Tuesday, 26 February 2008

Ubunge Kiteto: CCM yashinda

*Nangoro amgaragaza Kimesera kwa kura 8,900

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekigaragaza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika uchaguzi mdogo wa ubunge kwenye jimbo la Kiteto, mkoani Manyara.

Ushindi huo unatokana na aliyekuwa mgombea wa CCM, Bw. Benedict ole Nangoro kumshinda mgombea wa CHADEMA, Bw. Victor Kimesera, katika uchaguzi uliofanyika juzi jimboni humo.

Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na kifo cha mbunge wa zamani wa jimbo hilo Bw. Benedict Nusurutia, aliyefariki dunia mwaka jana kwa maradhi.

Akitangaza jana matokeo ya uchaguzi huo, Msimamizi wa Uchaguzi huo, Bw. Festo Kang'ombe, alisema mshindi Bw. Nangoro alipata kura 21,506 dhidi ya kura 12,561 alizopata mshindani wake, Bw. Kimesera.

Wengine waliogombea ni PPT-Maendeleo ambapo mgombea wake, Bw. Juma Ali, alipata kura 110 huku Bw. Mashaka Fundi wa Sauti ya Umma (SAU) akipata kura 300 ambapo kura 734 ziliharibika.

Bw. Kang'ombe alisema waliojiandikisha kupiga kura walikuwa watu 74,626 huku waliopiga wakiwa ni watu 35,261 na kura halali zikiwa 34,477 na zilizokataliwa kura 734.

Akizungumza mapema kabla ya matokeo rasmi baada ya kuona 'chombo' chake kinazama, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe, alisema chama chake kinatafakari cha kufanya hasa baada ya kubaini kuwa watu wengi hawakushiriki kupiga kura.

"Lazima kuna kitu, haiwezekani watu wapatao 26,000 waliotarajiwa kupiga kura wasionekane. Tutaona ni hatua gani tuchukue," alisema.

Hata hivyo Bw. Kang'ombe alithibitisha kwamba uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu katika vituo vyote 222 licha ya rabsha za hapa na pale zilizotokea wakati wa kampeni.

Kampeni ziligubikwa na vurugu za hapa na pale hata kusababisha viongozi sita wa CHADEMA na askari mmoja wa mgambo kujeruhiwa na kulazwa hospitalini.

Kabla ya virugu hizo, Bw. Kimesera naye akiwa kwenye kampeni alilazimika kukimbizwa hospitalini Dar es Salaam, pale ilipodaiwa kuwa alilishwa sumu na maadui zake wa kisiasa.

Katika tuklio lingine helkopta ya CHADEMA ilishindwa kuruka baada ua kupata hitoilafu mjini Dodoma, huku CCM nayo kwa mara ya kwanza ikilazimika kutumia helkopta kwa kiichoelezwa ni kutokana na barabara kutopitika kutokana na mvua.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa jana, wafuasi wa CCM walishangilia na kuingia mitaani wakiandamana kushangilia ushindi huo.

Kutoka gazeti Majira, 26.02.2008
(Na Mwandishi Wetu, Kiteto -www.majira.co.tz)

No comments: