Thursday, 24 April 2008

Hakuna tena kurudia 'form II'

(kutoka: majira, 24.04.2008 0146 EAT. Na Joseph Lugendo, Dodoma)

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe amesema wanafunzi watakaopata alama za chini katika mtihani wa kidato cha pili, wataruhusiwa kuendelea kidato cha tatu chini ya uangalizi maalumu wa waalimu.

Alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Kongwa, Bw. Job Ndugai (CCM), aliyesema kuwa mtihani huo umekuwa kero kwa wanafunzi na wazazi kwa kuwa wanafunzi wanaofeli hutakiwa kurudia mwaka.

Bw. Ndugai ambaye aliipongeza Serikali kwa kuondoa adhabu ya kurudia kwa watahiniwa wa mtihani wa darasa la nne, alisema mfumo wa ufundishaji kwa lugha ya Kiswahili katika elimu ya msingi unasababisha wanafunzi wengi kufeli mtihani wa kidato cha pili kwa kushindwa kumudu lugha ya Kiingereza.

Prof. Maghembe, alisema mtihani huo unashabihiana na wa darasa la nne kwakuwa unawaandaa wanafunzi kukabili mtihani wa kidato cha nne bila woga, pia unasaidia kupima mafanikio na maendeleo ya mwanafunzi ili kubaini iwapo malengo yaliyokusudiwa katika ufundishaji yamefikiwa.

Umuhimu mwingine wa mtihani huo ni pamoja na kusaidia katika tathimini itakayowawezesha wataalamu wa elimu kubaini matatizo mbalimbali katika ufundishaji na kujifunza ili kuweza kuboresha mitaala na kurekebisha mapema kasoro zinazojitokeza.

Alisisitiza kwamba upimaji wa wanafunzi katika kila somo ni muhimu kwasababu unawapa wanafunzi ari ya kuongeza bidii katika masomo yote na kuongeza kuwa mitihani hiyo itaendelea kuwepo kama kawaida ila itakuwa na lengo la kutathimini ufundishaji na kujifunza kwa wanafunzi na siyo kumfanya arudie darasa anaposhindwa kufikia alama.

Alibainisha kwamba wanafunzi ambao watashindwa kufikia alama zinazotakiwa, watapewa msaada katika maeneo yanayowapa shida kadri watakavyokuwa wakiendelea na elimu ya sekondari.

No comments: