Thursday, 3 April 2008

'Maji salama kwa wote'

Wanamuziki wa OTTU Jazz waliwahi kuimba wimbo 'Maji ni Uhai'. Huu wimbo ni moja kati ya nyimbo kadhaa zenye maudhui mazuri ktk jamii.

Nakumbuka, katika miaka ya 1980 mwanzoni mwanzoni, niliwahi kusoma malengo fulani ya serikali yetu kuhusu usambazaji maji kwa wananchi.

Hayo malengo yalieleza wazi kuwa 'ifikapo mwaka 1992 wananchi wote wataweza kupata maji safi na salama ndani ya umbali wa mita 400 kutoka katika makazi yao'.

Mwaka 1992 ulifika na kupita!

Ni jambo la kushangaza kuwa hadi hii leo mwaka 2008, miaka 16 baada ya 1992, bado wananchi hawana huduma ya maji safi na salama. Leo hii tungekuwa tunaongelea kila kaya kupata maji safi na salama. Lakini hali imebaki kuwa nadharia tu katika makaratasi. Sio vijijini wala mijini, wananchi wanalia na uhaba wa maji. Wengi wao wanatumia muda mwingi kuhangaika na kutafuta maji. Pale yanapopatikana huwa sio salama na yanauzwa kwa bei za juu.

Muda ambao mwananchi angeutumia ktk uzalishaji kiuchumi, unapotea katika kutafuta ndoo ya maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kifamilia.

Serikali imeunda wizara mpya ya 'Maji na Umwagiliaji'. Ni wazo jema lakini ni la kinadharia zaidi. Hivi inawezekana kweli maji ya yatafutwe na kuelekezwa mashambani kwa ajili ya kumwagilia, wakati wananchi hawana maji ya kunywa au ya kupikia chakula?

Ninapenda kuishauri serikali kuwa iweke kipaumbele cha pekee katika;
- kutafuta vyanzo vya maji na kuyasambaza kwa wananchi.
- kuwekeza zaidi katika miundombinu ya maji ili kuhakikisha wananchi wanaipata huduma ya maji katika majira/misimu yote kwa mwaka.

Kwa kufanya hivyo ninaamini kila kaya inaweza kupata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika na kwa umbali mfupi zaidi!

Huduma ya maji ni haki ya kila mtanzania, kwa hiyo serikali iwajibike kwa hilo!

No comments: