Monday, 21 April 2008

Yanga Bingwa TZ (Bara) 2008/09

(SOURCE: Nipashe, 21 Apr 2008. By Somoe Ng'itu)

Pamoja na kubanwa na kujikuta ikifungana 2-2 na Prisons ya Mbeya, Yanga jana ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa soka wa Tanzania Bara katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam.

Kwa matokeo hayo iliweza kufikisha pointi 48, ambazo haziweza kufikiwa na timu nyingine yeyote katika ligi hiyo.

Yanga sasa imekata tiketi ya kushiriki mwakani katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Pia timu hiyo inatazamiwa kupata kitita cha Sh. milioni 30 kutoka wadhamini wa ligi hiyo, ambayo ni kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom na kiasi cha Dola 12,000 (sh. milioni 14) kutoka kampuni ya televisheni ya GTV.

Hata hivyo, ubingwa huo unaweza kuingia utata ikiwa Kamati ya Usuluhishi ya Shirikisho la soka la Kimataifa (CAS) itasikiliza na kukubali rufaa iliyokatwa na Simba kudai pointi zake tatu ilizopokonywa katika mchezo wake na Coastal Union.

Simba yenye pointi 40 ikiwa itashinda mechi zake mbili zilizosalia itakuwa na pointi 46 na ikibahatika ikapewa na zile za CAS basi itakifikisha pointi 49.

Yanga imeacha kizaizai cha vita ya kuwania nafasi ya pili kati ya wapinzani wao wa jadi, Simba na Prisons.

Prisons baada ya sare ya jana, imeweza kufikisha pointi 42 na imebakiwa mchezo mmoja wakati Simba ina pointi 40 wakati imebakiza mechi mbili mojawapo ikiwa dhidi ya watani wa jadi, Yanga.

Yanga ilianza kwa kishindo mchezo huo uliofanyika katika hali ya mvua na huku uwanja ukiwa umejaa maji na kuweza kujipatia bao la kuongoza lililofungwa katika dakika ya nane na Maurice Sunguti baada ya kupokea pasi ya Prisons, ambapo mabeki wa Prisons walijichanganya kuokoa mpira huo.

Prisons walicharuka na kufanikiwa kusawazisha bao hilo katika dakika ya 32 kwa bao lililozamishwa kwa kichwa na Godfrey Bonny baada ya kuunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na Stephen Mwasika.

Yanga ilianza kwa nguvu kipindi cha pili lakini ikapata bao la kutatanisha baada ya Jerry Tegete kuujaza mpira wavuni lakini baada ya kuunawa lakini kinyume na matarajio ya wengi mwamuzi Aranusi Luena akakubali bao hilo.

Prisons, hata hivyo, ilicharuka na kurudisha bao hilo katika dakika ya 77 kupitia kwa Godfrey aliyeunganisha krosi ya Mwasika.

Akizungumza baada ya mchezo huo Kocha wa Yanga, Dusan Kondic alisifia kiwango cha timu ila akaonya msimu ujao anautaka uongozi wa Yanga kuongeza makipa.

Naye Kocha wa Prisons, Juma Mwamusi alidai kiwango cha uamuzi nchini iko chini na kuonya ni vizuri waamuzi wakapandisha kiwango chao ili kuweza kupata mabingwa wa kweli.

Alimponda mwamuzi wa mchezo wa jana, Luena kwa kuonyesha wazi kuibeba Yanga kwa kukubali bao la utatanishi la Yanga na kukataa lile la Oswald Morris kwa madai alikuwa ameotea katika dakika ya 71.
Timu zilikuwa:

Yanga: Bernjamin Hakule, Fred Mbuna, Abuu Ntiro, Nadir Haroub, Wisdomu Ndlovu, Hamisi Yussuf,
Mrisho Ngassa, Maurice Sunguti, Ben Mwalala na Athumani Iddi.

Prisons: Xavery Mapunda, Lusanjo Mwakifamba, Stephano Mwasika, Aloyce Adam, Mbega Daffa, Msafiri Hassan, Misanga Migayi, Geofrey Bonny, Oswald Morris, Shabaan Mtupa na Yona Ndabila.

No comments: