidi abwage manyanga na kuhamia kituo kingine cha tv kiitwacho Five. Huko Five alikohamia alibadili jina na kutumia jina jipya la Trisha Goddad.

3. Mzee Parkinson alikuwa na shoo ktk BBC one ikiitwa Parkinson na baadae akahamia itv, lakini yeye hakubadilisha jina la shoo - aliendelea kutumia jina lilelile 'Parkinson'.

Kitu cha msingi ktk hali kama hizi ni yale makubaliano kati ya wahusika pamoja na maandishi madogo (small prints), wenyewe wanaita kwa kifupi T&C*. Kutokana na makubaliano hayo ndipo itajulikana endapo jina libaki eatv au lihame na waigizaji!

Tatizo la kutosoma au kutozingatia maandishi madogo/small prints kabla ya kutia sahihi ktk mikataba ndilo pia linalotusumbua hata ktk mikataba mikubwa nchini, mfano mikataba ya madini, ITCL, Richmond n.k.


..........................
*T&C -Terms and Conditions
..........................

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

(source: majira 11/07/2008)
Waandishi: Kulwa Mzee, Dodoma na Grace Michael, Dar

*Kesi yao dhidi ya EATV kusikilizwa Jumatano
*Mengi asema hana chuki nao na anawapenda

SAKATA la kikundi maarufu cha uchekeshaji cha 'Ze Comedy' na Kampuni ya East Africa Televisheni (EATV), limeibukia bungeni ambapo Serikali imesisitiza kuwa kina haki ya kwenda Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwani mkataba wao wa awali ulishamalizika.

Sakata hili liliibuka jana, baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Bi Suzan Lyimo (CHADEMA), kuitaka Serikali kutoa tamko juu ya kundi hilo, ambalo ni kipenzi cha wananchi.

Mbunge huyo alitaka kujua hayo alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, aliitaka pia Serikali kueleza sababu za kikundi hicho kuzuiwa maonesho yake.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Bw. Joel Bendera, alisema Serikali inalifahamu tatizo lililopo kati ya 'Ze Comedy' na EATV.

Hata hivyo, alisema Serikali imekiagiza Chama cha Hatimiliki (COSOTA), kukaa na wahusika wote kulimaliza tatizo hilo.

“'Ze Comedy' wana hatimiliki na EATV nao wana hatishiriki, 'Ze Comedy' wamemaliza mkataba wao na EATV, wana haki ya kwenda TBC ... hivi karibuni tatizo hili litakwisha,” alisema Bw. Bendera.

Awali, Bw. Bendera alikiri kuwapo tatizo la COSOTA kutekeleza majukumu yake, ikiwamo kushughulikia matatizo yanayowakabili wasanii na kusisitiza kwamba Serikali itajitahidi kukiimarisha chombo hicho, kwa lengo la kuwasaidia wasanii hasa katika kupigania haki zao.

Bw. Bendera alisema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maaluumu, Bibi Martha Mlata (CCM), aliyeuliza iwapo Serikali ina mpango wa kuisaidia COSOTA kifedha, ili iweze kusimamia vyema kazi za wasanii, baada ya kuonesha chombo hicho kushindwa kufanya kazi zake kutokana na kutokuwa na fedha.

Wakati huo huo, kesi iliyofunguliwa na 'Ze Comedy' dhidi ya EATV, Msajili wa Nembo za Biashara na COSOTA, inatarajiwa kusikilizwa Jumatano mchana Katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara.

Hatua hiyo ilifikiwa jana baada ya walalamikiwa katika kesi hiyo, kuwasilisha ombi la kuongezwa muda wa kujibu hati ya madai iliyowasilishwa na kikundi cha wasanii hao kupitia wakili wao, Bw. Peter Swai.

Kwa ombi la walalamikiwa la kuongezwa muda ambalo liliwasilishwa kupitia wakili wao, Bibi Blandina Gogadi, upande wa wadai nao uliiomba mahakama kutoa kibali cha kuendelea na biashara yao, huku upande wa walalamikiwa ukiendelea kujibu maombi hayo.

Baada ya Jaji Catherine Urio kukutana na pande zote mbili, walikubaliana kusikilizwa kesi hiyo Jumatano mchana katika mahakama ya wazi, ili kila mtu aweze kuisikiliza.

Wasanii hao walifika mahakamani hapo ili kujua hatma ya kesi yao, ambapo mmiliki wa EATV, Bw. Reginald Mengi naye alihudhuria.

Akiwa mahakamani hapo, Bw. Mengi alikutana faragha na vijana hao huku akisema hana chuki nao na anawapenda.

Wasanii hao waliwasilisha maombi wakiiomba mahakama kuwazuia walalamikiwa kuingilia biashara zao na kuruhusu kutumia jina lao.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyoko mahakamani hapo inaiomba mahakama hiyo kutoa tamko kuwa walalamikaji hao ni wamiliki wa jina la 'Ze Comedy' kabla na baada ya kuingia makubaliano na walalamikiwa.

Mbali na maombi hayo, pia wasanii hao wanaiomba mahakama hiyo kuamuru walalamikiwa hao kulipa fidia ya sh. milioni 200 kama adhabu kwa usumbufu waliowasababishia.

Walalamikaji hao wanaiomba mahakama kuwaruhusu kuendelea na biashara yao huku kesi ya msingi ikiendelea, ambayo ni kuthibitisha madai ya walalamikiwa, wanaodai kuwa wao ndio waliounda kikundi hicho na wamiliki halali wa nembo ya 'Ze Comedy'.

Maombi hayo yataanza kusikilizwa mahakamani hapo Jumanne saa 4 asubuhi mbele ya Jaji Catherine Urio.

Hati ya walalamikaji iliyopo mahakamani hapo inadai kuwa wao ni kikundi cha sanaa ambacho kimesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa na kinatimiza taratibu zinazotakiwa katika kazi za sanaa.

Inadaiwa kuwa wasanii hao baada ya kuondoka EATV, kampuni hiyo iliwazuia kutumia jina la kikundi hicho na majina yao ikidai kuwa ndiye mmiliki halali wa nembo hiyo.

Walalamikaji katika kesi hiyo ni Isaya Mwakilasa (Wakuvanga), Mujuni Sylivester (Mpoki), Lucas Muhuvile (Joti), Emmanuel Mgaya (Masanja), Alex Chalamila (McRegan), Joseph Shamba (Vengu) na Sekioni David (Seki).