Saturday, 9 February 2008

Pinda Waziri Mkuu

Kikwete amteua Pinda Waziri Mkuu
*Aahidi kupambana na uovu serikalini
*Baraza la Mawaziri kutangazwa Jumatatu

RAIS Jakaya Kikwete amemteua Mbunge wa Mpanda Mashariki, Bw. Mizengo Pinda, kuwa Waziri Mkuu kuchukua nafasi ya Bw. Edward Lowassa, aliyejiuzulu juzi.

Uteuzi huo ulitangazwa jana na Spika wa Bunge, Bw. Samwel Sitta, katika kikao cha jioni na kutoa fursa kwa wabunge kumpigia kura za kumpitisha. Alipitishwa kwa kura 279 kati ya 282 sawa na asilimia 98.9 ambapo moja iliharibika huku mbili zikimkataa.

Mapema kabla ya upigaji kura, Spika kama kawaida alimkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Johnson Mwanyika, kutoa hoja ya kutaka kupitishwa kwa Waziri Mkuu mteule.

Kama ilivyotarajiwa, Mwanasheria Mkuu alimsifu Waziri Mkuu mteule kuwa ni mchapakazi, mwadilifu, msikivu, mnyenyekevu na mvumilivu aliyestahili nafasi hiyo.

Naye Waziri Mkuu Mteule, alipopewa nafasi hiyo alimshukuru Rais kwa kumteua na kuahidi kumsaidia katika shughuli zake za kuliongoza Taifa na hasa kusimamia shughuli za Serikali bungeni, lakini kubwa likiwa ni kuzingatia Katiba ya nchi.

Waziri Mkuu wa zamani, Bw. Edward Lowassa alipopewa nafasi ya kuzungumza, alimsifu Bw. Pinda na kusema Rais ameteua mtu anayefanana na Bunge hilo, kutokana na uchapakazi wake usio na kifani.

Msemaji wa kambi ya Upinzani bungeni, Bw. Hamad Rashid Mohammed (CUF), mbali na kumsifia Bw. Pinda alisema ameridhika na uteuzi na kuitaka kambi kumpa ushirikiano mkubwa ili kufanikisha malengo ya Taifa.

"Sisi hatuko hapa kwa lingine bali kuhakikisha matatizo ya wananchi yanamalizika na tukishahakikisha hilo tofauti zetu za kisiasa tutazimaliza," alisema Bw. Hamad na kuongeza kuwa hilo litawezekana kwa kushirikiana na Waziri Mkuu mpya.

Wengine waliopata nafasi ya kuzungumza na kumsifia Waziri Mkuu mteule, ni Mbunge wa Ukerewe, Bibi Getrude Mongella (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Anna Abdallah, Mbunge wa Mtera, Bw. John Malecela (CCM) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA).

Waziri Mkuu mteule ana elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako alijiunga mwaka 1971 na kuhitimu mwaka 1974 akipata Shahada ya Kwanza ya Sheria (LLB).

Kati ya mwaka 1974 na mwaka 1978 alikuwa akifanya kazi kama mwanasheria katika Wizara ya Sheria kabla ya kwenda Ikulu mwaka 1978 kuwa Ofisa Usalama wa Ikulu hadi 1982.

Kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 1992 aliteuliwa kuwa Katibu Msaidizi wa Rais chini ya Mwalimu Julius Nyerere na mwaka 1996 hadi mwaka 2000 alikuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri.

Waziri Mkuu mteule, Bw. Pinda kuanzia mwaka 2000 hadi 2005 alikuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Mwaka 2006 hadi anateuliwa kuwa Waziri Mkuu, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI.

Bw. Pinda ana uzoefu mkubwa wa kazi Ikulu, akiwa amefanya kazi kwa miaka saba chini ya Mwalimu Nyerere, miaka 10 na Alhaji Ali Hassan Mwinyi na miaka mingine na Bw. Benjamin Mkapa.

Akishukuru baada ya kupitishwa na Bunge, Bw. Pinda aliahidi kumsaidia Rais kupambana na maovu serikalini na kuomba ushirikiano wa wabunge wamsaidie.

"Kama lengo letu ni kusaidia wananchi na kuleta maisha bora ni kuhakikisha wabunge tunafanya hayo wananchi wanayotarajia tuwafanyie," alisema Waziri Mkuu mteule.

Hatua hiyo sasa inampa fursa Rais Kikwete ya kushauriana na Waziri Mkuu wake mara baada ya kumwapisha, ili kuunda Baraza jipya la Mawaziri ambalo nalo lilivunjwa juzi.

Bw. Pinda anakuwa Waziri Mkuu wa 10 tangu Uhuru akiwa ametanguliwa na
1. marehemu Mwalimu Nyerere,
2. Mzee Rashid Kawawa,
3. Mzee John Malecela,
4. Dkt. Salim Ahmed Salim,
4. Bw. Cleopa Msuya,
5. Bw. Joseph Warioba,
6. marehemu Edward sokoine,
7. Bw. Frederick Sumaye na
8. Bw. Lowassa.
9. ?
10. Mizengo Pinda

Spika wa Bunge, Bw. Sitta aliwatangazia wabunge kuwa Waziri Mkuu mteule ataapishwa leo na Rais Kikwete, Ikulu, Chamwino mjini Dodoma, saa 5 asubuhi.

Pia alisema Baraza la Mawaziri litatangazwa kesho kutwa na kuapishwa Jumatano ijayo. Kwa hali hiyo Bunge liliahirisha shughuli zake hadi Alhamisi.

from: Majira, 09.02.2008 1311 EAT
Na Said Mwishehe

No comments: