Friday, 1 August 2008

Kifo cha Mhe Chacha Wangwe (MB)

Tarime wazuia maziko ya Wangwe

MWENYEKITI wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe, amenusurika kauawa kwa mapanga na mishale, baada ya kuwasili katika kijiji cha Kemakorere, kuhudhuria maziko ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake na Mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Wangwe.

Sakata hilo lilianza kujitokeza jana saa nane mchana baada ya Bw. Mbowe kuwasili kijijini hapo akifuatana na viongozi wengine wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Bw. Augustino Mrema (TLP), Bw. Joseph Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Bw. Bob Makani Mwenyekiti mstaafu wa CHADEMA.

Baada ya kuwasili kwa viongozi hao, kundi kubwa la watu hasa vijana walianza kumzonga Bw. Mbowe kwa kumwonesha mabango mbalimbali kuhusu kifo cha Bw. Wangwe wakisema hakitokani na mapenzi ya Mungu bali ameuawa.

Baadhi ya mabango hayo yalisomeka ifuatavyo: 'Tarime bila Wangwe hakuna amani'; 'Hii ni ajali au risasi?'; 'Viongozi bora hufa kwa ajali na risasi, viongozi wasio waadilifu hufa kwa BP'na 'Hadi kieleweke CCM hawana chao, tutakufa tukiilalamikia Nyamongo'.

Mengine yalisema: 'CCM chunguza Richmond na vijisenti, hatutampata kama Wangwe';'Tutakumbuka msimamo, utetezi, ujasiri na hoja zako' na 'Nyota ya Tarime imezimika meseji sent.'

Kutokana na hali hiyo, watu wa usalama wakiongozwa na askari Polisi wa kawaida na wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliwazuia wananchi hao kumzonga kiongozi huyo, lakini hawakufanikiwa kirahisi na hivyo kumlazimisha kuingia uani ambako shughuli za maandalizi ya maziko hayo zilikuwa zikifanyika.

Hatua hiyo ilibadilisha kabisa mazingira ya msiba huo, ambao ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wabunge na wanasiasa, vingozi wawakilishi kutoka Kenya na maelfu ya wananchi.

Hali hiyo ya kutisha ya baadhi ya wananchi kubeba mapanga, mikuki, sime na fimbo huku baadhi yao wakiwa wameziweka hadharani na wengine katika makoti na kujificha migombani, ilimfanya kiongozi wa ukoo huo, Profesa Samwel Wangwe, kuwaeleza baadhi ya viongozi msimamo wa ukoo kabla ya kutangazwa hadharani.

Baada ya maelezo hayo ambayo yalimhusisha pia Mkuu wa Mkoa, Luteni Kanali mstaafu Issa Machibya, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Bw. Liberatus Barlow, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw. Zitto Kabwe na viongozi wengine wa ukoo, iliwabidi kuingia ndani kwa dakika 10 kufanya mjadala wa kuzika au la.

Baada ya muda huo, viongozi hao walitoka nje na Profesa Wangwe kupanda jukwaani na kutoa matangazo ambayo muda wote yalikuwa hayasikiki kutokana na kelele za waombolezaji, wakidai hawamtaki Mbowe bali wanataka Mbunge wao.

Hata hivyo, Bw. Kabwe alionekana kuwavuta wananchi hao kwa kusema maneno ya kumpamba marehemu, kuwa alikuwa kiongozi aliyependa kutetea wanyonge, hasa wapiga kura wake, hivyo kulazimika kunyamaza na kusikiliza kilichokuwa kikielezwa na msemaji huyo wa familia.

Katika kauli hiyo ya ukoo, Profesa Wangwe alisema:
"Sisi kama ukoo baada ya kupokea mwili wa marehemu na kuufikisha hapa, maneno mengi yamesemwa na ili kuondoa maneno hayo, tumeona ni vizuri tukachunguza mwili wa marehemu kwa kutumia mtaalamu wetu ambaye atawasili wakati wowote kuanzia sasa ... naomba sasa tuwe watulivu wakati tukisubiri hatua hiyo na mwili leo hauzikwi,” alisema Profesa Wangwe na kushangiliwa.

Kauli hiyo pamoja ya kuonesha imani kwa wananchi, lakini bado wangine walianza kutoa maneno yaliyolenga kwa Mbowe kuwa "tunataka Mbunge wetu si Mbowe," hali hiyo ilimfanya Mkuu wa Mkoa kusimama na kuomba amani.

Hata hivyo, kauli hizo hazikueleweka kwa wananchi hao hasa vijana, hivyo kumlazimu Mkuu wa Mkoa kuita polisi na kumsindikiza Bw. Mbowe katika gari lake, ambapo pamoja na ulinzi huo mkali, bado wananchi hao walimfuata hadi alipoingia ndani ya gari na kusindikizwa kwa ulinzi mkali kuelekea Tarime na hatimaye Musoma.

Pamoja na Bw. Mbowe, viongozi wengine waliohudhuria msiba huo wakiwamo wa Kenya, kila mmoja aliondoka kivyake wakihaha kutafuta magari ya kuwavusha ili kuepuka kipigo hicho kilichokuwa kikitangazwa na wananchi.

Kiongozi wa wabunge 20 waliotumwa kuwakilisha Bunge, Bw. William Shelukindo, akielezea hali hiyo alisema katika historia hajawahi kuona kitendo kama hicho lakini ilionesha jinsi wananchi hao walivyompenda Mbunge wao.

“Imesikitisha kweli imenifanya kutosoma salamu za Spika wa Bunge hata kutoa ubani wa Bunge tumekimbia kuepuka kufa pale...sasa vitu hivi vitaandaliwa utaratibu wake, lakini nawaomba wananchi watulie wamzike mbunge wao,” alisema Bw. Shelukindo.

Kwa upande wake, Waziri aliyewakilisha Serikali Bw. Steven Wassira, alisema kitendo hicho kimewasikitisha, lakini alisema hakuna njia ya kupata ukweli wa kifo cha Mbunge huyo hivyo ni vema familia kama ilivyoamua, kufanya uchunguzi huo upya katika kujiridhisha.

Bw. Wassira aliwataka wananchi wa jamii ya Tarime kuamini kuwa Bw. Wangwe amekufa na hakuna siasa kwenye jambo hilo.

"Sisi hatukuja hapa kufanya siasa , Rais (Jakaya Kikwete) alipoenda kutoa heshima hakuwa anafanya siasa, tumekuja kushirikiana na familia kufanikisha mazishi," alisisitiza Bw. Bw. Wassira na kuongeza;

"Sisi hatuna mgogoro, kama serikali tunakubaliana nao (wanafamilia) na tunaafiki uamuzi huo kwa heshima ya marehemu na familia." Bw. Wassira alisema tukio hilo ni kubwa na ni la majonzi na yanakuwa makubwa zaidi kutokana na kifo chake kuwa cha ghafla.

Alisema kabla ya kifo chake alizungumza na Bw. Wangwe Bungeni jioni akiwa mzima lakini walivyopata taarifa za kifo chake ilishangaza sana. Alisema baada ya kupata taarifa za kifo chake alikuwa wa kwanza kumjulisha kaka yake Profesa Wangwe.

Aliwataka wananchi wa Tarime kuwa wavumilivu kwani tukio hilo sio la kwanza kuwatokea na kutolea mfano kifo cha Baba wa Taifa, Marehemu Julius Nyerere.


Awali, baada ya Profesa Wangwe kutoa kauli hiyo, Bw. Kabwe alisema watahakikisha uchunguzi unafanyika na kutangaza hadharani matokeo yake na kusema tayari Polisi wamemkamata mmoja wa abiria waliokuwa wakisafiri na Mbunge huyo siku ya ajali.

"Kama kila kitu kitakwenda sawa tunatarajia kesho (leo) uchunguzi utakuwa umekamilika," alisisitiza. Alipoulizwa kama vurugu zilizojitokeza jana hazitaweza kujirudia leo Profesa Wangwe alijibu: "Mimi na wewe hatukujua kama haya (vurugu) yatatokea siwezi kusema kesho itakuwaje."

Shughuli za ujenzi wa kaburi hadi hatua hiyo inafikiwa, zilikuwa zimekamilika.

(source:majira, Imetolewa mara ya mwisho: 01.08.2008 0112 EAT.
George John, Tarime na Reuben Kagaruki, Dar)

..........................................................................

No comments: