Monday, 21 April 2008

Ukiwaona Ditopile Mzuzuri afariki dunia!

Dito aaga dunia (SOURCE: Nipashe, 21 Apr 2008. By Idda Mushi, PST, Morogoro)
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ukiwaona Ditopile Mzuzuri (65), amefariki dunia.
Ditopile alifariki dunia ghafla jana asubuhi akiwa amejipumzisha akiangalia televisheni kwenye hoteli ya Hilux, mkoani Morogoro. Imeelezwa kuwa, Ditopile alikuwa amepanga chumba namba 106 katika hoteli hiyo akiwa na mke wake, Bi. Tabia.
Taarifa kutoka hotelini hapo zilieleza kuwa, aliaga dunia muda mfupi baada ya kuswali Swala ya Alfajiri.

Kabla ya kifo chake hicho, Ditopile alikuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji ya kumpiga risasi dereva wa daladala, Hussein Mbonde Novemba, 2006 jijini Dar es Salaam. Wakati wa tukio hilo, Ditopile alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambapo kutokana na kesi hiyo, aliwekwa rumande kwa miezi kadhaa kwa ajili ya upelelezi. Mapema mwaka jana, kesi yake ilibadilishwa kutoka ya mauaji na kuwa ya kuua bila kukusudia na kuachiwa kwa dhamana. Mwishoni mwa mwaka jana, Ditopile aliripotiwa kujihusisha na ujasiriamali kwa kununua asali mkoani Tabora na kuuza Dar es Salaam.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Meshack Massi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Bw. Thobias Andengenye na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Said Kalembo, walithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa alifariki dunia jana saa 3:00 asubuhi.

Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Massi alisema alipokea taarifa ya kuzidiwa kwa Ditopile asubuhi na kuagiza gari la wagonjwa kumfuata ambapo baada ya kuwasili alipelekwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na alipopimwa ilibainika kuwa alikwishakata roho.

``Aliletwa akiwa hana dalili za uhai, hadi sasa hatujafahamu kilichosababisha kifo chake, lakini tunaendelea na uchunguzi ili kubaini,`` alisema Dk. Massi mara baada ya mwili wake kutolewa katika chumba cha uangalizi maalum wa wagonjwa (ICU), daraja la kwanza ili kupelekwa chumba cha kuhifadhi maiti.

Mganga Mkuu alisema wafanyakazi wa hoteli ya Hilux walipiga simu hospitalini hapo kuomba msaada wa gari la kubeba wagonjwa ili kumsaidia mteja wao huyo ambaye wakati huo alikuwa mgonjwa.

Naye Kamanda wa Polisi, Bw. Andengenye alisema baada ya kupokea taarifa ya kuwasili kwa mwili wa Ditopile hospitali ya Mkoa, waliongea na mdogo wa marehemu, Bw. Selemani Mzuzuri aliyekuwa amefuatana naye aliyesema hadi juzi saa 4 :00 usiku, walipoachana kaka yake alikuwa mzima.

Kwa mujibu wa Bw. Andengenye, marehemu, mkewe na mdogo wake, walifika Morogoro Ijumaa iliyopita na baada ya shughuli zao walipanga kurejea Dar es Salaam juzi wakitokea shambani Mgongola wilayani Mvomero.

Hata hivyo, kutokana na ubovu wa barabara walichelewa na kuwalazimu kulala Morogoro.

``Baada ya kurejea walitembelea jamaa na marafiki hadi saa 4:00 usiku walipolala na asubuhi waliamka kwa swala.`` alisema Kamanda Andengenye.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Kalembo aliyekuwa hospitalini hapo na viongozi wengine mbalimbali wa serikali alieleza kusikitishwa kwake na kifo cha ghafla cha Bw. Ditopile ambapo alisema wamekipokea kwa mshtuko mkubwa.

``Dito ni mdogo wangu, ndugu yangu ni zaidi ya kumfahamu akiwa Mkuu wa Mkoa...madaktari wanadhani alikuwa na ugonjwa wa moyo, kwani juzi na jana alifanya shughuli zake kama kawaida hakuwa na tatizo hadi asubuhi wakati akiangalia televisheni,`` alisema.

Alisema kifo hicho kimemshtua kwa vile hivi karibuni aliwasiliana na Bw. Ditopile kwa simu ya mkononi akimweleza kuwa, anakwenda mkoani humo kibiashara na alitaka wakutane.

Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Bi. Mary Chatana, aliyefika hospitalini hapo, alieleza kusikitishwa na kifo hicho cha ghafla.

Mdogo wa marehemu, Bw. Mzuzuri alishindwa kuongea na waandishi wa habari.

Ditopile amefariki dunia huku akiacha kesi iliyokuwa ikisikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Baada ya kusomewa maelezo hayo kesi hiyo, ilihamishiwa Mahakama Kuu lakini hadi kifo chake, ilikuwa haijapangiwa tarehe.

Wakati huo huo, Lucy Lyatuu anaripoti kuwa, mwili wa Ditopile unatarajia kuzikwa kesho katika shamba lake lililoko Kinyerezi, jijini Dar es Salaam. Mwili wake ulitarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam jana kwa gari la wagonjwa la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambapo pia umehifadhiwa katika hospitali Kuu ya JWTZ Lugalo.

Mdogo wa marehemu, Bw. Abdallah Mwinshehe, aliyasema hayo jana nyumbani kwa marehemu Upanga Mtaa wa Mfaume. Alisema wakati wa uhai wake, Ditopile alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu na kisukari tangu mwaka 1995 na magonjwa hayo yalichachamaa zaidi wakati wa kesi yake.

Wakati wa uhai wake, Ditopile aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika chama na serikali. Baadhi ya nyadhifa alizowahi kushika ni Katibu Mkuu wa CCM Wilaya ya Sengerema, Mwanza, Tabora na baadaye kuteuliwa kuwa mbunge wa Ilala.

Pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kigoma, Lindi, Pwani na Tabora.

Alisema marehemu ameacha wajane wawili na watoto watatu.
Baadhi ya viongozi waliofika nyumbani kwa marehemu jana ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Abbas Kandoro na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Jaka Mwambi, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Bw. John Guninita.

Akimzungumzia marehemu Ditopile Bw. Kandoro alisema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na kwamba alikuwa mcheshi aliyekuwa akiongea kwa mizaha kufikisha ujumbe wake.

No comments: