(SOURCE: Alasiri, 22 Apr 2008. By JACQUELINE MOSHA , JIJINI 'Dar')
Baada ya kukithiri kwa baadhi ya wadada wanaotinga na viguo vifupi vinavyoweza kuwakwaza wengine, Kanisa la Watakatifu Mashahidi wa Uganda lililopo Magomeni Jijini limewapiga `stop` waumini wa aina hiyo kuhudhuria ibada zake hadi watakapovaa kistaarabu.
Wito huo na tahadhari vimetolewa na Paroko msaidizi wa Kanisa hilo, Padri Venance Tegete wakati wa ibada ya Jumapili kanisani hapo.
Padri Tegete akasema kuwa, ni aibu kwa baadhi ya waumini wanaovaa mavazi hayo yanayoonyesha jiografia ya maumbile yao na kisha kujaribu kuhudhuria ibada kanisani.
Mbaya zaidi, wanaofanya hivyo wanajua wazi kwamba kila vazi lina mahala pake na kwamba kanisani ambako mwanadamu hujinyenyekeza mbele ya Mungu, kamwe si mahala pa kuvaa viguo vya ajabu kiasi cha kuwakwaza wengine.
``Jamani kuna wengine hawana uvumilivu, wengine uimara wao katika kuvumilia ni mdogo, sasa kwanini mnataka kuwaharibia ibada zao kwa kuvaa nguo zinazoonyesha Jiografia ya maumbo yenu? Si vizuri, naomba muwe makini katika uvaaji wenu kabla ya kuhudhuria ibada. Yawezekana, baadhi ya watu wakajikuta wakiacha kusali na kuwakodolea macho wale wanaovaa viguo vya ajabu... mnawakwaza. Na si busara kuwatia majaribuni wenzenu... mjikague vyema kabla ya kuingia kanisani ili ibada zifanyike vizuri,`` akasisitiza Padri Tegete.
Akasema mavazi ya ufukweni yavaliwe ufukweni, ya muziki yavaliwe kunako kumbi za muziki na yale ya staha ndiyo yanayostahili zaidi kanisani, ambako viguo vifupi na vya kubana havina nafasi.
Katika hatua nyingine, kanisa hilo limeanzisha utaratibu wa kuwapa khanga wale wote wanaoonekana wakiwa na mavazi yasiyostahili ili kuwafanya wasiwakwaze wenzao wakati wa ibada.
Tuesday, 22 April 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment