Saturday, 19 April 2008

CD akerwa na ufisadi

Ufisadi wamkera Msuya (SOURCE: Nipashe, 19 Apr 2008. By Simon Mhina)

Waziri Mkuu wa awamu ya (kwanza na ya) pili, Bw. Cleopa Msuya, amesema kushamiri ufisadi na uporaji nchini ni matokeo ya ulegevu mkubwa wa udhibiti mali za umma uliokithiri katika awamu ya tatu.

Kiongozi huyo alisema wizi uliotokea kupitia akaunti ya madeni ya nje ya Benki Kuu (EPA), ni mfano halisi juu ya ulegevu huo. Alisema fedha za EPA hazikuchotwa siku moja bali kwa nyakati tofauti na watu wengi hivyo ni ajabu kuona serikali haikugundua.

Alisema inasikitisha kuona kwamba EPA imezalisha mabilionea ambao hawakulipa kodi na ndiyo wanaochangia Shilingi kushuka thamani na kuongeza umaskini.

Bw. Msuya alisema ulegevu huo haukuwa wa bahati mbaya bali ulipangwa, ulifahamika na uwepo kwa makusudi.

``Mambo haya yameanza muda mfupi baada ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere kufariki, huko nyuma walitaka kuyafanya haya, lakini walikuwa wakimhofu Mwalimu,`` alisema.

Alisikitika kuwa wakati Watanzania wanaogolea kwenye ufukara EPA imezalisha mabilionea wanaoagiza magari ya kifahari kutoka nje na kuyasafirisha kwa ndege kama keki hadi nchini ili yasipigwe na joto wala mvuke wa baharini.

``Hivi kweli mtu unanunua magari na kuyasafirisha kwa ndege kwa sababu zipi hasa?
Alihoji na kuongeza mambo hayo ni uthibitisho kwamba wanaofanya hivyo hawana uchungu na pesa wanazotumia kwa vile hawajazitokea jasho.``

Alipoulizwa iwapo awamu ya kwanza na ile ya pili aliyoongoza kwa nyadhifa za Uwaziri na Uwaziri Mkuu, mafisadi hawakuwepo au serikali ilikuwa inaficha taarifa zao?

Bw. Msuya alisema enzi hizo palikuwa hakuna kiongozi aliyekuwa anathubutu kufanya ufisadi kutokana na miiko na taratibu zilizokuwepo.

Alisema kama kuna watu walitumia madaraka yao kuiba walikuwa wachache.

No comments: