Ni vizuri serikali itimize makubaliano yake ktk mikataba inayojiwekea na watoa huduma wa ndani ya nchi. Serikali isiwe msitari wa mbele kulipa madeni ya nje tu wakati wananchi wanaumia kutolipwa madai yao halali!
-mosonga
..................................
Wazabuni waanza mgomo
(* SOURCE: Nipashe, 17 Apr 2008. By Idda Mushi, PST Morogoro)
Wazabuni wanaotoa vyakula katika shule za sekondari za mabweni zinazomilikiwa na serikali na vyuo vya ualimu mkoani Morogoro wanaanza mgomo wao leo wa kutoa huduma hiyo.
Wamesema wamelazimika kuchukua hatua hiyo kwa kuwa sasa wamefilisika na serikali imeshindwa kuwalipa malimbikizo ya madeni yao ya muda mrefu.
Walimweleza msimamo huo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa, wanapaswa kuwa wavumilivu na kuendelea kutoa huduma zao kwani serikali inashughulikia madai yao.
Walipinga kipengele katika taarifa iliyotolewa na Profesa Maghembe cha kuwataka kusubiri hadi baada ya wiki tatu ndipo walipwe madai yao.
Walisema wakati Waziri akisema hayo, waraka mwingine umewataka kupeleka madeni yao mjini Dodoma na kwamba serikali inaendelea na uhakiki wa madeni hayo.
``Tunaambiwa tubebe madeni yetu kupeleka Dodoma, halafu huko tukifika tutagharimiwa na nani na hali zetu zimekuwa mbaya, tutaishije na tutatumia usafiri gani kufika huko?
Kama Waziri ana wasiwasi, aunde tume ije kutukagua, hatuna wasiwasi, tumefilisika kabisa na hatukopesheki,`` alisema mmoja wa wazabuni hao, Bw. Juma Ng'ondavi.
Wazabuni hao wa mkoani Morogoro, walisema lengo lao sio kugoma bali wameishiwa fedha za kuendelea kutoa huduma na huku wakitakiwa kulipa madeni waliyokopa benki.
``Kama huyu mmoja wa wazabuni mwenzetu, anadaiwa Sh. milioni 121 na benki ya CRDB. Aliandikiwa barua ya kuhimizwa kulipa tangu mwishoni mwa mwaka jana, lakini hadi sasa hajalipa na anatishiwa mali zake kupigwa mnada, tutafika kweli kwa hili?``
Alihoji mmoja wa wazabuni hao, Bw. Paschal Kihanga, kwa niaba ya wenzake huku wakionyesha barua ya mwenzao aliyoandikiwa na benki.
Wazabuni hao, walisema wanashangazwa na malimbikizo ya madeni yao ya tangu mwaka 2005 hadi sasa, huku bajeti za wizara zikiwa zinapitishwa mwaka hadi mwaka na kuhoji iwapo kama waliwahi kusikia shule hizo wanazopeleka huduma zikifungwa kwa kukosa chakula.
Walibainisha kuwa, wanaamini kauli inayotolewa na serikali kwa sasa ni ya kisiasa zaidi kwani hata Aprili, mwaka jana, walipolalamikia madai yao, Wizara ilituma wakaguzi kuhakiki madeni na baada ya zoezi hilo, walilokuwa wakidai Sh. milioni 100 walijikuta wakipelekewa milioni tano tu na kwamba hadi leo hakuna utekelezaji wa kuridhisha wa ulipwaji wa madeni yao.
``Wenzetu wazabuni wa maeneo mengine hawana matatizo, sisi tulio chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ndio tatizo... Inashangaza sana kwani wizara hii imejaa wasomi ambao tuna imani wanapanga vyema mambo yao,`` alisema.
Wazabuni wengine, Karama Abdalah, Juma Tembo na Mahendeka Sebastian kwa niaba ya wenzao walisema tatizo hilo la madeni sio kwa mkoa wa Morogoro pekee bali pia kwa mikoa mingine nchini hivyo kitendo cha kuwataka waende Dodoma ni kusababisha usumbufu na gharama zisizo za lazima.
Alisisitiza kwamba uamuzi wao wa kutoendelea kutoa huduma haulengi kugoma bali ni kufikia mwisho wa uwezo wao kifedha kutokana na kufilisika.
Mkoa wa Morogoro pekee, kwa mujibu wa wazabuni hao, unadai serikalini zaidi ya shilingi bilioni 1.5 .
Thursday, 17 April 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment