Friday, 25 April 2008

U/Taifa ni wa nini?

Mbona Uwanja wa Taifa unabaniwa-baniwa sana! Kwani ni wa maonyesho tu au umejengwa kwa ajili ya kutumika ktk michezo na kama kitega uchumi!! Watu wa serikalini wananishangaza sana!!!
........................

Stars ruksa kutumia Uwanja Mpya - Mkuchika
(SOURCE: Nipashe, 25 Apr 2008. By Mwandishi Wetu)
Serikali imeruhusu timu ya soka ya taifa, Taifa Stars kutumia Uwanja Mpya wa Taifa kwa ajili ya mechi zake za michuano ya awali ya Kombe la Dunia zinazoanza mwezi ujao.

Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Kapteni George Mkuchika, alisema serikali imechukua uamuzi huo baada ya kuzingatia ndio pekee uliokaguliwa na Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA).

Mkuchika alieleza kuwa serikali imetoa ruhusa kwa mechi za Stars tu kuchezewa kwenye uwanja huo.

``Serikali baada ya kushauriana na wataalamu wa michezo wa hapa nchini pamoja na wajenzi wa uwanja huu mpya, imeridhia kuanzia hivi sasa, mechi zote za kimataifa zinazohusu Taifa Stars tu, zitachezwa katika uwanja wetu mpya,``

Mechi ya kwanza, ambayo Stars itatumia uwanja kwa ajili ya mechi hizo itakuwa ile dhidi ya Mauritius, itakayochezwa Mei 31, 2008.

Stars haitaweza kucheza usiku kutokana na matatizo ya umeme na wahusika wamepeleka maombi Shirikisho la Kimataifa la soka (FIFA) ili kuomba mechi za Stars zichezwe kuanzia saa 10 jioni.

Alisema ili kulinda uhai wa majani katika uwanja na kudumisha uzuri wake, wataalamu wamependekeza kwamba mechi mbili tu kwa wiki zinaweza kuchezwa kwenye uwanja huo.

Serikali ilikuwa imezuia matumizi ya uwanja huo kutokana na kuwepo kazi ndogo ndogo za kukamilisha katika uwanja huo. Alitoa mfano wa kazi ya kuweka ving'amuzi katika njia za kuingilia, umeme na pia kutokuwepo kwa uongozi wa kuendesha uwanja huo kibiashara.

Uwanja Mpya ulioanza kujengwa Januari 2005, ulitumika mwaka jana kwa mechi mbili za Stars, moja ya kirafiki dhidi ya Uganda na nyingine ya Kombe la Mataifa ya Afrika ilipokabiliana na Msumbiji.

Mechi hizo zilichezwa katika uwanja huo wenye thamani ya Sh. bilioni 56.4 kutokana na mechi ya Stars na Msumbiji kutakiwa kuchezwa usiku na hakukuwa na uwanja mwingine wenye taa.

No comments: