(SOURCE: Nipashe, 2008-06-14 10:11:12)
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo, Sokine (SUA), Dk. Damiani Gabagambi:
``Nilitarajia kwenye bajeti serikali izungumzie suala la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima (mfano magari ya kifahari -mashangingi) lakini sijaona kitu, wasipobana matumizi hakuna kitakachofanyika. Fedha watakusanya na zitaishia kwenye matumizi yasiyoeleweka na ambayo hayamsaidii mtanzania,`` alisema.
Dk. Gabagambi alisema hakuna sababu kwa viongozi wa serikali kununuliwa magari ya kifahari ya aina hiyo. Landrover inaweza kuwa gari mwafaka kwa kiongozi wa nchi inayoendelea kama Tanzania.
Dk. Semboja Haji Khatib, mchumi kitaaluma, aliisifu bajeti hiyo kwamba haina makali sana kwa wananchi.
Hata hivyo, alisema:
1. bajeti hiyo inaandamwa na changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kupanda kwa bei ya mafuta duniani pamoja chakula na mfumuko wa bei.
2. suala la chakula linapaswa kuchukuliwa kama changamoto badala ya tatizo kwa vile Tanzania ikijipanga vyema ina uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha hadi kuuza nje, hususan mchele katika eneo la Afrika Mashariki.
Naye Dk. Damian Gabagambi, alisema:
1. hii ni bajeti ya kibiashara ambayo haionekani kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.
Kiwango cha asilimia 6 kilichopangwa kwa ajili ya kilimo ni kidogo kwani nchi za Afrika ziliwahi kukutana Maputo, nchini Msumbiji, na kukubaliana kwamba bajeti ya kilimo inatakiwa kufika asilimia 10.
2. sio vizuri serikali kuwazuia wakulima wanaopata soko la mazao yao nje.
3. ndege ya kisasa inayotumiwa na rais, aina ya Gulfstream 550, iuzwe kwani gharama zake za uendeshaji ni mzigo kwa uchumi wa Tanzania.
Ndege hiyo iliyonunuliwa kwa Sh. bilioni 40 kutoka kampuni moja nchini Marekani, inatumia mafuta ya mabilioni inaporuka.
``Hakuna sehemu hapa Afrika ambapo unaweza kuifanyia matengenezo ile ndege, hivyo hata matengenezo kidogo lazima iende Marekani, iruke isiruke lazima ikafanyiwe matengenezo,``
Ingawa ndege hiyo muda mwingi haitumiki lakini lazima ifanyiwe matengenezo kila mwisho wa mwezi, hali inayolitia hasara kubwa taifa. Hata Rais Kikwete amekuwa akiitumia ndege hiyo mara chache kutokana na kutambua gharama kubwa za uendeshaji wa ndege hiyo. Licha ya ndege hiyo kununuliwa kwa gharama kubwa haiwezi kutua katika viwanja vingi vya ndege havya hapa nchini.
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Godius Kahyarara, ameitaka serikali kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa matumizi mbalimbali kupunguza matumizi ya mafuta, ili iweze kufanikiwa kupunguza mfumuko wa bei nchini.
Alisema njia itakayosaidia kupunguza mfumuko wa bei, ni matumizi makubwa ya nishati mbadala kama gesi ya majumbani na katika vyombo vya usafiri hasa magari ya serikali.
``Gesi tunayo ya Songosongo, lakini bila kuhamasisha matumizi yake, bei ya mafuta katika soko la dunia na hapa nchini itapandisha bei ya bidhaa nyingine, jambo ambalo litakwamisha jitihada za kupunguza mfumuko wa bei,`` alisema.
Kuhusu sekta ya miundombinu na kilimo ambazo kwa ujumla zimetengewa asilimia 19 ya bajeti yote, alisema sekta hizo zinapaswa kutengewa bajeti kubwa zaidi.
``Miundombinu isiangalie ujenzi wa barabara pekee, maana tuna-overload barabara zetu, tuangalie reli na ndege, lakini kwa kujua mchango wa kilimo chetu ambacho ni uti wa mgongo wa taifa katika kukuza uchumi``
Aidha, alisema sekta ya elimu inapaswa kwenda sambamba na ukuaji wa uchumi.
``Tujue namna elimu itakavyosaidia kupunguza uhaba wa wataalam ili kukuza uchumi wetu, tuiboreshe kwa lengo la kushindana katika ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi,``
Hata hivyo, alisema bajeti ya mwaka huu ni nzuri na kwamba imeangalia vitu muhimu na kumlinda mwananchi wa kawaida.
Mwenyekiti wa chama cha Sauti ya Umma (SAU), Bw. Paul Kyara, alisema bajeti hiyo ina mapungufu katika maeneo kadhaa, na kutoa mfano kuwa haijatoa kipaumbele kwa sekta ya kilimo iliyotengewa asilimia sita ya bajeti yote.
``Kilimo pamoja na kuwaajiri watu zaidi ya asilimia 80, kuchangia zaidi ya asilimia 40 ya pato la taifa, na asilimia 30 ya mapato ya fedha za kigeni, inawezekana vipi kikatengewa asilimia 6.8, tu, ``
Wakati huohuo, ubalozi wa Marekani nchini, umeipongeza bajeti ya Tanzania na kueleza kuwa inamuelekeo mzuri kwa Watanzania kujikwamua na umaskini.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na ubalozi huo, ilieleza kuwa Watu wa Marekani wamepongeza bajeti hiyo pia kwamba si tegemezi kama ilivyokuwa bajeti zilizopita. Pongezi nyingi zimeelekezwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Fedha kwa kutoa bajeti yenye muelekeo mzuri hasa katika sekta ya elimu, kwani itaboresha elimu nchini.
Saturday, 14 June 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment