Tuesday, 24 June 2008

TZ: Mbunge afafanua 'madudu' ya EPA

Asante Mhe. Slaa kwa kutufafanulia, hata mie nilikuwa sifahamu haya mambo kwa undani!
......................................................
....................................................
Slaa amjibu Mkulo
(SOURCE: Nipashe, 2008-06-24 12:23:01. Na Mwandishi Wetu, Dodoma)
Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, amemjibu Waziri wa Fedha, Bw. Mustapha Mkulo, kuwa amepotosha umma na kwamba kambi ya upinzani imeshtushwa na kauli aliyoitoa kuwa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) si za serikali bali za wafanyabiashara.

Dk. Slaa ambaye ni Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu makadirio ya matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, alisema bungeni jana kuwa kauli hiyo ni ya kupotosha.

Taarifa hiyo ni ya kupotosha. Kambi ya Upinzani imefanya utafiti wa kina na kugundua kuwa fedha hizo kimsingi zinatokana na programu inayoitwa ``Debt Buy Back Program``.

EPA imefanyiwa kazi sana na Timu ya Lazard na baadaye ukaguzi wa PricewaterhouseCoopers (France) tarehe 25 November, 2004,`` alisema.

Aliongeza, hata hivyo, kwamba ukaguzi uliofanywa na Deloitte and Touche 2006 na baadaye kuthibitishwa na Ernst and Young, 2007 ulithibitisha kuwa kampuni 22 zilifanya biashara na makampuni yanayodhaniwa kuwa ni ``hewa``.

Alisema hivyo wafanyibiashara hao, wala ``principles`` wao kutoka nchi za nje hawakuweka fedha zozote BoT kwa lengo kutumiza masharti ya Debt Buy Back Program kama alivyotaka kueleza Waziri wa Fedha.

Alisema kwa msingi huo, fedha zilizoibwa ni za serikali na kwamba kwa taarifa aliyonayo, Ripoti ya Ukaguzi wa EPA katika kifungu cha 3.20, 3.23, na 3.24, kinatamka wazi uwepo wa ``fraudulent supporting documents submitted in to support claims`` (nyaraka za kughushi ili kuhalalisha malipo).

Alisema ufisadi uliotumika ni pamoja na kutumia hati za kughushi katika kutoa fedha kutoka BoT, malipo ya viwango visivyo sahihi au kutumia viwango visivyo sahihi vya kubadilisha fedha (incorrect amounts and incorrect exchange rate).

Alisema ukaguzi ulionyesha kuwa kati ya Sh. bilioni 133, malipo ya zaidi ya sh. bilioni 90.3 yalifanyika kwa kutumia hati za kughushi (invalid and fraudulent supporting documents) na kwamba nyaraka hizo zimeonyeshwa katika kiambatanisho C, zikionyesha pia majina ya makampuni husika.

Dk. Slaa alisema katika kifungu cha 3.25, ukaguzi huo ulishauri kuwa kwa malipo ya zaidi ya Sh. bilioni 42.6, uchunguzi wa kina unahitaji kufanyika.

Alisema taarifa hiyo haikutolewa wazi kwa Bunge wala kwa Watanzania ambao ndio wenye mali hiyo na serikali ni mdhamini kwa niaba yao tu.

``Ufisadi unaotisha zaidi ni ule uliofanyika kupitia Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd iliyosajiliwa nchini, chini ya Sheria ya Makampuni, Sura ya 212, tarehe 29 Septemba, 2005 na kupata hati namba 54040.

Wakurugenzi waliosajiliwa wa Kagoda ni watu wawili wenye anuani za Kipawa Industrial area, Plot no 87 Temeke Dar es Salaam, na P.O. Box 80154 Dar es Salaam, kinyume na utaratibu wa kusajili makampuni kwa wakawala wa serikali, BRELLA, ambao unahitaji wakurugenzi wa makampuni kujisajili kwa kuonyesha anuani ya mahali anapoishi na siyo Sanduku la Posta,`` alisema.

Aliongeza kuwa kwenye fomu za usajili, ambapo John Kyomuhendo amejionyesha kuwa ``Promoter`` hawakuonyesha kama ni wakurugenzi mahali pengine kwenye kampuni nyingine yeyote.

``Cha kushangaza ni kuwa kampuni hiyo ambayo wakurugenzi wake dhahiri wanaonekana wapya kabisa katika uwanja wa biashara, ndani ya wiki nane tu walikuwa wamekwisha kuchotewa zaidi ya Dola za Marekani milioni 30.8, yaani zaidi ya sh. bilioni 40 kwa kinachoelezwa na ukaguzi wa EPA kuwa hati bandia ambazo dalili za wazi ni kuwa hati hizo karibu zote zimesainiwa na watu wasiohusika,`` alisema.

Alisema baadhi ya makampuni yaliyodhaniwa kufanya biashara na Kagoda au hayako kabisa au yamekwisha kubadilisha majina yao (Kif.3.27).

Alisema makampuni hayo yako Marekani, Japan, Ujerumani, Italia, Ufaransa mengine hata anuani zake hazikujulikana kabisa. Alisisitiza kwamba katika hali kama hii, inayoonyesha wazi kuwa kulikuwa na kugushi.

``Waziri Mkulo alipokuwa akijibu alitetea kuwa fedha za EPA si za Serikali. Kinachotisha zaidi, Mhe. Spika, hata Kampuni ya Ukaguzi ya Deloitte kwa barua yao kwa Gavana wa Benki Kuu ya tarehe 6, Septemba 2006 na kwa Wakurugenzi wote wa BoT ya Oktoba 10, 2006 walipomjulisha Gavana, pamoja na wajumbe wote wa Bodi ni pamoja na Katibu Mkuu wa Hazina Bw. Gray Mgonja, kuwa kuna utata kuhusu Kampuni ya Kagoda,`` alisema.

Alifafanua utata huo kwamba japo kampuni hiyo ilisajiliwa Septemba 29, 2005, Septemba 10 2005 ilikuwa tayari na mkataba wa kiasi cha fedha za Japan 956,110.986 na Kampuni ya Nishizawa Ltd na mkataba mwingine wa Dola za Marekani 9,057,463.90 wa Septemba 12, 2005 na Kampuni ya Textima Ltd.

``Mikataba hii yote inatamka kuwa `Kampuni hii imesajiliwa Tanzania kwa mujibu wa Sheria,` jambo ambalo dhahiri ni udanganyifu na ni uvunjifu wa Sheria,`` alisema.

Aliongeza kuwa Kampuni ya Deloitte ilionyesha katika barua walizomwandikia Gavana na wajumbe wa Bodi zikiwa na dosari kadhaa, moja ikiwa mikataba hiyo na maneno na mfumo unaofanana, jambo linaloashiria kuna kughushi, kwani makampuni kwa kawaida yanapenda kuwa na vipengele visivyofanana.

Alisema kwamba kati ya hati zote hizo, hakuna hata moja iliyowekwa kwenye barua halisi (letterhead) za Kampuni zao, na kwamba mikataba yote ilisainiwa ukurasa wa mwisho tu, tofauti na kawaida ya kusaini mikataba.

Alisema makampuni 12 katika sakata hilo yalikuwa na mhuri (seal) unaofanana na ule wa Kampuni ya Kagoda.

``Mambo haya yote yalipaswa kutoa ishara kwa Benki Kuu kuwa mikataba yote imeghushiwa lakini wala siyo Benki Kuu wala Wakurugenzi walioshituka na kuchukua hatua pamoja na barua hiyo ya Deloitte,`` alisema.

``Mheshimiwa Spika, fedha hizi zililipwa kupitia Benki zetu wenyewe, yaani Benki ya Kitanzania ambayo ni CRDB.

Hii ni Benki ambayo ilipaswa kuonyesha uzalendo kwani pamoja na ukweli kuwa benki za kigeni kama vile Kenya Commercial Bank na Barclays Bank walikataa kulipa fedha hizo baada ya kuona kuwa zina harufu ya kifisadi na hata ikafikia mahali wakafunga Account za mteja mmojawapo baada ya kutilia shaka malipo hayo na kuwaandikia BoT pamoja na kuwarudishia hundi zao.``
..............................................................

No comments: