Thursday, 17 April 2008

Kashfa zaidi?

(source: www.raiamwema.co.tz)
Nchi sasa inayumba
Mwandishi Wetu Aprili 16, 2008
Watu mbalimbali waliozungumza na Raia Mwema wiki hii wanalitaja suala la kuzuiwa kwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kujitetea kuwa dalili za jinsi hali ilivyo mbaya ndani ya CCM, hali ambayo inaigusa pia Serikali.

Watu hao wanataja tukio la Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ambaye ana fedha nyingi za kigeni nje ya nchi kuwa ufa mwingine ndani ya CCM na Serikali ambako Chenge anaheshimiwa sana.

Yanatajwa pia matukio ya wizi ndani ya Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), mikataba mibaya ya uchimbaji madini na kushindwa kwa Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua thabiti juu ya watuhumiwa, wengine watu wa karibu naye, kuwa ambayo yanatia doa katika mchakato wa nchi kujiletea maendeleo.

Vyanzo vya habari vinasema sababu ya kukua kwa mtikisiko huo ni jinsi Kikwete “alivyoliachia gurudumu” la mapambano dhidi ya ufisadi, huku likiwakumba watu waliokaribu naye na hata wasaidizi wake ndani na nje ya serikali.

Matuko ya hivi karibuni yaliyotokea bungeni mjini Dodoma na katika vikao vya CCM kijijini Butiama, yamechochea moto wa mtikisiko huo ndani ya CCM na serikali yake.

Moto huo unaelezwa kuwashwa/kuchochewa zaidi na wahusika/watu walio karibu na waathirika wa ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu mradi tata wa umeme wa dharura uliokabidhiwa kampuni ya Richmond ya Marekani, wale wanaoguswa na uchunguzi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na maeneo mengine yanayonuka rushwa.

Tayari Kikwete anaelezwa kupokea maelezo, ushauri hata lawama baada ya kuibuka kwa tuhuma na uchunguzi wa masuala yote yanayohusishwa na ufisadi ambayo yakaitikisa Serikali yake.

Mjini Dodoma wiki hii hali haikuwa shwari kutokana na mkanganyiko wa maelezo aliyotaka kuwasilisha Rostam Aziz, akielezwa kujiandaa kikamilifu “kupasua bomu”.

Kwa kutumia Kanuni za Bunge, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ameyazuia maelezo ya Rostam katika kulinda maslahi na hadhi ya Bunge, na pia “kulinda mshikamano ndani ya Bunge na ndani ya CCM”.

Uamuzi wa kumzuia Rostam kuwasilisha maelezo yake ulifikiwa baada ya vikao vya wabunge wa CCM wakiongozwa na Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa chama na kamati ya wabunge wote wa CCM. Rostam ni mjumbe wa vikao vyote kutokana na wadhifa wake wa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.

Rostam mwenyewe amenukuliwa katika vyombo vya habari akisema kwamba alikuwa na maelezo yenye nguvu ambayo yangebainisha kuwa yeye ni mtu safi ambaye hakuhusika na mkataba wa Richmond pamoja na kuwa na uhusiano wa kibiashara na kampuni iliyorithi mkataba huo ya Dowans.

Unyeti wa maelezo ya Rostam unaelezwa pia kuhofiwa kuwachafua ama kuwaingiza hata viongozi wa juu wa CCM wa sasa na wa zamani ambao hawakuguswa kabisa katika ripoti ya Mwakyembe, jambo ambalo lingezidisha hasira na chuki miongoni mwa wana CCM.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wanasema pamoja na nia nzuri ya Kikwete, uamuzi wa kuanika hadharani uozo wa BoT na hata kuruhusu Waziri Mkuu wake kujiuzulu, ni mambo yatakayoisumbua sana serikali na CCM kwa muda mrefu.

Kuchunguzwa kwa kuhusika na rushwa ya ununuzi wa rada ya Sh bilioni 70, na hatimaye kupekuliwa kwa Waziri Chenge ni tatizo jingine kwa Rais Kikwete.

Chenge amekutwa na kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti zake za nje na akaunti moja pekee katika benki moja ya kisiwa cha Jersey nchini Uingereza imekutwa na fedha zinazofikia Sh bilioni moja za Tanzania.

Ugumu mwingine unaomuweka pabaya Kikwete ni kauli yake ya kwamba Mkapa kama walivyo wastaafu wengine anastahili “kuachwa apumzike kwa amani”, kutokana na tuhuma kadhaa kumgusa Rais huyo aliyeingia madarakani mwaka 1995.

Uchunguzi unaondelea dhidi ya Chenge kuhusiana na kesi ya rada na baadhi ya tuhuma nyingine na habari za kuchunguzwa kwa mawaziri wengine wawili wa zamani, bila shaka kutamgusa moja kwa moja Mkapa na hivyo kumpa Kikwete mtihani mwingine mgumu wa kuamua kuachia sheria kuchukua mkondo wake dhidi ya mtu ambaye hakupenda ashughulikiwe kupitia mikono yake.

Baadhi ya wana CCM wamesema Kikwete hapaswi kutishika kwa kuwa mambo mengi anayoyafanya anaungwa mkono na wananchi walio wengi pamoja na wanasiasa ambao wamekuwa wakiweka pembeni maslahi binafsi na hivyo kumshauri kutorudi nyuma katika mapambano dhidi ya ufisadi na maovu mengine katika jamii.

No comments: