(SOURCE: Nipashe, 2008-06-13 09:32:43. Na Boniface Luhanga)
Serikali imefanya marekebisho ya viwango vya ushuru kwa bidhaa mbalimbali kwa ama kuvipandisha, kuvishusha au kusamehe kwa mwaka ujao wa fedha wa 2008/09.
Hata hivyo, ushuru wa mafuta ya petroli, haukuguswa na viwango hivyo vipya vitaanza kutumika Julai Mosi, mwaka huu.
Hatua hiyo ilitangazwa jana mjini hapa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustapha Mkulo, wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2008/09 utakaoanza rasmi Julai Mosi.
Bidhaa zilizofanyiwa marekebisho ya ushuru kwa asilimia 12, viwango vya sasa na vya zamani kuwa ni vinywaji baridi kutoka Sh. 48 hadi Sh. 54 kwa lita, bia zinazotengenezwa na nafaka ya hapa nchini ambayo haijaoteshwa, kutoka Sh. 173 hadi Sh. 194 kwa lita.
Bia nyingine zote kutoka Sh. 294 hadi 329 kwa lita huku ushuru wa mvinyo unaotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango cha asilimia 25, ukipanda kutoka Sh. 940 hai Sh. 1,053 kwa lita.
Viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara vimebadilishwa ambapo zile zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka Sh. 4,775 hadi Sh. 5,348 kwa sigara 1,000.
Sigara zenye kichungi zinazotengenezwa kwa tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, zitapanda kutoka Sh. 11,266 hadi Sh. 12,618 kwa sigara 1,000.
Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b), pia zimerekebishwa ushuru kutoka Sh. 20,460 hadi Sh. 22,615 kwa sigara 1,000.
Tumbaku ambayo iko tayari kutengenezwa sigara (cut filler) inapanda kutoka Sh. 10,333 hadi Sh. 11,573.
Ushuru wa `cigar`, unabaki asilimia 30.
Ushuru wa bidhaa katika huduma za simu za mkononi unapanda kutoka asilimia saba ya gharama ya matumizi ya huduma, hadi asilimia 10 ya gharama hiyo. Sababu kubwa ya rekebisho hilo katika bidhaa ya huduma za simu ni kwenda sanjari na mfumuko wa bei (adjustment for inflation).
Serikali imepunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye mafuta mazito ya HFO, kutoka Sh. 117 hadi Sh. 97 kwa lita, lengo likiwa ni kupunguza gharama ya uzalishaji viwandani na kuongeza uwezo wa ushindani wa bidhaa katika soko.
Mfumo wa kutoza ushuru wa bidhaa kwenye magari pia umerekebishwa kutoka ule wa sasa wa asilimia 10 kwa magari yenye ukubwa wa injini cc 2000 na kuwa na viwango viwili vya asilimia tano na 10 kama ifuatavyo:
Magari yenye ujazo wa injini isiyozidi CC 1,000 lakini hauzidi cc 2000 kiwango cha ushuru kitakuwa asilimia tano ya thamani ya gari, wakati magari yenye ujazo wa injini unozidi cc 2,000, kiwango cha ushuru kitakuwa asilimia 10 ya thamani ya gari.
Kuhusu sheria zinazosimamia kodi za magari, viwango vya ada zake vimepunguzwa ambapo kwa magari yenye ujazo wa injini usiozidi cc 500 kutoka Sh. 50,000 hadi Sh. 30,000.
Kwa magari yenye ujazo wa injini unaozidi cc 500 lakini hauzidi cc 2500, kutoka Sh. 80,000 hadi Sh. 50,000 ambapo magari yenye ujazo wa injini usiozidi cc 1500 lakini hauzidi cc 2500 kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 120,000.
Magari yenye ujazo wa injini usiozidi cc 2500 lakini hauzidi cc 5000 kutoka Sh. 330,000 hadi Sh. 140,000 wakati yale yenye ujazo wa injini usiozidi cc 5000 kutoka Sh. 175,000 hadi Sh. 150,000.
Serikali imesamehe ada ya mwaka ya leseni za magari kwa matrekta ya kilimo lakini imeongeza ada ya usajili wa magari kutoka Sh. 27,000 kwa pikipiki na Sh. 20,000 kwa gari na kwamba ada hii inalipwa mara moja tu na mwenye gari.
Hatua zote hizo kwa pamoja, zitapunguza mapato ya serikali kwa takriban Sh. milioni 2,380.
Serikali imesamehe ushuru wa forodha kwenye majembe ya mkono pamoja na pembejeo nyingine zote za kilimo zinazoingizwa kutoka nje.
Vile vile, serikali imesamehe ushuru wa forodha kwenye mali ghafi na vifaa vinavyoagizwa na kampuni ya TANELEC kwa ajili ya kutengeneza mashine za kuongeza na kupunguza nguvu ya umeme.
Ushuru wa forodha kwenye shayiri pia umeondolewa lakini kwa ile itakayoagizwa na kampuni za bia za hapa nchini kwa kiwango isichozidi tani 20,000 hadi mwisho wa Desemba, mwakani.
Ushuru wa forodha kwenye mashine za jamii ya kompyuta zinazotambulika chini ya HSCODE 8443.31.00 na 844.32.00 kwa kuwa kompyuta kwa sasa hazitozwi ushuru wa forodha.
Ushuru wa forodha kwenye madini ya Sodium Sulphate, kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10 ili kupunguza gharama za uzalishaji viwandani.
Serikali imeondoa ushuru wa forodha kwa magari yaliyotengenezwa maalum kwa ajili ya ukusanyaji takataka yatakayonunuliwa na serikali za mitaa au mawakala waliodhinishwa na serikali za mitaa.
Mafuta ghafi ya kula, pia yameondolewa ushuru wa forodha wa asilimia 10.
Mafuta yaliyosafishwa kidogo (semi-processed), yataendelea kutozwa ushuru wa asilimia 10 ambapo hatua hiyo itaviweka viwanda vya mafuta hapa nchini katika nafasi nzuri ya kiushindani na vile vya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hatua hizo kwenye ushuru wa forodha kwa pamoja, zitapunguza mapato ya serikali kwa takriban Sh. Milioni 762.
Katika mwaka wa fedha wa 2008/09, serikali imepanga kupata mapato ya jumla ya Sh. trilioni 7.216 ambapo kati ya kiasi hicho, mapato ya ndani ni Sh. trilioni 4.729.
Mapato kutoka kwa wahisani ni Sh. trilioni 2.249 wakati Sh. Bilioni 58.000, serikali inatarajia kutokana na uuzaji wa hisa zake asilimia 21 katika benki ya National Microfinance (NMB).
Katika mwaka wa fedha wa 2008/09, serikali imepanga kutumia Sh. trilioni 7.216 ambapo matumizi ya kawaida yatakuwa Sh. trilioni 4.727 ambayo alisema ni chini ya mapato ya ndani ya Sh. trilioni 4.729.
Matumizi ya maendeleo yamepangwa kuwa Sh. trilioni 2.489 ambapo katika matumizi hayo kiasi cha, Sh. bilioni 1,551.100, kitatokana na fedha za wahisani kupitia miradi pamoja na basketi.
Kiasi kilichobaki cha Sh. bilioni 938.380, kitatokana na mchango wa wahisani kupitia misaada ya bajeti, mapato yatokanayo na mauzo ya hisa za serikali pamoja na ziada itakayotokana na mapato ya ndani.
Maeneo sita ambayo yamepewa vipaumbele katika bajeti hiyo kuwa ni miundombinu ya barabara Sh. bilioni 973.3, afya Sh. bilioni 803.8, kilimo Sh. bilioni 460, maji Sh. bilioni 230.6 na nishati Sh. bilioni 383.1.
Sekta hizo sita za miundombinu ya uchumi na huduma za jamii, zimetengewa takriban asilimia 64 ya bajeti yote ya mwaka 2008/09.
Friday, 13 June 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
13.06.2008 0140 EAT
Ni bajeti ya kuuma, kupuliza
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA UCHUMI
MHESHIMIWA MUSTAFA HAIDI MKULO (MB.),
AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2008/2009
DODOMA 12 Juni, 2008
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2008/09. Pamoja na hotuba hii, vipo vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina takwimu za bajeti. Kitabu cha Kwanza kinahusu makisio ya mapato. Kitabu cha Pili na cha Tatu ni vya makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Halmashauri za Miji na Wilaya. Kitabu cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa, pamoja na Halmashauri. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2008, ambao ni sehemu ya bajeti hii.
2. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya bajeti yamehusisha taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali, na wadau wengine. Kama ilivyokuwa mwaka jana, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walipata fursa ya kujadili Mwongozo wa Mpango na Bajeti mapema mwaka huu, na kutoa maoni yao hasa kuhusu vipaumbele vya bajeti hii ya 2008/09. Mwongozo wa Serikali wa Mpango na Bajeti ni hatua muhimu katika maandalizi ya bajeti, kwa kuwa unatoa fursa kwa wadau, na hasa Waheshimiwa Wabunge kutoa michango yao mapema kabla mapendekezo ya bajeti hayajakamilika na kuwasilishwa Bungeni kwa ajili ya kupitishwa rasmi. Kwa niaba ya Serikali, nachukua nafasi hii kutoa shukrani zangu kwa Waheshimiwa Wabunge kwa maoni yao ambayo kwa kiasi kikubwa yamezingatiwa katika bajeti hii. Utaratibu huu utakuwa wa kudumu, na tutautumia kwa pamoja kuweka mikakati itakayoharakisha utekelezaji wa ahadi ya Chama Tawala ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.
3. Mheshimiwa Spika, nawashukuru kwa dhati wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho ya bajeti hii. Napenda kuishukuru Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge, chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda, Mbunge wa Handeni, kwa kazi nzuri ya kuchambua mapendekezo ya bajeti kwa undani na kutoa ushauri katika maeneo mbalimbali ya bajeti hii. Ushauri wa Kamati hii umesaidia sana katika kuboresha bajeti ninayoiwasilisha leo.
4. Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani zangu kwa Wizara zote, Idara zinazojitegemea, Mikoa, Serikali za Mitaa, taasisi za kitaifa na kimataifa, na wawakilishi wa sekta binafsi, kwa michango yao iliyosaidia kufanikisha maandalizi ya bajeti hii. Naomba niishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2008 na nyaraka mbalimbali za kisheria ambazo ni sehemu ya bajeti hii. Aidha, napenda kuwashukuru wafanyakazi wenzangu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, nikianza na Naibu Mawaziri, Mhe. Jeremia S. Sumari (Mb.) na Mhe. Omari Y. Mzee (Mb.); Katibu Mkuu, Gray S. Mgonja, Naibu Makatibu Wakuu; Ramadhani M. Khijjah, John M. Haule na Laston T. Msongole, Wakuu wa Idara, Taasisi na Wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha na Uchumi. Aidha, namshukuru Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha hotuba hii kwa wakati. Mwisho nawashukuru kipekee wataalamu na wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu sera, mikakati na masuala mbalimbali ya kodi ambayo yamezingatiwa kwa kiasi kikubwa katika bajeti hii.
5. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii, kumshukuru aliyekuwa Waziri wa Fedha kabla yangu Mhe. Zakia Hamdani Meghji (Mb), na aliyekuwa Naibu wake Mhe. Abdisalaam Issa Khatib (Mb). Napenda pia kumshukuru aliyekuwa Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji Mhe. Juma Alifa Ngasongwa (Mb), na aliyekuwa Naibu wake Mhe. Gaudence Kayombo kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuongoza zilizokuwa Wizara mbili. Nimejifunza mengi kutoka kwao ambayo yananisaidia katika kuongoza Wizara hii mpya ya Fedha na Uchumi. Nawatakia afya njema.
6. Mheshimiwa Spika, leo asubuhi nilitoa maelezo ya mapitio ya utekelezaji wa sera za uchumi jumla katika mwaka wa 2007/08, na mtazamo wa Serikali kuhusu hali ya uchumi katika muda wa kati (2008/09 – 2010/11). Sasa napenda nitoe maelezo kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Sera za Bajeti ya mwaka 2007/08 hasa katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya mwaka huu wa fedha.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA SERA ZA BAJETI YA MWAKA 2007/08
7. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, bajeti ya mwaka 2007/08 imetekelezwa kwa msingi wa sera mbalimbali zilizotangazwa wakati wa kuwasilisha bajeti hiyo Bungeni mwezi Juni 2007. Sera hizo ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuimarisha mgawanyo wa fedha za bajeti kwa mujibu wa vipaumbele vya Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya 2005 na MKUKUTA, usimamizi mzuri wa matumizi ya Serikali, na uwajibikaji. Maelezo kamili ya utekelezaji wa sera hizo yanafuata.
8. Mheshimiwa Spika, mambo muhimu yaliyojitokeza katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa miezi tisa ya kwanza ya mwaka wa 2007/08 ni pamoja na yafuatayo:
(i) Bajeti yetu iliendelea kuwa tegemezi kwa misaada ya nje kwa kiasi kikubwa licha ya mapato ya ndani kuendelea kukua. Kwa hiyo, changamoto ya kwanza mwaka 2008/09 ni kuongeza mapato ya ndani na kudhibiti kukua kwa haraka kwa bajeti ya kawaida; ili tuanze kujitegemea.
(ii) Mchango wa mapato yasiyo ya kodi katika bajeti ni mdogo tukizingatia fursa zilizoko za kukusanya mapato mengi kutoka kwenye maeneo hayo. Serikali inaandaa mkakati maalumu wa kuimarisha vyanzo hivyo vya mapato.
(iii) Hata hivyo, mapato ya kodi yanakusanywa kama yalivyolengwa, na matarajio ni kwamba tutafikia malengo ya makusanyo ya mwaka mzima wa 2007/08 bila wasiwasi.
(iv) Taratibu za ununuzi wa Umma bado zinasumbua taasisi nyingi katika utekelezaji wa bajeti. Mpango wa kuviimarisha vitengo vya ununuzi Serikalini unaandaliwa. Aidha, Mpango Mkakati wa kujenga taaluma ya Ununuzi wa Umma unaandaliwa.
(v) Kwa ujumla wake, matumizi ya Serikali yanaendelea kulingana na bajeti na inatarajiwa kwamba bajeti ya 2007/08 itakuwa imetekelezwa kama ilivyoidhinishwa na Bunge, isipokuwa maeneo kadhaa yaliyofanyiwa uhamisho wa ndani kukidhi mahitaji ya dharura.
9. Mheshimiwa Spika, yako pia maeneo mengine ambayo Serikali iliahidi kuyatekeleza katika mwaka huu wa fedha unaokaribia kwisha. Ningependa kutoa maelezo mafupi ya utekelezaji wa ahadi hizo za Serikali kama ifuatavyo:
(i) Serikali ilitangaza kwamba ilikusudia kuondoa fedha zake zinazowekwa katika benki za biashara na kuzihamishia Benki Kuu, ili benki zisitumie fedha za Serikali kununulia dhamana za muda mfupi za Serikali (Treasury Bills), utaratibu ambao Serikali ilijikuta inalipa riba kwa fedha zake yenyewe. Sehemu kubwa ya fedha za Serikali katika amana zilizoko kwenye benki za biashara ni fedha za misaada na mikopo yenye masharti nafuu. Hatua ambazo zimeshachukuliwa katika zoezi hilo ni pamoja na hizi zifuatazo:-
(a) Serikali imeshatambua na kuhakiki akaunti zinazohusika.
(b) Serikali imeanza majadiliano na wahisani wanaochangia katika tatizo hili.
(c) Tumetambua mahitaji ya Benki Kuu ili iweze kuhimili usimamizi wa akaunti hizo zitakazofunguliwa hapo, na kuhakikisha kuwa Benki hiyo itaweza kutoa fedha hizo kwa wakati zitakapohitajika kwenda kwenye miradi.
(d) Utaratibu wa kufungua akaunti mpya Benki Kuu za miradi ya Serikali umeanza.
(ii) Serikali imeanza kutumia mfumo wa kisasa wa malipo “Tanzania Interbank Settlement System (TISS)” kwa majaribio, ili hatimaye mfumo huo utumike na kuondoa umuhimu wa akaunti za Serikali kuwa na fedha nyingi katika benki za biashara. Mfumo huu tayari unatumiwa na Mamlaka ya Mapato, katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali kutoka kwa walipakodi wakubwa. Aidha, Serikali inajiandaa kutumia mfumo huu wakati wa utekelezaji wa miradi itakayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la “Millenium Challenge Corporation” (MCC). Miradi hiyo itaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha ujao (2008/09). Chini ya mfumo huo, fedha za malipo ya ujenzi wa miradi husika zitaingizwa na kutumwa moja kwa moja kwenye akaunti bila kuandika hundi za malipo. Mfumo huu wa malipo unapunguza matumizi ya hundi na ya fedha taslimu.
(iii) Katika juhudi za kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani, Serikali, kupitia TRA, imefanya uchambuzi wa misamaha ya kodi kwa lengo la kuipunguza ili kuokoa mapato ya Serikali. Uchambuzi huo umebaini kwamba misamaha yote ya kodi inatolewa kwa mujibu wa Sheria. Sehemu kubwa ya misamaha inatolewa kwa wawekezaji katika sekta ya madini chini ya Sheria ya Madini na Mikataba husika, wawekezaji katika sekta nyingine wanaopewa Hati za Vivutio kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) chini ya Sheria ya Uwekezaji. Kundi lingine linalofaidika na misamaha ya kodi ni lile la Mashirika ya dini na asasi zisizo za Serikali, na hasa zile zinazotoa huduma kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Hata hivyo, kodi zinazosamehewa kwa kundi hili zinalipiwa na Serikali kwa utaratibu wa Hati ya Hazina (Treasury Voucher System).
10. Mheshimiwa Spika, Serikali sasa inatafakari na kuainisha marekebisho ya Sheria mbalimbali ambayo yatahitajika yafanywe ili kupunguza misamaha ya kodi na kuokoa mapato ya Serikali. Zoezi hili linaendelea.
11. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mapato inaendelea kutoa elimu ya biashara na kodi kwa walipa kodi wadogo ili kuwawezesha wapate ufahamu wa kutosha kuhusu biashara na ukokotoaji wa kodi. Mamlaka imekua ikitoa machapisho mengi yenye maelezo kuhusu maadili ya biashara, ujasiriamali, na ulipaji wa kodi – hasa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) , na kodi ya mapato.
12. Mheshimiwa Spika, kutokana na hatua ambazo Serikali inachukua – kwa mfano kupunguza matumizi ya hatifungani za Serikali katika soko la fedha na dhamana za Serikali, uamuzi wa Serikali wa kupunguza kiasi cha fedha zake kinachokaa katika benki za biashara; na usimamizi mzuri wa soko la Dhamana za Serikali, riba za mikopo ya benki zimeanza kushuka, na inategemewa kwamba zitaendelea kushuka. Aidha, Sheria ya Ukopeshaji Vifaa (Finance Leasing) imetungwa ili kuweka mazingira yatakayowezesha wananchi kupata mitambo na vifaa vya uzalishaji, usafirishaji, ujenzi, nk. kwa njia ya kukodi. Aidha zoezi la kuainisha marekebisho yanayotakiwa katika Sheria mbalimbali ili kuweka mazingira mazuri ya kuwezesha vyombo vya fedha vitoe mikopo ya nyumba, limekamilika. Mapendekezo ya marekebisho mbalimbali ya Sheria husika yataletwa Bungeni katika mwaka ujao wa 2008/09. Pamoja na hatua hizi, viko vyombo vya fedha ambavyo vinatoa mikopo ya nyumba kwa kutumia sheria zilizoko hivi sasa.
13. Mheshimiwa Spika, Serikali ilidhamiria kwamba katika kipindi cha miaka mitatu, itaongeza mtaji katika Benki ya Rasilimali (TIB) ufikie angalau shilingi bilioni 50. Dhamira hiyo sasa imekamilika. Bajeti ya 2008/09 imetenga shilingi bilioni 21 kwa ajili ya kuimarisha mtaji wa TIB, ambao utafika shilingi bilioni 50. Uamuzi huu wa Serikali ni wa makusudi kwa kutambua tatizo kubwa la ukosefu wa mikopo ya uzalishaji katika viwanda na kilimo.
14. Mheshimiwa Spika, baada ya kuimarisha mtaji wa benki hii, Serikali itaelekeza nguvu katika Benki ya Posta ambayo pia ni Benki ya Umma. Zoezi la kuirekebisha benki hiyo linaendelea. Tathmini ya awali ya Benki ya Posta ilionyesha kwamba benki hiyo ilihitaji iimarishwe kimfumo na ki-utendaji, kwanza ndipo ifanyiwe uamuzi kuhusu majukumu yake katika uchumi wa nchi. Kazi ya benki hiyo kujiimarisha inaendelea ambayo ni pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia, kufungua matawi mapya, kuongeza wateja na amana, na kubuni huduma mpya (new products). Hivi sasa Benki ya Posta inajiendesha vizuri na mkakati wa kuimarisha benki hiyo unaendelea.
15. Mheshimiwa Spika, zoezi la kuuza kwa wananchi asilimia 21 ya hisa za Serikali katika Benki ya NMB linakaribia kukamilika, baada ya hesabu za mwaka 2007 kukaguliwa. Kwa kuwa zoezi hili litakamilika baada ya Juni 2008, mapato yatokanayo na uuzaji wa hisa hizo yataingia katika bajeti ya Serikali ya 2008/09. Mapato hayo yanakadiriwa kuwa shilingi bilioni 58 baada ya kuondoa gharama zinazokadiriwa kufikia shilingi bilioni 5. Aidha mchakato wa kurekebisha na kubinafsisha Shirika la Bima la Taifa unaendelea kwa utaratibu wa kutenganisha majengo na biashara ya bima, badala ya utaratibu wa mwanzo ambao ulikuwa unachanganya biashara ya bima na majengo ya Shirika.
16. Mheshimiwa Spika, Serikali imeainisha utaratibu wa kuzitaka Wakala, Taasisi na Mashirika ya umma kuchangia katika bajeti ya Serikali kwa utaratibu utakaokubalika, kama nitakavyoeleza baadae. Aidha, utaratibu wa “retention” wa Wizara na Idara zinazokusanya maduhuli ya Serikali na kubakiza kiasi fulani cha mapato, umeimarishwa na sasa utatoa fursa nzuri kuwawezesha wale wanaokusanya maduhuli makubwa wasirudi nyuma.
MAPATO YA NDANI
17. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2007/08, Serikali ilikusudia kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kurekebisha mfumo wa kodi na taratibu za kusimamia ukusanyaji mapato ili kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua shilingi bilioni 3,502.583 (trilioni 3.5), sawa na asilimia 18.1 ya Pato la Taifa kwa takwimu zilizokuweko wakati huo, ikilinganishwa na asilimia 14.3 mwaka 2006/07. Kufuatia mabadiliko ya takwimu za Pato la Taifa, kiwango hicho cha asilimia 18.1 sasa ni sawa na asilimia 16.7.
18. Mheshimiwa Spika, baadhi ya hatua zilizochukuliwa ili kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ni pamoja na kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kupanua wigo wa kodi, na kusajili walipa kodi wapya. Aidha, chini ya Mpango Mkakati wa Pili wa Mamlaka ya Mapato (TRA Second Corporate Plan) kumekuwa na maboresho katika usimamizi, utendaji na uwajibikaji wa TRA. Kama nilivyosema awali, Serikali imeanza kutathmini mchango wa mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Wizara na Idara mbalimbali zinazokusanya mapato hayo, ili kubaini mapungufu na kufanya marekebisho yanayofaa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi.
19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2007/08, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Sura 148. Marekebisho haya yalitoa unafuu wa kodi kwa pamba za usafi wa watoto (pampers), na mitungi ya kuzimia moto kwa nia ya kuhamasisha matumizi yake. Aidha, Serikali ilipunguza kiwango cha chini cha kukokotoa kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 18.5 hadi asilimia 15, ili kupunguza mzigo wa kodi kwenye kipato cha wafanyakazi. Ili kulinda thamani halisi ya mapato, Serikali pia ilirekebisha viwango vya ushuru wa Bidhaa sanjari na kasi ya kupanda kwa fahirisi ya bei. Vile vile, Serikali iliongeza ushuru wa mafuta ya petroli na kurekebisha mfumo wa kutoza ada ya mwaka ya leseni za magari ili kuongeza uwezo wa Mfuko wa Barabara kumudu ongezeko la gharama za matengenezo ya barabara. Kwa ujumla matokeo ya hatua hizo yameonyesha mafanikio kama ilivyotarajiwa.
20. Mheshimiwa Spika, mapato ya ndani kwa kipindi cha Julai 2007 hadi Machi 2008 yalifikia shilingi 2,656.2 bilioni, ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi 2,633.9 bilioni katika kipindi hicho, sawa na asilimia 100.8 ya makadirio. Kodi ya mapato ya ajira (PAYE) na kodi ya mapato ya makampuni; na pia tozo ya kuendeleza ufundi stadi (Skills Development Levy) zimekuwa na mchango mkubwa katika mwenendo huu mzuri wa makusanyo ya mapato. Kwa upande mwingine, ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Wizara na Idara mbalimbali za Serikali, pamoja na ushuru na kodi zinazokusanywa kutoka bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, siyo wa kuridhisha. Hata hivyo, pamoja na vianzio hivyo vya mapato kutokufikia malengo, Mamlaka ya Mapato ilivunja rekodi yake kwa kukusanya shilingi bilioni 328.6 katika mwezi wa Desemba, 2007. Kiwango cha juu kilichowahi kukusanywa na TRA kabla ya Desemba, 2007 kilikuwa shilingi bilioni 259 zilizokusanywa mwezi Machi 2007. Mwenendo huu mzuri ni matokeo ya usimamizi thabiti wa utawala wa kodi katika TRA, utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Pili wa Mamlaka ya Mapato, na hatua mbalimbali za mapato ambazo zilipitishwa na Bunge katika bajeti ya mwaka huu wa 2007/08. Aidha, Mpango Mkakati wa Tatu wa TRA utaweka mkazo, pamoja na mambo mengine, katika kuongeza ukusanyaji wa ushuru na kodi za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
MIKOPO NA MISAADA YA NJE
21. Mheshimiwa Spika, misaada na mikopo ya masharti nafuu kutoka nje katika kipindi cha Julai 2007 hadi Machi 2008 ilifikia shilingi bilioni 1,873.781, ambayo ni asilimia 80 ya makadirio ya mwaka mzima. Fedha hizo ni pamoja na misaada na mikopo ya bajeti (General Budget Support – GBS) ambayo ilikuwa shilingi bilioni 956.038, zilizokwishatolewa na ambazo ni asilimia 8 zaidi ya makadirio ya mwaka mzima. Hali hii imetokana na sababu kuu mbili: ya kwanza ni kwamba fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika zilizotegemewa kuingia mwaka 2006/07, zilichelewa kutolewa na, zikaingia katika Akaunti ya Serikali mwaka huu wa fedha. Pili ni kwamba Wahisani wengi walitoa sehemu kubwa ya misaada yao ya bajeti mwanzoni mwa mwaka wa fedha sanjari na makubaliano chini ya Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA). Aidha, misaada na mikopo ya kisekta na programu maalum (basket funds) kwa kipindi cha Julai 2007 hadi Machi 2008 ilikuwa shilingi bilioni 383.786 ambazo ni asilimia 33 zaidi ya makisio ya mwaka mzima. Kwa upande mwingine, misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ilifikia shilingi bilioni 533.957 katika kipindi cha Julai 2007 hadi Machi 2008, sawa na asilimia 60 ya makisio katika kipindi hicho. Hii imetokana na kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya miradi kwa sababu mbalimbali.
MATUMIZI
22. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi tisa ya mwanzo ya mwaka wa fedha 2007/08, mwenendo wa bajeti kwa ujumla ni wa kuridhisha. Matumizi ya jumla yanaendelea kama yalivyoidhinishwa na Bunge. Hata hivyo, utekelezaji wa bajeti umekabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo mfumuko wa bei unaotokana na kupanda kwa bei ya chakula, bei ya mafuta ya petroli, na bei ya mbolea katika soko la dunia. Serikali imechukua hatua kadhaa kukabiliana na changamoto hizi.
Hatua hizo ni pamoja na kufuta ushuru wa mahindi kutoka nje ya nchi ili kutoa motisha kwa wafanyabiashara kuagiza mahindi kutoka nje. Hata hivyo hatua hii haikufanikiwa kwa kuwa nafaka hazipatikani katika masoko duniani kote. Aidha, kutokana na upungufu mkubwa wa saruji, Serikali ilipunguza ushuru wa saruji ili kuhamasisha uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje kuziba pengo. Hatua zaidi za kukabiliana na tatizo la ukosefu wa chakula zitaelezewa na Waziri wa Sekta hiyo, atakapowasilisha sera na bajeti ya Wizara yake.
23. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwisho wa Machi 2008, jumla ya matumizi ya Serikali ilikuwa shilingi bilioni 4,147.415 (trilioni 4.147) ikilinganishwa na makisio ya shilingi bilioni 4,836.919 (trilioni 4.836) katika kipindi hicho. Shilingi bilioni 2,451.925 (trilioni 2.452) ni matumizi ya kawaida, na shilingi bilioni 1,695.491 (trilioni 1.695) ni miradi ya maendeleo. Matumizi ya kawaida ni pamoja na mishahara, malipo ya mikopo na riba, pensheni, na uendeshaji wa Serikali. Kwa kuzingatia jumla ya mapato ya ndani na misaada ya nje ya shilingi bilioni 4530.0 na jumla ya matumizi ya shilingi bilioni 4147.4 ya bajeti ya kipindi cha Julai 2007 hadi Machi 2008 ilikuwa na ziada ya shilingi bilioni 282.6
24. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha huu unaoisha tarehe 30 Juni 2008, Serikali iliendelea na utaratibu wake wa kutumia kulingana na mapato yaliyoko. Utaratibu huu umeonyesha mafanikio makubwa katika kudhibiti matumizi ya Serikali na kuepuka kukopa kutoka soko la fedha la ndani kwa ajili ya kugharamia matumizi ya kawaida ya Serikali. Wizara ya Fedha na Uchumi pia imechukua hatua kadhaa za kuboresha zaidi utaratibu huo wa “tumia ulichonacho”, katika kutoa fedha kwa watumiaji mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa kuwezesha watumiaji kuwa na maoteo ya matolewo ya mgao wa fedha katika kipindi cha miezi mitatu, na kuimarisha Mtandao wa Kompyuta wa Mfumo wa Usimamizi wa Fedha (IFMS ) katika ngazi mbalimbali za Serikali. Aidha, Vitengo vya Wizara ya Fedha na Uchumi vya ufuatiliaji wa matumizi vimeimarishwa na vinakagua matumizi ya fedha za Serikali katika maeneo mbalimbali nchini.
UDHIBITI WA UNUNUZI WA UMMA
25. Mheshimiwa Spika, wakati wa kuwasilisha Bungeni bajeti ya Serikali ya mwaka 2007/08, Serikali ilieleza kwamba ilikuwa imetunga Kanuni za Ununuzi wa Umma katika Serikali za Mitaa ili kupunguza matatizo na migogoro ya ununuzi katika Halmashauri mbalimbali. Kanuni hizi zilichapishwa katika Gazeti la Serikali toleo namba 177 la tarehe 3 Agosti, 2007. Hata hivyo, imedhihirika kwamba, pamoja na kanuni hizo, upungufu wa wanataaluma ya ununuzi ni tatizo kubwa. Serikali imepanga kuviimarisha vitengo hivyo vya ununuzi ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa wataalam wa fani ya ununuzi. Aidha, usimamizi wa taaluma ya ununuzi wa umma inahamishiwa katika Wizara ya Fedha na Uchumi, kutoka Wizara ya Miundombinu. Uamuzi huu umezingatia ukweli kwamba sehemu kubwa ya bajeti ya Serikali inatekelezwa kwa njia ya ununuzi, hivyo kwamba usimamizi wa fedha za Serikali ni pamoja na usimamizi wa Ununuzi wa Umma.
26. Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti matumizi ya Serikali katika ngazi ya Halmashauri, Serikali itapitia upya Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura 290, pamoja na Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348, kwa lengo la kuainisha marekebisho yanayostahili ili kumpa uwezo Mlipaji Mkuu wa Serikali akisaidiwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, kusimamia na kudhibiti matumizi ya fedha kwenye Halmashauri.
KUPELEKA MADARAKA KWA WANANCHI (D by D)
27. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/08, Serikali iliongeza kasi ya kutekeleza sera ya kupeleka madaraka kwa wananchi kupitia Serikali zao za Mitaa. Utekelezaji huo umepitia katika Wizara za Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Kilimo, Chakula na Ushirika; Maji na Umwagiliaji; Afya na Ustawi wa Jamii; Miundombinu; na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na jumla ya shilingi bilioni 216.2 zilihamishwa kwenda kwenye Halmashauri kutoka kwenye Wizara hizo. Zoezi hili liliongeza kiwango cha bajeti za Halmashauri na kufikia jumla ya shilingi trilioni 1.074.6 mwaka 2007/08 kutoka shilingi bilioni 858.4 mwaka 2006/07.
28. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hii ya kupeleka madaraka kwa wananchi, Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto ambazo ni pamoja na kujenga uwezo wa Halmashauri ili ziweze kutekeleza kwa ufanisi majukumu yaliyohamishiwa kwao, kuboresha huduma kwa wananchi, kuhakikisha kwamba shughuli zote zinazohamishiwa huko zinapewa rasilimali za kutosha; na kuoanisha na kurahisisha taratibu za kupeleka fedha kwenye Halmashauri.
29. Mheshimiwa Spika, Wizara nyingine nane zimefanyiwa tathmini na kuainisha shughuli zitakazohamishiwa kwenye Halmashauri. Wizara hizo ni: Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi; Maliasili na Utalii; Nishati na Madini; Viwanda, Biashara na Masoko; na Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana.
30. Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa fedha nyingi zinazopelekwa katika Halmashauri zinawafikia walengwa na kutekeleza malengo yaliyokusudiwa, Serikali itaimarisha ufuatiliaji wa fedha hizo katika ngazi zote, ikiwemo Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo. Ili kufanikisha azma hiyo, Serikali katika mwaka wa fedha 2008/09 itaendelea kuimarisha uwezo wa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri za Wilaya na Mameya wote nchini ili waweze kusimamia utekelezaji wa bajeti, kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma katika mamlaka zao. Serikali pia inatafakari hatua za kuchukua kwa kushirikiana na wadau wengine kupunguza idadi ya akaunti za benki zinazopokea fedha kutoka vyanzo mbalimbali katika Halmashauri.
TUME YA PAMOJA YA FEDHA
31. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea na zoezi la kupitia na kuchambua Ripoti ya Tume ya Pamoja ya Fedha kuhusu vigezo vya kugawana mapato na kuchangia gharama za Muungano. Kama sehemu ya mchakato huo, Tume ya Pamoja ya Fedha inachambua maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ya ziada ili kuziwezesha Serikali hizo mbili kufikia maamuzi kuhusu mapendekezo ya Tume.
MWELEKEO WA BAJETI YA 2007/08 HADI 30 JUNI, 2008
32. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mwenendo wa utekelezaji wa bajeti ya 2007/08 hadi mwezi Machi 2008, Serikali inaamini kwamba lengo la ukusanyaji wa mapato litafikiwa kama ilivyopangwa ifikapo mwisho wa Juni, 2008. Mapato ya ndani yanategemewa kuvuka kidogo lengo la bajeti la shilingi bilioni 3, 502.583 (trilioni 3.5). Matokeo haya yanatokana na mwenendo wa kuridhisha wa ukusanyaji wa kodi hususan katika vianzio vya VAT na kodi ya mapato. Lengo la mapato ya ndani litafikiwa licha ya ushuru wa forodha na kodi zinazokusanywa kutoka kwenye bidhaa zinazotoka nje, na nyingine zisizo za kodi, kutofikia malengo. Misaada na mikopo ya bajeti kutoka nje inatarajiwa pia kuvuka lengo. Hata hivyo, uko wasiwasi kwamba misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo haitapatikana kama ilivyoahidiwa, kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa Serikali. Kwa upande wa matumizi, mwelekeo unaonyesha kwamba matumizi ya kawaida yatafikiwa. Matumizi ya maendeleo yanayotegemea fedha za ndani vilevile yatafikia lengo. Matumizi ya maendeleo yanayotegemea misaada ya nje kwa ajili ya miradi hayatafikia lengo.
CHANGAMOTO ZILIZO MBELE YETU
33. Mheshimiwa Spika, baadhi ya changamoto za kibajeti ambazo nchi yetu inakabiliana nazo ni pamoja na hizi zifuatazo:-
(i) Mahitaji ya fedha kwa ajili kutekeleza MKUKUTA, hasa ujenzi wa miundombinu ya uchumi na huduma za jamii, ni makubwa sana kuliko uwezo wa Serikali, hata kama mapato yanaongezeka. Zinahitajika juhudi za ziada kuhusisha sekta binafsi ya ndani na ya nje katika kutekeleza MKUKUTA.
(ii) Utegemezi mkubwa wa bajeti kwa misaada ya wahisani, ambayo haitabiriki, unaathiri mipango ya Serikali ya muda wa kati na utekelezaji wa mpango wa kila mwaka. Kwa hiyo, ingawa bado tutahitaji misaada ya nje, ni lazima tuanze mbio ya kujitegemea.
(iii) Utekelezaji wa bajeti ya Serikali katika maeneo ya ununuzi, na utoaji wa taarifa za matumizi ya fedha za Serikali, haujaimarika ipasavyo;
(iv) Utekelezaji wa bajeti hasa ya miradi katika sekta za miundombinu unakabiliwa na upungufu wa wakandarasi wenye uwezo, ujuzi, vifaa, na uzoefu wa kutosha. Tatizo hili linahitaji kuwekewa mkakati wa kuliondoa.
(v) Bei za mafuta ya petroli, vyakula, malighafi, na pembejeo, zikiendelea kupanda zitaathiri bajeti kwa kiasi fulani.
MISINGI NA SHABAHA YA BAJETI YA MWAKA 2008/09
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2008/09, Serikali itaendelea kutekeleza malengo ya kitaifa kama yalivyofafanuliwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2005, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na MKUKUTA. Aidha, mgawanyo wa fedha utaendelea kuzingatia maeneo ya kipaumbele ambayo yataleta msukumo katika uchumi na huduma bora za jamii. Vipaumbele ambavyo vimezingatiwa katika Misingi ya Sera za Uchumi Jumla nilizowasilisha leo asubuhi, ni pamoja na elimu, miundombinu, kilimo, afya, maji na nishati.
35. Mheshimiwa Spika, Malengo ya Bajeti ya mwaka 2008/09 ni pamoja na yafuatayo:
(i) Kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua asilimia 18.5 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 16.7 ya Pato la Taifa mwaka 2007/08;
(ii) Kuzingatia kwa makini vipaumbele vilivyoainishwa kupitia mchakato uliojumuisha sekta zote na wadau wengine na pia katika MKUKUTA, Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya 2005, na Malengo ya Milenia;
(iii) Kuanzia mwaka 2008/09, matumizi ya kawaida ya Serikali yatagharamiwa na mapato ya ndani, kwa asilimia mia moja na ushee;
(iv) Kuongeza nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali, ikiwa ni pamoja na kusimamia kwa dhati posho ambazo hazina uhusiano na tija na ambazo sio za kisheria;
(v) Aidha, katika kutekeleza bajeti ya maendeleo umuhimu wa kwanza utakuwa kulipa madeni ya mikataba ya ujenzi, na kukamilisha miradi inayoendelea hasa ya mbiundombinu na maji.
MAPATO:
36. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2008/09, mapato ya ndani yamelengwa kufikia shilingi bilioni 4, 728.595 (trilioni 4.728) sawa na asilimia 18.5 ya Pato la Taifa (kwa takwimu za sasa). Hili ni ongezeko la asilimia 31 kutoka mapato yanayotegemewa kukusanywa mwaka 2007/08. Ili kufikia lengo hili kubwa la ukusanyaji wa mapato ya ndani, hatua zifuatazo zitachukuliwa:
(i) Mkazo utawekwa katika kupanua zaidi wigo wa kodi, kwa kusajili walipakodi wapya na kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara.
(ii) Wigo wa kodi utapanuka kutokana na kasi ya kukua kwa uchumi hasa katika sekta ambazo zinatoa mchango mkubwa wa mapato ya Serikali. Usimamizi na udhibiti mzuri wa misamaha ya kodi pia utaongeza wigo wa kodi.
(iii) Kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa ushuru na kodi katika forodha.
(iv) Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tatu wa Mamlaka ya Mapato (TRA Third Corporate Plan) utaongeza uwajibikaji miongoni mwa walipakodi na watoza kodi kadhalika. Mpango huo unataka kuweka mkazo katika ufanisi wa ukusanyaji wa kodi.
(v) Serikali itaweka taratibu nzuri zaidi za kukusanya mapato yasiyo ya kodi. Matunda ya taratibu hizo yataonekana kuwa ya uhakika kuanzia mwaka 2009/10.
37. Mheshimiwa Spika, kutokana na kupanuka kwa shughuli za kiuchumi nchini, mapato ya Taasisi, Wakala na Mamlaka za Serikali yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kuziwezesha baadhi ya Taasisi hizo kuwa na mapato ya ziada ambayo yangeweza kuchangia mapato ya Serikali. Baadhi ya sheria zilizounda Mamlaka za Udhibiti na Usimamizi wa Umma haziweki bayana nafasi ya Waziri wa Fedha na Uchumi katika usimamizi wa fedha na rasilimali nyingine za umma, na hivyo uko mgongano kati ya Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348, na zile sheria zilizoanzisha Asasi hizo.
38. Mheshimiwa Spika, Serikali imeona kuna umuhimu wa Taasisi na Wakala za Serikali na Mamlaka mbalimbali ambazo zinatoza kodi ya huduma kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Kwa kuzingatia hili, Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348, itafanyiwa marekebisho ili kumpa mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kuzitaka Asasi hizo kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali kila mwaka kulingana na Bajeti za taasisi hizo. Utaratibu wa kuchangia utaainishwa katika Kanuni za Fedha za Umma.
MISAADA NA MIKOPO MIPYA:
39. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA), au Joint Assistant Strategy for Tanzania (JAST), kwa lengo la kuboresha mahusiano yetu na nchi wahisani na mashirika ya fedha ya kimataifa. Hatua hii itatuwezesha kuendelea kupata misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa MKUKUTA. Hata hivyo, uzoefu katika usimamizi wa misaada umebaini kwamba, wahisani wanachelewa kuthibitisha ahadi zao au wanatoa fedha kidogo kuliko walizoahidi, jambao ambalo linaadhiri utekelezaji wa miradi. Serikali inatafakari njia bora zaidi ya kusimamia misaada ya nje katika muda wa kati ili kuwe na uhakika wa upatikanaji wa fedha zinazoahidiwa na wahisani. Kama nilivyosema awali, kuanzia mwaka wa fedha 2008/09, Serikali imedhamiria kwamba matumizi yote ya kawaida yatatokana na mapato yetu ya ndani. Kwa maana hii, fedha zote za misaada zitaelekezwa kwenye programu na miradi ya maendeleo, kuchochea uchumi kukua kwa kasi zaidi.
MIKOPO YA NDANI:
40. Mheshimiwa Spika, kama ilivyokuwa katika mwaka 2007/08, Serikali itaendeleza Sera ya kutokukopa kutoka benki za ndani kupitia soko la dhamana na hatifungani za Serikali kugharamia bajeti yake hasa matumizi ya kawaida. Hata hivyo, dhamana na hatifungani za Serikali zitaendelea kuuzwa katika soko hilo ili kulipia zile zinazoiva (rollover) na kusaidia kudhibiti ujazi wa fedha. Aidha, kamati maalum ya usimamizi imeundwa kufuatilia kwa karibu mzunguko wa fedha za Serikali.
SERA ZA MATUMIZI
41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2008/09, Serikali itaendelea kuzingatia sera za matumizi ambazo zimekuwa zikitekelezwa mwaka uliopita, hasa kutoa kipaumbele katika kukuza uchumi, kuboresha huduma za jamii, kupeleka madaraka kwa wananchi, utawala bora, na uwajibikaji, na malengo ya uchumi jumla niliyo yaelezea kwenye Hotuba yangu ya Hali ya Uchumi leo asubuhi. Aidha, vipaumbele katika bajeti ijayo vimezingatia changamoto zilizoelezwa hapo awali pamoja na maoni ya Waheshimiwa Wabunge. Vile vile, Serikali itaendelea na utaratibu wa “kutumia tulichonacho” lakini utaratibu huo utaboreshwa. Usimamizi wa matumizi ya Serikali nao utaendelea kuimarishwa kwa kuziba mianya ya matumizi yasiyo na tija kwa kushirikisha ngazi zote za Serikali.
42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2008/09, Serikali imetenga fedha kwenye maeneo mengi muhimu kwa kuzingatia vipaumbele na mipango ya kitaifa niliyoeleza wakati nikiwasilisha Hotuba yangu ya Hali ya Uchumi wa Taifa (mwaka 2007) na mwelekeo wa muda wa kati (2008/09 - 2010/11). Napenda kutaja baadhi ya maeneo yaliyozingatiwa;
i) Maeneo makuu ya kipaumbele yametengewa fedha kama ifuatavyo:- Sekta ya Elimu imetengewa Shilingi trilioni 1.43 mwaka 2008/09 ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.086.0 mwaka 2007/08. Miundombinu ya barabara imetengewa shilingi bilioni 973.3 mwaka 2008/09 ikilinganishwa na shilingi bilioni 777.2 mwaka 2007/08. Sekta ya afya imetengewa shilingi bilioni 803.8 mwaka 2008/09 ikilinganishwa na shilingi bilioni 589.9 mwaka 2007/08. Sekta ya Kilimo imetengewa shilingi bilioni 460.0 mwaka 2008/09 ikilinganishwa na shilingi bilioni 379.0 mwaka 2007/08. Sekta ya Maji imetengewa shilingi bilioni 230.6 mwaka 2008/09 ikilinganishwa na shilingi bilioni 309.1 mwaka 2007/08, na Nishati imetengewa shilingi bilioni 383.4 mwaka 2008/09 ikilinganishwa na shilingi bilioni 354.0 mwaka 2007/08.
43. Mheshimiwa Spika, sekta hizo sita za miundombinu ya uchumi na huduma za jamii, zimetengewa takriban asilimia 64 ya bajeti yote ya 2008/09. Ukiongeza bajeti ya Utawala Bora ambayo ni moja ya maeneo makuu ya MKUKUTA, vipaumbele vya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala na MKUKUTA vitakuwa vimepata fedha zaidi ya asilimia 64 ya bajeti.
44. Mheshimiwa Spika, ningependa kutoa maelezo zaidi kuhusu sekta hizi muhimu, kama ifuatavyo:-
a) kwanza nianze na kilimo ambacho kimetengewa shilingi bilioni 438.1 au asilimia 6 ya bajeti ya 2008/09. Ni muhimu ieleweke kwamba fedha hizi hazijumuishi fedha zilizotengwa kwa Halmashauri za Wilaya ambazo pia zinahudumia kilimo. Aidha, kama nilivyoeleza awali, utekelezaji wa MKUKUTA ni jukumu la Serikali, Sekta binafsi, na wadau wengine wa maendeleo. Ni vizuri pia nieleze kwamba maendeleo ya kilimo yanategemea michango ya sekta nyingine kama vile miundombinu, mikopo na huduma nyingine za fedha, masoko, viwanda, n.k. Katika bajeti ya 2008/09, sehemu kubwa ya fedha zilizotengwa kwa kilimo zitaelekezwa katika ruzuku ya mbolea, Hifadhi ya Taifa ya Chakula (SGR), utafiti, hasa wa mbegu bora, na mafunzo. Serikali inategemea kwamba mahitaji mengine ya kilimo kama uzalishaji wa mbolea hapa nchini, na upatikanaji wa matrekta, ni jukumu la sekta binafsi, ikishirikiana na Serikali au Mashirika ya Serikali. Ni muhimu kukumbusha pia kwamba kilimo chetu kitakua cha kisasa chenye tija kama tutakuwa na viwanda vya kusindika mazao na kuacha kuuza nje mazao ghafi. Viwanda vinajengwa na sekta binafsi.
b) Miundombinu ya barabara imetengewa fedha za kutosha kulipa madeni yote ya mikataba ya barabara na kukamilisha miradi inayoendelea kulingana na mpangilio wa vipaumbele vya Wizara na Halmashauri husika.
c) Sekta ya afya imetengewa asilimia 11 ya bajeti ya 2008/09. Ni vizuri nieleze hapa kwamba fedha zilizotengwa kwa ajili ya sekta ya afya hazijumuishi zile zinazotolewa na wahisani na mashirika yasiyo ya Serikali nje ya mfumo wa Serikali, kama vile fedha za kupambana na Ukimwi, Malaria, na TB, na nyingine za namna hiyo ambazo zinasimamiwa na ama wahisani wanaotoa fedha hizo, au wakala wao. Ni vyema pia kukumbusha kwamba asilimia zaidi ya 20 ya huduma za afya zinatolewa na Mashirika ya Dini.
d) Bajeti ya Maji – inaonekana kushuka ikilinganishwa na mwaka huu wa 2007/08. Sababu kuu ni kwamba ujenzi wa mradi mkubwa wa maji Shinyanga na Kahama, umekamilika. Aidha mradi wa maji wa Monduli umepata fedha pungufu za wahisani mwaka ujao, kulinganisha na mwaka huu wa 2007/08.
e) Katika bajeti ya Nishati na Madini, ni vyema nieleze kwamba zile fedha zitokanazo na kufutiwa madeni ya IMF (MDRI), ambazo zilitumika kulipia mitambo na jenereta za kuzalisha umeme wa dharura na kulipia chakula likichoagizwa kutoka nje wakati ule wa uhaba wa chakula sasa zimekwisha. Hivyo miradi katika sekta hiyo sasa itategemea fedha za wahisani pamoja na za kwetu wenyewe.
f) Kama ilivyokuwa mwaka wa 2007/08, sekta ya elimu imetengewa fedha nyingi kuliko sekta nyingine zote. Hapana ubishi kwamba elimu ndio ufunguo wa maisha. Tumepanua sana fursa za watoto wote wa Tanzania kupata elimu, na tunafahamu kwamba mahitaji ya walimu, vifaa na nyenzo za kufundishia, maabara, chakula, n.k. vinahitajika na ni vya gharama kubwa.
45. Mheshimiwa Spika, pamoja na maeneo hayo sita ya miundombinu ya Uchumi na Huduma za jamii, liko eneo lingine muhimu la MKUKUTA yaani Utawala Bora, ulinzi na usalama, ambayo yana uzito sawa na yale maeneo sita niliyoyaelezea hapo juu. Yako pia maeneo mengine kama vile malipo ya madeni, pensheni, bima ya Afya, n.k.
46. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba mwezi Februari mwaka huu, Rais George W. Bush wa Marekani na Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walisaini mkataba wa “Millenium Challenge Compact” unaotoa msaada kwa Tanzania wa dola za Marekani milioni 698 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya barabara, umeme, maji, na uwanja mmoja wa ndege. Miradi itakayotekelezwa ni ya Tanzania Bara na Visiwani. Mkataba uliosainiwa na Marais hao wawili ni wa miaka mitano. Kwa mwaka wa kwanza wa utekelezaji (2008/09) kiasi kilichotengwa kwenye bajeti ni shilingi bilioni 68.5, kutegemea mpango wa kazi wa utekelezaji wa miradi hiyo ya “Compact”.
MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO:
47. Mheshimiwa Spika, Ili kujenga uwezo endelevu wa kukusanya mapato ya ndani kulipia matumizi yote ya kawaida, Serikali itachukua hatua mbali mbali za kuboresha ukusanyaji wa mapato, ikiweno kupanua wigo wa kodi kwa kusajili walipa kodi wapya na kuendelea kuimarisha uchumi tulivu, pamoja na kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji yenye kuiwezesha sekta binafsi kukua. Aidha Mamlaka ya Mapato itaanza utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tatu wa Maboresho (Third Corporate Plan) wa Miaka Mitano, kufuatia kukamilika kwa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maboresho.
48. Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza kufanyia marekebisho mfumo wa kodi, pamoja na kurekebisha baadhi ya viwango vya kodi, ushuru na tozo zisizo za kodi chini ya Sheria mbali mbali, na pia taratibu za ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali. Marekebisho hayo yanalenga kuweka mazingira mazuri zaidi ya uzalishaji hapa nchini kupunguza makali ya mfumuko wa bei, na kurahisisha ukusanyaji wa kodi. Maboresho hayo yatakuwa chini ya sheria zifuatazo:-
(a) Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani;
(b) Sheria ya Kodi ya Mapato;
(c) Sheria ya Ushuru wa Bidhaa;
(d) Sheria zinazosimamia Kodi za Magari;
(e) Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
(f) Sheria zinazosimamia Mapato yasiyo ya Kodi
A. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani:-
49. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura ya 148:-
(i) Kurekebisha na kupanua wigo wa huduma zinazotozwa asilimia sifuri ya Kodi ya Ongezeko la Thamani zinapokuwa zimetolewa kwa watumiaji wa nje ya nchi (export of services) ili kuhusisha huduma za ushauri wa kitaalam; huduma za mawasiliano ya simu; huduma za kurusha matangazo ya redio na luninga; huduma zinazotolewa na wakala; na huduma saidizi za uchukuzi na usafirishaji wa bidhaa. Hatua hii inakusudiwa kutoa motisha zaidi kukuza biashara ya kimataifa katika huduma ili kuongeza mchango wa sekta ya huduma katika fedha za kigeni na katika Pato la Taifa. Inapendekezwa hatua hizi zianze kutumika rasmi tarehe 1 Januari 2009 ili kutoa fursa ya kuandaa kanuni za kuzisimamia;
(ii) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye mafuta mazito yanayotumika kama nishati ya kupikia (kwa mfano “Moto Poa”) ili kuhamasisha wananchi kutumia mafuta hayo badala ya kuni na mkaa kwa matumizi ya nyumbani ili kulinda mazingira;
(iii) Kutoa msamaha maalum wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT Special Relief) kwenye “ethanol”; “dyienstuff” na “thickening agent” zinazoagizwa na kampuni ya Moto Poa kwa ajili ya kutengeneza mafuta mazito ya nishati;
(iv) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye gesi asilia iliyosindikwa (Compressed Natural Gas -CNG) na mitungi ya kuhifadhia gesi hiyo, kama ilivyo hivi sasa kwa gesi ya kupikia ya LPG, ili kuhamasisha matumizi ya gesi hiyo badala ya mafuta ambayo ni ghali, au mkaa ambao unaharibu mazingira;
(v) Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye lami (bitumen) ili kupunguza gharama za matengenezo ya barabara; na
(vi) Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye magunia yanayotengenezwa hapa nchini kwa ajili ya kuhifadhi nafaka itozwe katika kiwango cha asilimia sifuri.
Hatua hizi katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa pamoja zitapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 1,211 milioni.
B. Sheria ya Kodi ya Mapato:-
50. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo katika Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332:-
(i) Kuanzisha kodi mbadala ya mapato kwa kiwango cha asilimia 0.3 ya mauzo ghafi (gross turnover), kwa kampuni zinazoonyesha kupata hasara kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo. Aidha, kampuni hizi hupata faida ya kibiashara, (commercial profits) lakini katika kukokotoa faida inayostahili kulipiwa kodi hujikuta zinaonyesha hasara (tax loss) inayosababishwa na vivutio vya uwekezaji ikiwemo viwango vikubwa vya punguzo la gharama za mitaji (capital expenses) vinavyoruhusiwa kisheria;
(ii) Kuanzisha kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia 2 kwa malipo yote ya Serikali kwa wauzaji wa bidhaa na huduma Serikalini wasio na Namba ya Usajili ya Walipa Kodi (TIN);
(iii) Kusamehe kodi ya mapato inayotozwa kwenye faida itokanayo na mauzo ya mitaji (capital gains tax) kwa vipande kutoka katika mfuko wa uwekezaji wa pamoja ulioidhinishwa (Approved Collective Investment Schemes);
(iv) Kufanya marekebisho katika mfumo wa kodi binafsi ya mapato (Personal Income Tax) na mapato ya ajira ili kuzingatia ongezeko la kima cha chini cha mshahara Serikalini, na kulinda mapato ya ajira dhidi ya athari za mfumuko wa bei. Viwango vya sasa na vile vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo:
Viwango vya Sasa
Mapato kwa mwezi Kodi kwa Mwezi
Shilingi 0 mpaka Shilingi 80,000 Asilimia sifuri
Shilingi 80,001 mpaka Shilingi 180,000 Asilimia 15 ya kiasi kinachozidi Shilingi 80,000
Shilingi 180,001 mpaka Shilingi 360,000 Shilingi 15,000 kuongeza asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Shilingi 180,000
Shilingi 360,001 mpaka Shilingi 540,000 Shilingi 51,000 kuongeza asilimia 25 ya kiasi kinachozidi Shilingi 360,000
Zaidi ya Shilingi 540,000 Shilingi 96,000 kuongeza asilimia 30 ya kiasi kinachozidi Shilingi 540,000
Viwango Vinanyopendekezwa
Mapato kwa mwezi Kodi kwa Mwezi
Shilingi 0 mpaka Shilingi 100,000 Asilimia sifuri
Shilingi 100,001 mpaka Shilingi 360,000 Asilimia 15 ya kiasi kinachozidi Shilingi 100,000
Shilingi 360,001 mpaka Shilingi 540,000 Shilingi 39,000 kuongeza asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Shilingi 360,000
Shilingi 540,001 mpaka Shilingi 720,000 Shilingi 75,000 kuongeza asilimia 25 ya kiasi kinachozidi Shilingi 540,000
Zaidi ya Shilingi 720,000 Shilingi 120,000 kuongeza asilimia 30 ya kiasi kinachozidi Shilingi 720,000
Hatua hizi za Kodi ya Mapato kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 4,353 milioni.
C. Sheria ya Ushuru wa Bidhaa:-
51. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura ya 147 kama ifuatavyo:-
(i) Kupunguza kiwango cha Ushuru wa Bidhaa kwenye mafuta mazito ya HFO kutoka Shilingi 117 kwa lita hadi Shilingi 97 ili kupunguza gharama ya uzalishaji viwandani, na kuongeza uwezo wa ushindani wa bidhaa zetu katika soko;
(ii) Kurekebisha mfumo wa kutoza Ushuru wa Bidhaa kwenye magari kutoka mfumo wa sasa wa kutoza ushuru wa asilimia 10 kwa magari yenye ukubwa wa ingini unaozidi cc2000 na kuwa na viwango viwili vya asilimia 5 na asilimia 10 kama ifuatavyo:
(a) Magari yenye ujazo wa ingini usiozidi cc1000 hayatalipa ushuru wa bidhaa;
(b) Magari yenye ujazo wa injini unoazidi cc1000 lakini hauzidi cc2000 kiwango cha ushuru kitakuwa asilimia 5 ya thamani ya gari;
(c) Magari yenye ujazo wa ingini unaozidi cc2000 kiwango cha ushuru kitakuwa asilimia 10 ya thamani ya gari.
(iii) Kurekebisha kiwango cha ushuru wa bidhaa katika huduma za simu za mkononi kutoka asilimia 7 ya gharama ya matumizi ya huduma, hadi asilimia 10 ya gharama hiyo. Sababu kubwa ya rekebisho hili ni kwenda sanjari na mfumuko wa bei (adjustment for inflation);
(iv) Kurekebisha kwa asilimia 12 viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zinazotozwa ushuru huu kwa viwango maalum (specific rates), isipokuwa zile za mafuta ya petroli. Viwango vya sasa na vile vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo:
(a) Vinywaji baridi kutoka shilingi 48 kwa lita hadi shilingi 54 kwa lita;
(b) Bia inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa, kutoka shilingi 173 kwa lita hadi shilingi 194 kwa lita;
(c) Bia nyingine zote, kutoka shilingi 294 kwa lita hadi shilingi 329 kwa lita;
(d) Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi 940 kwa lita hadi shilingi 1,053 kwa lita; na
(e) Vinywaji vikali, kutoka shilingi 1,394 kwa lita hadi shilingi 1,561 kwa lita.
(v) Kurekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara kama ifuatavyo:-
(a) Sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 4,775 hadi shilingi 5,348 kwa sigara elfu moja;
(b) Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi 11,266 hadi shilingi 12,618 kwa sigara elfu moja;
(c) Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi 20,460 hadi shilingi 22,915 kwa sigara elfu moja;
(d) Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (“cut filler’) kutoka Shilingi 10,333 hadi shilingi 11,573 kwa kilo; na
(e) Ushuru wa “Cigar” unabaki asilimia 30.
D. Sheria zinazosimamia Kodi za Magari
52. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo katika kodi za magari:-
(i) Kupunguza viwango vya ada ya mwaka ya leseni za magari kama ifuatavyo:-
(a) Kwa magari yenye ujazo wa ingini usiozidi cc500 kutoka shilingi 50,000 hadi shilingi 30,000;
(b) Kwa magari yenye ujazo wa injini unaozidi cc500 lakini hauzidi cc1500 kutoka shilingi 80,000 hadi shilingi 50,000;
(c) Kwa magari yenye ujazo wa injini unaozidi cc1500 lakini hauzidi cc2500 kutoka shilingi 150,000 hadi shilingi 120,000;
(d) Kwa magari yenye ujazo wa injini unaozidi cc2500 lakini hauzidi cc5000 kutoka shilingi 330,000 hadi shilingi 140,000; na
(e) Kwa magari yenye ujazo wa ingini unaozidi cc5000 kutoka shilingi 175,000 hadi shilingi 150,000.
(ii) Kusamehe ada ya mwaka ya leseni za magari kwa matrekta ya kilimo
(iii) Kuongeza viwango vya ada ya usajili wa magari kutoka shilingi 27,000 kwa pikipiki na shilingi 90,000 kwa gari, hadi shilingi 35,000 kwa pikipiki na shilingi 120,000 kwa gari. Ada hii inalipwa mara moja tu na mwenye gari.
Hatua hizi kwa pamoja zitapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 2,380 milioni.
E. Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki:-
53. Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya marekebisho ya viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha yalijadiliwa pamoja na yale ya kutoka Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi katika kikao cha maandalizi ya Bajeti cha Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika tarehe 2 mwezi Juni 2008 Jijini Nairobi. Makubaliano ya Mawaziri wa Fedha yatawasilishwa katika Kamati ya Kisekta ya Mawaziri wa Biashara, Fedha na Uwekezaji ili wathibitishe kwa pamoja. Baada ya kuthibitishwa, yatachapishwa katika Tamko la Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Makubaliano hayo ni kama ifuatavyo:-
i. Kusamehe ushuru wa forodha kwenye majembe ya mkono pamoja na pembejeo nyingine zote za kilimo zinazoagizwa kutoka nje ili kupunguza mzigo wa gharama kwa wakulima hasa wale wadogo. Aidha, Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inatafiti uwezo wa nchi wanachama kuzalisha pembejeo hizo;
ii. Kusamehe ushuru wa forodha kwenye mali ghafi na vifaa vinavyoagizwa na kampuni ya TANELEC kwa ajili ya kutengeneza mashine za kuongeza na kupunguza nguvu ya umeme (transformers and switch gears);
iii. Kuondoa ushuru wa forodha kwenye shairi itakayoagizwa na kampuni za bia za hapa nchini kwa kiwango kisichozidi tani 20,000 hadi mwisho wa mwezi Desemba 2009;
iv. Kuondoa ushuru wa forodha kwenye mashine za jamii ya kompyuta (data processing machines) zinazotambulika chini ya HSCODE 8443.31.00 na 8443.32.00 kwa kuwa kompyuta hivi sasa hazitozwi ushuru wa forodha;
v. Kupunguza kiwango cha ushuru wa forodha kwenye madini ya “Sodium Sulphate” kutoka asilimia 25 hadi asilimia 10, ili kupunguza gharama za uzalishaji viwandani;
vi. Kutoa msamaha wa ushuru wa forodha kwa magari yaliyotengenezwa maalum kwa ajili ya ukusanyaji takataka yatakayonunuliwa na Serikali za Mitaa au mawakala walioidhinishwa na Serikali za Mitaa; na
vii. Kuondoa ushuru wa forodha wa asilimia 10 kwenye mafuta ghafi ya kula. Mafuta yaliyosafishwa kidogo (semi-processed) yataendelea kutozwa ushuru wa asilimia 10. Hatua hii itaviweka viwanda vya mafuta hapa nchini katika nafasi nzuri ya kiushindani na vile vya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hatua hizi katika Ushuru wa Forodha kwa pamoja zitapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi 762 milioni.
F. Sheria zinazosimamia Mapato yasiyo ya Kodi
54. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kurekekebisha Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, Sura ya 348 pamoja na Sheria zinazounda Wakala na Mamlaka za Usimamizi na Udhibiti pamoja na Asasi za Serikali ili kumpa mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kuzitaka Asasi, Wakala na Mamlaka hizo kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali kila mwaka kutokana na mapato ya ziada ya mashirika hayo.
G. Usimamizi wa Misamaha ya Kodi
55. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho yafuatayo katika Jedwali la Tatu la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kuimarisha usimamizi wa msamaha wa kodi unaotolewa kwa mashirika yasiyo ya Serikali kama ifuatavyo:-
(i) Kurekekebisha kifungu cha 10 cha Jedwali la Tatu ili kuyataka mashirika yanayonufaika na msamaha wa kodi kuwasilisha kwa Mamlaka ya Mapato maelezo ya utekelezaji wa , mipango yao ya kazi ya mwaka yakianisha manufaa kwa jamii. Aidha TRA itatoa hati ya stahili ya msamaha (Tax Clearance Certificate) itakayowezesha taasisi husika kuendelea kupata msamaha wa kodi;
(ii) Kurekebisha kifungu cha 10 cha Jedwali la Tatu ili kuyataka mashirika yanayonufaika na msamaha wa kodi kuwasilisha uthibitisho kwamba vifaa au huduma zinazoombewa msamaha wa kodi zitatumika katika miradi husika tu na si vinginevyo;
(iii) Kurekebisha kifungu cha 10 cha Jedwali la Tatu ili msamaha unaotolewa chini ya kifungu hiki usihusishe bidhaa za matumizi ya nyumbani (household consumables)
(iv) Kufuta kifungu cha 11 cha Jedwali la Tatu la Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kuwa tayari msamaha huu unatolewa katika kifungu cha 10;
H. Marekebisho madogo madogo katika baadhi ya Sheria za Kodi:-
56. Mheshimiwa Spika, inapendekezwa kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika Sheria mbalimbali za kodi ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake.
I. Tareheya Kodi Mpya Kutumika:-
57. Hatua hizi mpya za kodi zitaanza kutumika Julai mosi 2008, isipokuwa pale ilipoelezwa vinginevyo.
MFUMO WA BAJETI YA MWAKA 2008/09
58. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2008/09, Serikali imepanga kupata mapato ya jumla ya shilingi bilioni 7,216.130. Kati ya kiasi hicho, mapato ya ndani ni Shilingi bilioni 4, 728.595 na mapato kutoka kwa wahisani ni shilingi bilioni 2,429.535. Aidha, Serikali inategemea kupata shilingi bilioni 58.000 kutokana na uuzaji wa hisa zake asilimia 21 katika benki ya NMB.
59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, matumizi ya Serikali yatakuwa shilingi bilioni 7,216.130. Matumizi ya kawaida yatakuwa shilingi bilioni 4,726.650 ambayo ni chini ya mapato ya ndani ya shilingi bilioni 4,728.595. Matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi bilioni 2,489,480. Katika matumizi ya maendeleo, kiasi cha shilingi bilioni 1,551.100 kitatokana na fedha za wahisani kupitia miradi pamoja na basketi. Kiasi kilichobaki cha shilingi bilioni 938.380 kitatokana na mchango wa wahisani kupitia misaada ya kibajeti, mapato yatakayotokana na mauzo ya hisa za Serikali pamoja na ziada itakayotokana na mapato ya ndani. Kwa muhtasari, sura ya bajeti inakuwa kama inavyoonekana katika jedwali lifuatalo.
Sura ya Bajeti 2008/09
Mapato Shilingi Milioni
A. Mapato ya Ndani 4,728,595
(i) Mapato ya Kodi (TRA) 4,497,070
(ii) Mapato yasiyo ya Kodi 231,525
B. Mikopo na Misaada ya Nje Ikijumuisha MDRI/MCA(T) 2,429,535
C. Mauzo ya Hisa za Serikali 58,000
JUMLA YA MAPATO YOTE 7,216,130
Matumizi
D. Matumizi ya Kawaida 4,726,650
(i) Deni la Taifa 648,284
(ii) Wizara 2,478,099
(iii) Mikoa 85,743
(iv) Halmashauri 908,756
(v) Matumizi Maalum 364,391
(vi) Marekebisho ya Mishahara ya Serikali 241,377
E. Matumizi ya Maendeleo 2,489,480
(a) Fedha za Ndani 938,380
(b) Fedha za Nje 1,551,100
JUMLA YA MATUMIZI YOTE 7,216,130
HITIMISHO
60. Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka wa fedha 2008/09 itatekelezwa katika kipindi ambacho dunia nzima inakabiliwa na changamoto kubwa ya kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, bei ya nafaka, bei ya pembejeo za kilimo, na bei ya malighafi za viwanda. Ongezeko hilo limesababisha kasi ya mfumuko wa bei katika nchi zote duniani. Aidha, kuvurugika kwa masoko ya fedha ya kimataifa kunaweza kuathiri mtiririko wa vitega uchumi (FDI) kutoka nchi zilizoendelea kuja nchi zinazoendelea. Kwa hiyo, kunahitajika umakini mkubwa katika kuhimili athari za hali hii ya uchumi wa dunia. Hata hivyo, nchi zinazozalisha mafuta ya petroli zinategemewa kuendelea kunufaika na ongezeko la bei ya mafuta hasa kwa kuwa mahitaji ya nchi kama China, India, na Brazil ni makubwa. Aidha, urari wa malipo ya nje unaonyesha umuhimu mkubwa wa kuweka nguvu zaidi katika kukuza mauzo ya nje ya bidhaa na huduma, ili kuongeza uhimili wa uchumi dhidi ya misukosuko kama hii ya kupanda kwa bei ya bidhaa tunazoagiza kutoka nje.
61. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, kwa upande wa bajeti, changamoto zinazoikabili Serikali ni kutotabirika kwa misaada kutoka kwa wafadhili. Kwa hiyo, tunahitaji kupunguza kasi ya kuongezeka kwa matumizi ya kawaida, hasa yale ambayo hayawezi kurekebishwa iwapo mapato yatapungua. Ili kukabiliana na hali hiyo mambo yafuatayo yatazingatiwa katika mwaka ujao wa fedha;
(i) Kutekeleza kwa dhati azma yetu ya kupunguza utegemezi wa bajeti yetu kwa wafadhili. Kuanzia mwaka ujao wa fedha, matumizi ya kawaida yatakidhiwa na mapato ya ndani, na kiwango cha utegemezi wa bajeti nzima kwa ujumla kinatarajiwa kupungua hadi asilimia 34 ukilinganisha na asilimia 42 mwaka 2007/08. Ukiondoa mikopo ya nje, ambayo italipwa na Serikali, kiwango cha utegemezi kitapungua zaidi na kufikia asilimia 20.
(ii) Kudhibiti mfumuko wa bei kwa kuimarisha usimamizi wa ujazi wa fedha katika uchumi, na kuongeza mashauriano na wadau hasa mabenki ili kuwapa taarifa sahihi za sera za fedha (Monetary Policy), utekelezaji wake na muelekeo wake.
(iii) Kuongeza upatikanaji wa nafaka ambazo bei zake zinapanda kwa kasi na kuathiri maisha ya wananchi, ama kusitisha usafirishaji nje wa bidhaa hizo, au kuzitoza kodi ya mauzo nje, au hatua zote mbili kwa pamoja; na kuboresha miundombinu hasa ya usafiri vijijini, ili kupunguza gharama za kusafirisha chakula hadi maeneo ya miji; na
(iv) Hatua muhimu kuliko zote ni kutumia ongezeko la bei ya chakula duniani kama fursa ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula hapa nchini, kwa kuhimiza kuwekeza katika mashamba makubwa na kuhimiza wananchi walime chakula kwa wingi ili kujipatia chakula na kipato. Ni vizuri tuitumie changamoto ya upungufu wa chakula duniani kama fursa kubwa ya kuneemeka kwa kuzalisha chakula chetu wenyewe kwa wingi, kwa kuwa aridhi tunayo, watu tunao, na hali ya hewa inaruhusu.
62. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
(from: majira.co.tz, 13/06/2008)
Post a Comment