Mimi nasema:
Pamoja na yote yaliyosemwa na kutokea mimi napenda kuchukua njia mbadala (different angle of perspective).
Mheshimiwa Lowassa amefanya la maana sana kuamua kuachia madaraka kwa hiari yake bila shinikizo. Hili ni jambo la kistaarabu, kiungwana na kimaendeleo. Huko ndiko tunatakiwa kwenda na sio vita ya kumwaga damu. Tunapotofautiana au kutokuelewana au kukosea taratibu za kiungwana zinatakiwa kufuatwa na sio ugomvi.
Ni vizuri watanzania tuelewe kuwa kitendo alichofanya mhe Lowassa ni cha kujivunia.
Pia hiki kitendo cha Mhe Lowassa inabidi tukipime kwa mapana na marefu, hasa kutoka kutoka kila pembe kimtazamo.
Ndio, nakubali, amekiuka taratibu lakini kwa upande mwingine ametupa urithi mkubwa watanzania; utamaduni wa kujiuzulu!!
Ameonyesha ujasiri wake sio ktk maneno matupu bali hata ktk kuchukua maamuzi, tena maamuzi mazito na ya kihistoria.
Asante. 08/02/2008
..........................................................................
Kutoka gazeti 'majira' 11/02/2008:
Askofu ampongeza Lowassa kujuzulu
ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi
ya Dodoma, Dkt. Peter Mwamasika amepongeza kitendo cha
aliyekuwa Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa kujiuzulu na kusema ni cha ujasiri.
Akitoa mahubiri katika ibada ya asubuhi Dodoma jana,
Askofu Mwamasika alisema uamuzi huo haukuwa rahisi na kwamba umeonesha jinsi Bw. Lowassa anavyokumbuka mafundisho ya dini na kumwogopa Mungu.
"Nilidhani zile hisia za Kimasai na Kimeru zingechanganyika na kumfanya aseme siondoki," alisema Askofu Mwamasika na kusababisha kicheko kwa waumini wake.
"Natarajia watakaoteuliwa watamwogopa Mungu kwani watatumia vitabu vitakatifu kuapa," alisema Askofu Mwamasika na kuongeza kwamba watakapokutwa na kashfa watatakiwa kufuata njia iliyooneshwa na Bw. Lowassa.
Askofu Mwamasika alilinganisha uamuzi wa Bw. Lowassa na kinachotokea nchini Kenya hivi sasa na kusema kuwa Tanzania imebarikiwa.
"Wenzetu huko wanakataa na sasa wanaoumia ni watu wa chini, hivi ingekuwa ni Kenya, kisha Bw. Lowassa akasema Wamasai na Wameru ninatakiwa kuondoka, anzeni kazi, pangekalika?" Alihoji Askofu Mwamasika.
Alisema tofauti ya kinachoonekana Kenya, Tanzania makabila yanazungumza kwa utani na wakati mwingine utani huo unazungumzwa katika mambo muhimu.
"Jana wakati wa kumwapisha waziri mkuu mpya, kule Chamwino, niliona mahali wamekaa mawaziri waliopita na baadhi yao walikuwa Wasukuma na Wanyamwezi, walimwambia Dkt. Msabaha (Ibrahim) na Bw. Karamagi (Nazir) kwa utani kwamba, nyinyi mmesababisha tumekuwa si mawaziri tena," alisema Askofu Mwamasika na kuongeza kuwa mazungumzo hayo yalikuwa muhimu lakini yalifanyika katika hali ya utani huku wote waliokuwepo wakicheka.
"Ninakumbuka waliwahi kuja wageni wanne kutoka Kenya, wakajitambulisha kuwa wapo watu watatu na Mkikuyu mmoja," alisema Askofu huyo na kuongeza kwamba kwa mtazamo wao, Mkikuyu anakuwa mtu akiwa ndani ya Kenya tu na kwamba nje nchi hiyo si mtu.
Aliwataka waumini kuliombea Baraza jipya la Mawaziri linalotarajiwa kutangazwa leo ili lisaidie kutekeleza wajibu wao na kuondoa umasikini nchini.
Source: Majira, 11.02.2008 0059 EAT
Na Joseph Lugendo
........................................................................
kutoka gazeti 'majira' 12/02/2008 habari zasema:
... NCCR-Mageuzi imemtetea aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Lowassa ikisema hakutendewa haki kwa kunyimwa nafasi ya kusikilizwa na Kamati Teule.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, alipozungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa kama angepewa fursa hiyo, mambo mengi yangefichuliwa.
"Kama ningekuwa Rais nisingemkubalia ajiuzulu bila kueleza yale aliyotaka kuyasema," alisema Bw. Mbatia.
Alisema kauli ya Bw. Lowassa bungeni Dodoma, kuwa hakupewa nafasi ya kusikilizwa na Kamati ya Bunge, ilitosha kumwezesha Rais Kikwete, kutomkubalia kujiuzulu ili aweze kusikilizwa.
"Naamini kama angepewa nafasi hiyo angeeleza mambo mengi na sasa hivi tungekuwa tunazungumza mengine," alisema Bw. Mbatia na kuongeza kuwa kauli ya Bw. Lowassa aliyoitoa bungeni kwamba maneno ya mitaani yakianza kusikilizwa ndani ya chombo hicho, hakuna atakayebaki, inabeba ujumbe mzito na ni wosia mzito kwetu," alisisitiza Bw. Mbatia.
Kuhusu ripoti ya Richmond alisema yaliyojitokeza katika mkataba huo ni sawa na tone la maji ndani ya bahari. Alitolewa mfano mkataba wa IPTL na kusema Watanzania wanabebeshwa mzigo wa kulipa sh. bilioni 3.6 kwa mwezi hata kama umeme haukuzalishwa.
Alisema wanachotaka Watanzania ni kuona fedha zilizochotwa kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) zinarejeshwa na mikataba kama ya IPTL inavunjwa. Alitaja mambo mengine yaliyojificha kuwa ni ununuzi wa ndege ya rais na rada.
Katika hatua nyingine Bw. Mbatia alielezea kushangazwa kwake na jinsi wabunge walivyokuwa wakichangia ripoti ya Richmond kwa ushabiki.
"Nimeshangaa kuona lugha za kishabiki na jazba zinatolewa na wabunge," alisema Bw. Mbatia.
Source: majira, 12/02/2008
Na Reuben Kagaruki
Mtaa wa Lugoda, Eneo la Gerezani, Simu:2118381,2119893 Faksi:2128640, 2118382
Friday, 8 February 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment