Bei ya vyakula sasa yatisha
(* SOURCE: Nipashe, 14 Apr 2008. By Lucy Lyatuu)
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe jana jijini Dar es Salaam kwenye baadhi ya masoko, ulibaini kuwa bidhaa nyingi zimepanda na kusababisha wananchi wenye kipato cha chini kuwa katika hali ngumu.
Katika soko la Kisutu, Kariakoo, Mwananyamala na Tandale, bei ya:
-mchele imepanda kutoka wastani wa Sh. 1,000 kwa kilo hadi kufikia Sh. 1,500
-maharage (soya) kwa kilo yaliuzwa Sh. 1,700 badala ya Sh. 900.
-karanga kwa kilo ziliuzwa Sh. 1,500 badala ya 1,000,
-choroko Sh. 1,500 badala ya Sh. 1,200,
-unga wa sembe Sh. 800 badala ya Sh. 550 kwa kilo,
-viazi viliuzwa Sh. 800 badala ya 500 na
-vitunguu Sh. 800 badala ya 500 (kwa kilo)
-gunia la viazi kwa sasa linauzwa Sh. 27,000 badala ya Sh. 22,000,
-nyanya boksi moja Sh. 35,000 badala ya Sh. 20,000
-vitunguu nusu gunia vinauzwa Sh. 60,000 tofauti na Sh. 45,000.
Akizungumza kutoka soko la Kariakoo jijini, Bw. Joseph Moses, alisema ni kweli mazao ya chakula yamepanda na sio mara ya kwanza kwani katika msimu wa mvua barabara nyingi zinakuwa hazipitiki na mafuta kutumika kwa wingi.
``Miundombinu ya barabara iliyopo ni mibovu huko vijijini kunakotoka chakula, ndio sababu kuu ya kupanda kwa bei ya mazao kutoka kwa wakulima mashambani kwani ufikishaji wake sokoni unakuwa mgumu,`` alisema.
Aliongeza kuwa chanzo kikuu cha kumfikishia mlaji wa mwisho bidhaa kinatokana na usafiri na hivyo kupanda kwa bei ya mafuta, petroli na dizeli, nako kumechangia ongezeko la bei ya bidhaa sokoni.
Bw. John Anthony, Mfanyabiashara wa Tandale alisema ni kweli bidhaa nyingi sokoni zimepanda kutokana na mpaka wa Tanzania na Kenya kufunguliwa.
``Wakati Kenya wakiwa kwenye mgogoro wafanyabiashara walielekeza nguvu nyingi kuleta bidhaa zao jijini Dar es Salaam, lakini baada ya kumalizika kwa ugomvi sasa wanaingia kwa wingi nchini humo hali inayofanya bidhaa kupungua Dar na kukosekana ushindani, hali ambayo inapandisha bei,`` alisema Bw. John.
Monday, 14 April 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment