Monday, 23 June 2008

Mbunge wa Tanzania ya leo!

Nilikuwa sielewi kuwa kazi ya mbunge TZ ni kutekeleza ahadi alizotoa ktk kampeni kwa kutumia hela toka mfukoni mwake? Kwa mtaji huu ili mtu awe mbunge anatakiwa kuwanazo!! Nayaunga mkono mawazo ya Rostam (MB) kuwa kuchangia maendeleo jimboni sio lazima uwe mbunge!
.................................

.................................
(Kutoka majira, 23.06.2008 1244 EAT)
VYAMA vya CHADEMA na CCM katika wilaya ya Igunga mkoani hapa, vimesema havitamruhusu Mbunge wa Jimbo la Igunga, Bw. Rostam Aziz, kuacha kugombea ubunge mwaka 2010.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti mjini Igunga juzi, kutokana na kauli ya Bw. Rostam ya kutogombea tena ubunge mwaka 2010, viongozi wa vyama hivyo walisema bado wanahitaji huduma yake.

Walisema Mbunge huyo amewafanyia mengi jimboni na kwamba mwaka 2010 ni mapema kuacha kugombea, kwa kuwa kuna mambo ambayo ameahidi kuyatekeleza, hivyo kuhitaji muda zaidi.

Katibu wa CHADEMA wa Wilaya, Bw. Moka Changarawe, alisema mbunge huyo amewasaidia kwa mambo mengi, yakiwamo ya kuwajengea mabwawa na huduma mbalimbali za maendeleo tena bila kujali itikadi za vyama.

"Mbunge huyu kuna ahadi ameanza kuzitekeleza, hivyo haitakuwa vema aachie ngazi huku akiwa katikati ya kuzikamilisha, sisi tutampa muda mwingine amalizie, lakini si sasa," alisema na kuongeza kuwa hata wanachama wa CHADEMA Igunga wana imani naye.

Naye Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Igunga, Bw. Felix Mkunde, alisema kauli ya Bw. Rostam, waliipokea kwa hisia tofauti na kwamba wataijadili ili wahakikishe anabadili msimamo wake kwa kuwa bado wanamhitaji.

"Hayo ni mawazo yake binafsi, hatuwezi kumlazimisha kubadili msimamo, lakini bila shaka ni mwelewa na ataelewa ni nini tunachokizungumza sisi na kwa nini tunahitaji bado mchango wake jimboni," alisema Bw. Mkunde.

Aliungwa mkono na Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo, Bibi Evelyne Jordan, ambaye alisema Halmashauri ya Wilaya ya CCM kwa kauli moja ilishasema kuwa haitambui wazo hilo la Mbunge Rostam na bado inamhitaji.

Hata hivyo, Bw. Rostam alipoulizwa, alisema ni kweli huo kwa sasa ndio msimamo wake na si lazima awahudumie wananchi wa Igunga akiwa bungeni, kwani anaweza kutoa mchango wake akiwa nje ya Bunge.

"Kama mwana Igunga, nitaendelea kuwatumikia wananchi hata nikiwa nje ya Bunge," alisema.

Kuhusiana na hilo, Bibi Jordan alisema akiwa bungeni na nje ya Bunge ni tofauti, na ndiyo sababu wafanyabiashara na vijana wa wilaya ya Igunga wameshasema hawatakubali kumpoteza na wanamtaka aendelee kuwawakilisha bungeni.

Bw. Rostam aliingia bungeni mwaka 1994 baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa Igunga, marehemu Charles Kabeho na katika uchaguzi wa 1995 na 2000 alipita bila kupingwa.
................................

No comments: