Richmond 'yatafuna' watatu: Lowassa, Karamagi, Msabaha wajiuzulu
MZIMU wa Richmond sasa umeanza kutafuna Baraza la Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Nne, baada ya mawaziri watatu akiwamo Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa kutangaza kujiuzulu, kutokana na kutajwa katika tuhuma za kuipa zabuni kampuni hiyo.
Wengine waliotangaza kujiuzulu jana ni pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Nazir Karamagi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ibrahim Msabaha.
Hatua hiyo inafanya hatma ya uhai wa Baraza la Mawaziri la sasa kubakia kiganjani mwa Rais Jakaya Kikwete, kwa kuwa Bw. Lowassa ndiye Kiongozi Mkuu wa shughuli za Serikali kila siku na bungeni, hivyo kutokuwapo kwake ni sawa na kukosekana kwa uhai wa Baraza la Mawaziri.
Akitangaza uamuzi wake bungeni jana, Bw. Lowassa alisema alitafakari kwa makini jinsi taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe, ilivyofanya kazi yake na kuwasilisha taarifa yake ambayo alidai haikumtendea haki, hivyo kuamua kumwandikia Rais barua ya kuomba kujiuzulu.
"Mheshimiwa Spika napenda kumpongeza Dkt. Mwakyembe kwa kuwasilisha taarifa ya Kamati kwa mbwembwe nyingi sana, nataka kuweka kumbukumbu ya kutoridhika kwangu katika hoja hii, Dkt. Mwakyembe ni mwanasheria, alifundisha vyuo Vikuu, anatambua maana ya Natural Justice (kutenda haki).
"Kamati Teule iliwaita watu wote mpaka Marekani, lakini mimi niliyetuhumiwa hawakuniita hata siku moja, umbali kutoka ofisini kwangu mpaka ofisi za Bunge ni karibu hata ningekosa gari ningekwenda kwa miguu, kulikuwa na shida gani kuniuliza Waziri Mkuu ulitoa dokezi hili je ni sawa?," alihoji Bw. Lowassa.
Aliendelea: "Taifa letu ni changa, chombo hiki (Bunge), ndicho chenye demokrasia na kinatakiwa kuwa na haki, kama haki, Demokrasia haitatendeka, basi nchi yetu haitakwenda vizuri, naona si sahihi, nimefadhaika sana, nimeonewa sana, nimedhalilishwa sana, Mheshimiwa Spika nimetafakari kwa makini jambo hili, nimejiuliza hivi kulikoni? Tatizo ni Waziri Mkuu ... kwa niaba ya Serikali na kwa niaba ya chama changu, nimeandika barua kwa Rais kuomba kuachia ngazi," alisema Waziri Mkuu.
Alisema hajui sababu za Kamati hiyo kuamini minong'ono ya mitaani, kabla ya kumuuliza yeye kama mtuhumiwa na kwamba alimpa taarifa Spika Bw. Samwel Sitta, kuwa katika taarifa ya Kamati hiyo, hakukuwa na maelezo yake.
Alisema yapo hadi magazeti ya udaku ndani ya taarifa hiyo na kwamba kujenga hoja bungeni ambapo nchi nzima wanasikia na kushuhudia moja kwa moja kupitia vyombo vya habari, kuonesha kwamba amefanya jambo fulani bila kuhojiwa ili kujua ukweli si jambo la kawaida.
"Naona moyo wangu mweupe, namshukuru sana mheshimiwa Rais kwa uteuzi wake kwangu kuwa Waiziri Mkuu kwa miaka miwili, nakushukuru Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana mawaziri na naibu mawaziri, nawashukuru waheshimiwa wabunge kwa heshima mliyonipa kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM," alisema Bw. Lowassa.
Mara baada ya hotuba hiyo fupi ya Waziri Mkuu, joto lilizidi kupanda ndani ya Bunge kutokana na mshituko mkubwa ambapo wabunge kadhaa walisimama kuomba mwongozo wa Spika, kuhusu kuendelea kwa mjadala au kusitisha shughuli za Bunge kwa muda, ili kutoa nafasi ya kutafakari jambo hilo.
Wabunge waliosimama kuomba mwongozo wa Spika juu ya suala hilo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe (CHADEMA), Mbunge wa Karatu Dkt. Wilbrod Slaa (CHADEMA), Mbunge wa Muleba Kusini, Bw. Willson Masilingi (CCM) baada ya kuombwa na Spika, Mbunge wa Bukoba Mjini Balozi Khamis Kagasheki na wengine ambao hata hivyo hawakupewa nafsi ya kuzungumza.
Akihitimisha hoja ya wabunge hao ambayo ilitaka kuleta mvutano wa aina fulani huku wengine wakiomba mwongozo wa kuendelea na mjadala na wengine wakitaka wapate nafasi ya kutafakari kwanza, Bw. Sitta alisema:
"Naona kama mnanipeleka mbali, sasa naamua, kutokana na hali hii isiyokuwa ya kawaida, nasitisha Bunge kwa muda hadi saa 11 jioni, ili nipate ushauri wa kisheria na kuwasiliana na mamlaka za juu," alisema na kuhitimisha mjadala huo.
Awali akiwasilisha taarifa yake bungeni juzi, Dkt. Mwakyembe, alisema Kamati yake haikumhoji Waziri Mkuu moja kwa moja, kwa kuwa watu ambao wangetoa ushahidi wa kuwafanya wamwite Waziri Mkuu hawakufanya hivyo, hivyo wasingemwita.
"Watu pekee waliokuwa na ukweli wenyewe, ukweli ambao ungeipa Kamati Teule msingi wa kumhoji Waziri Mkuu kwa kiapo, walikuwa watatu; Waziri Dkt. Msabaha (Ibrahim), Katibu Mkuu Mwakapugi na Mwenyekiti wa Bodi Balozi Kazaura, Kamati Teule mara mbili iliwaita Dkt. Msabaha na ndugu Arthur Mwakapugi kwa mahojiano zaidi, wote wawili walikataa kupokea maagizo kutoka kwa Waziri Mkuu ya kuipa Richmond upendeleo.
"Lakini Dkt. Ibrahim Msabaha baada ya mahojiano chini ya kiapo, akaiuma sikio Kamati Teule kuwa katika suala hilo yeye atakuwa kondoo wa kafara tu, au kwa maneno yake mwenyewe 'Bangusilo' kwa lugha ya kizaramo," alisema Dkt. Mwakyembe na Kuongeza:
"Maelezo ya Waziri nje ya kiapo yalioana na maelezo aliyotoa Balozi Kazaura nje ya kiapo Novemba 30, 2007, ambapo baada ya kumaliza mahojiano na Kamati Teule kwa kiapo, akatoa maelezo ya ziada kuwa Richmond ilikuwa mradi wa Bwana Mkubwa na mshirika mkubwa kibiashara akimaanisha Waziri Mkuu na Rostam Aziz," alisema.
"Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Balozi Kazaura kuhusisha uteuzi wa Richmond na mkono wa Waziri Mkuu, mara ya kwanza ilikuwa Januari 2007 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara, nimelazimika kueleza mambo tuliyoelezwa kwa siri kiungwana kutokana na uzito wa suala lenyewe na dhamana kubwa tuliyopewa na Bunge kueleza kilichotokea kwa uwazi na ukweli.
“Lakini ushahidi huu wa ziada na nje ya kiapo wa viongozi hao wawili haukutoa msaada stahili kwa Kamati Teule, kwa kuwa msingi wa uamuzi wote wa Bunge si minong'ono au tetesi, bali taarifa zenye uthibitisho halisi," alisema Dkt. Mwakyembe.
Alisema Kamati hiyo ilibaini, kwamba hali ya uoga na ya kutojiamini inawakumba Watanzania walio wengi, hususan pale wanapotakiwa kuelezea kwa uwazi maneno yale yale wanayoyanong’ona pembeni kwa hamasa kubwa na kwamba kwa mtindo huo, Taifa linaweza kuishia kuwa la walalamishi wasio na ujasiri wala dhamira ya dhati ya kukemea maovu inapobidi.
Baadhi tu ya vipengele vilivyomgusa Bw. Lowasa moja kwa moja katika taarifa hiyo ni pamoja na barua ya Katibu wake aliyeandikwa kwa jina moja la Bw. B. Olekuyan ya Juni 21 mwaka juzi, kwenda Wizara ya Nishati na Madini iliyoeleza kuwa Bw. Lowassa alikubali mapendekezo na ushauri wa Waziri wa Nishati na Madini, kuhusu Serikali kuteua kampuni ya Richmond kuingia mkataba na TANESCO.
Katika taarifa hiyo, pia ilielezwa kuwa barua nyingine iliyotoka kwa Waziri wa Nishati na Madini, Juni 19 mwaka juzi kwenda kwa Bw. Lowassa ikieleza kwamba Kamati ya Serikali ya Majadiliano na Richmond ilikuwa tayari imekamilisha majadiliano, hivyo kupendekeza Serikali iiteue kampuni hiyo kwa lengola kuingia mkataba wa kuzalisha umeme na TANESCO.
Akinukuu sehemu ya barua hiyo, Dkt. Mwakyembe alisema: “Kamati ya Serikali ya Majadiliano (GNT), inayojumisha wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Benki ya Tanzania (BoT) na TANESCO, ilifanya majadiliano na Richmond ya Marekani tangu Juni 8-16,” alisema akinukuu barua hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara tu baada ya kutoka ukumbini, Bw. Lowassa alisema huo ndio uamuzi wake kwa sasa. Alipoulizwa itakuwaje kama Rais atakataa kujiuzulu kwake alisema: "Nitafikiria kwa wakati huo." Alipotakiwa kumtaja Waziri Mkuu mtarajiwa kutokana na kauli yake kwamba 'tatizo ni Waziri Mkuu,' alijibu kwa kifupi: "sijui".
Hata hivyo kujiuzulu kwa Waziri Mkuu kuliandika historia mpya ambapo mtu wa kwanza kumsalimia na kutoka naye nje ya eneo lake hadi karibu na mlango wa kutokea alikuwa ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Bw. Hamad Rashid Mohamed (CUF).
Habari zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zilisema Rais Kikwete aliwakubalia viongozi hao maombi yao ya kujiuzulu na kwamba huenda leo Waziri Mkuu mpya akatangazwa.
kutoka: gazeti majira, 08.02.2008 0123 EAT
Na Waandishi Wetu, Dodoma
Richmond aibu! *Lowassa, Karamagi, Msabaha, Mwanyika, Hosea mh!
WINGU jeusi juu ya hatma ya Baraza la Mawaziri limetanda mkoani hapa baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Kamati Teule ya Bunge, iliyochunguza mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura ulioipa ushindi kampuni ya Richmond Development Company, kumhusisha moja kwa moja Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa.
Taarifa hiyo iliyosomwa bungeni jana asubuhi na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe (CCM), iliacha wingu hilo baada ya mapendekezo ya mwisho ya kamati hiyo kumtaka Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa kupima uzito wa yanayomuhusu na kufanya uamuzi wa 'busara'.
Weusi wa wingu hilo, ulizidi kuongezeka baada ya kikao cha Bunge
kuahirishwa jana asubuhi kwa ajili ya kutoa nafasi kwa wabunge kupitia na kutolewa taarifa kwa wabunge kwenda kumpokea Rais Jakaya Kikwete aliyetarajiwa kuwasili jana alasiri.
Wabunge hao kwa pamoja wanatakiwa kuhakikisha wameipitia, ili wawe tayari kuijadili kwa siku mbili mfululuzo, kuanzia leo asubuhi.
Taarifa ya kwenda kumpokea Rais Kikwete aliyeelezwa kuwa na kauli
ya mwisho kuhusu Baraza la Mawaziri, iliambatana na taarifa ya
kuwakumbusha wabunge wote wa CCM, kuhudhuria kikao maalumu
kilichotarajiwa kuanza saa mbili usiku.
Kikao hicho kilichokuwa kikisubiriwa kwa hamu na baadhi ya wabunge wa
CCM, kilielezewa kufanyika kwa ajili ya kuhoji wote waliotajwa katika ripoti hiyo.
Pamoja na ripoti hiyo kupendekeza baadhi ya mawaziri, akiwamo Waziri
wa Nishati na Madini, Bw. Nazir Karamagi, Waziri wa zamani wa wizara
hiyo ambaye ni Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Ibrahim
Msabaha, wachukuliwe hatua kali, kamati hiyo pia ilieleza kutofurahishwa na taarifa zilizomgusa Bw. Lowassa moja kwa moja.
Aidha Kamati hiyo ilipendekeza Bunge lililoidhinisha uteuzi wa Bw.
Lowassa, kuangalia athari za matokeo ya ripoti hiyo katika hadhi na
uzito wa Waziri Mkuu, katika utekelezaji wa shughuli za Serikali
bungeni.
Mapendekezo mengine ya kamati hiyo yalishabihiana na kauli ya hivi karibuni ya Rais Kikwete ya kuwataka viongozi kuchagua kati ya siasa na biashara.
Taarifa zilizomgusa Lowassa
Dkt. Mwakyembe alisema kamati yake ilipomhoji Dkt. Msabaha, alitoa
maelezo ya kiitifaki na mwishowe, akiwa nje ya kiapo, alisema "Mradi
huu ni wa Mkubwa, akimaanisha Bw. Lowassa na rafiki yake
kibiashara akimaanisha Mbunge wa Igunga, Bw. Rostam Aziz," Dkt.
Mwakyembe alinukuu kauli hiyo ya Bw. Msabaha bungeni huku baadhi ya
mawaziri wakibadilisha mikao kuonesha masikitiko.
"Mimi natolewa kafara tu," Bw. Mwakyembe aliendelea kunukuu sehemu ya
maneno hayo ya Dkt. Msabaha aliyomweleza nje ya kiapo na kuongeza
kuwa Waziri wa Nishati wa zamani, alitumia neno la kizaramo
'Bangusilo' lenye maana sawa na kondoo wa kafara.
Dkt. Mwakyembe alisema kiburi cha Wizara ya Nishati na Madini kukaidi
maagizo ya Baraza la Mawaziri na kukaidi ushauri wa wataalamu
mbalimbali wakiwamo Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kilitoka kwa Bw. Lowassa.
"Uamuzi wa Serikali kuizuia TANESCO kuvunja mkataba na kampuni hiyo
licha ya sababu zote kisheria kuwapo ni baadhi tu ya viashiria vya
nguvu kubwa, iliyo juu ya Wizara ya Nishati na Madini, kutumika katika
suala hili na hivyo, kamati teule kutokana na ushahidi wa kimaandishi,
kimazingira na wa mdomo, inaiona nguvu hiyo kuwa ni Waziri Mkuu,"
alisema Bw. Mwakyembe.
Vile vile Bw. Lowassa aliyelezewa kuhusika kwa karibu kuonesha upendeleo kwa kampuni hiyo ambayo Dkt. Mwakyembe aliita ya mfukoni na isiyokuwa na uzoefu hata wa kuweka balbu ya umeme kwenye kishikizo chake.
"Richmond Development Company LLC, imepewa zabuni ya umeme wa dharura
kutokana na maelekezo ya mara kwa mara ya Waziri Mkuu kwa Wizara ya Nishati na Madini katika kila hatua ya mchakato huo (Mchakato wa kumpata mkandarasi)," alisema Dkt. Mwakyembe.
Licha ya kuhusika katika mchakato huo, Bw. Mwakyembe alisema Bw.
Lowassa ndiye aliyefanya uteuzi wa mwisho wa kampuni hiyo.
"Uteuzi wa mwisho wa Richmond kuwa mkandarasi, ulifanywa na Waziri Mkuu mwenyewe tarehe 21 Juni 2006," alisema Bw. Mwakyembe.
Ushauri wa kamati kwa Lowassa, Bunge
Dkt. Mwakyembe alisema Kamati hiyo ilishindwa kumhoji Bw. Lowassa, kwa kuwa watu ambao wangeweza kutoa taarifa ambazo zingesaidia kuombwa kwa hati ya dharua ambao ni Bw. Karamagi na Dkt. Msabaha, walitoa ushahidi ambao haukuweza kusaidia kupatikana kwa hati hiyo.
"Waziri Mkuu ndiye mwenye madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji,
utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi za Serikali, kamati
haikufurahishwa na taarifa zinazomgusa moja kwa moja katika kuipendelea Richmond," alisema Dkt. Mwakyembe.
"Ni wajibu wake mwenyewe kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi huu ndani na nje ya Bunge," alielezea Dkt. Mwakyembe, ambaye hata baada ya muda wake kwisha, wabunge waliamua kwa kauli moja kumwongezea nusu saa zaidi ya kuzungumza.
"Vilevile ni wajibu wa Bunge ambalo linathibitisha uteuzi wake
kuangalia ikiwa matokeo ya uchunguzi huu hayajaathiri hadhi na uzito
wake ndani ya Bunge," aliendelea Dkt. Mwakyembe.
Wanaotakiwa kuchukuliwa hatua kali
"Kamati teule inapendekeza Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo, Dkt. Ibrahim Msabaha na Katibu Mkuu, Bw. Arthur Mwakapugi,
wachukuliwe hatu kali za kinidhamu kwa kuingiza Taifa kwa makusudi
kwenye mkataba na kampuni ya mfukoni ambao umesababisha hasara kubwa
kwa nchi," alisema Dkt. Mwakyembe.
Wengine waliotakiwa kuchukuliwa hatua ya kinidhamu ni Kamishna wa
Nishati, Bw. Bashir Mrindoko, kwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu mpya
wa Wizara kuhusu udhaifu wa kampuni hiyo.
Kutokana na matokeo ya taarifa ya uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kupotosha ukweli, Kamati hiyo pia
ilipendekeza uongozi wa juu wa taasisi hiyo ubadilishwe.
"Taarifa ya TAKUKURU, ililenga kuficha ukweli (White wash) hivyo
ikaishia kujikanganya kwa kukiri kuwapo upungufu, lakini yasiyokuwa na
athari. Taarifa hiyo iliondoa kwa kiasi kikubwa hadhi na heshima ya
chombo hiki muhimu cha kitaifa," alisema Dkt. Mwakyembe.
"Kamati teule inapendekeza mabadiliko ya haraka ya uongozi wa taasisi
hiyo," alisema Dkt. Mwakyembe.
Wengine waliotakiwa kuwajibishwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw.
Johnson Mwanyika kwa kushindwa kutumia taaluma yake kuishauri
Serikali.
Kilichotokea
Dkt. Mwakyembe alisema pamoja na dharura iliyokuwa inalikabili Taifa,
Serikali ilikuwa kinara wa kuvunja taratibu, kanuni na sheria za
nchi.
"Kamati teule imeainisha katika taarifa hii vitendo vya ubabe, ujeuri
na kiburi vilivyofanywa na viongozi wa Nishati na Madini, ili mradi
kampuni waliyotaka iteuliwe, kiasi cha kupindisha hata uamuzi wa
Baraza la Mawaziri bila wasiwasi wowote," alisema Dkt. Mwakyembe.
"Wizara ilikaidi ushauri wa kitaalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Ununuzi wa Umma mara tatu mfululuzo na kinyume na maagizo ya Baraza
la Mawaziri lililotaka Sheria ya Ununuzi wa Umma izingatiwe,"
alielezea Dkt. Mwakyembe.
Licha ya kupuuza sheria na agizo hilo, Dkt. Mwekyembe alisema wizara
hiyo pia ilipuuza vyombo vya ndani vya uamuzi vya TANESCO, ambavyo ni
Bodi ya Wakurugenzi na Bodi ya Zabuni.
"Waliilazimisha Bodi ya Menejimenti ya TANESCO, kuridhia uamuzi
uliofanywa na Wizara ya kuibeba Richmond, kinyume na sheria na taratibu," alisema Dkt. Mwakyembe.
"Ilifikia hatua ya kupotosha kwa makusudi ushauri wa Wizara ya Fedha
uliozuia malipo ya awali ya dola za Marekani milioni 10 (zaidi ya sh.
bilioni 10)," alielezea Dkt. Mwakyembe.
Maswali yaliyokosa majibu
Dkt. Mwakyembe alisema baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri cha
Februari 10, mwaka juzi kuagiza wataalamu kutoka wizara mbalimbali
kushungulikia suala la ununuzi, ukaguzi na mambo mengine kuhusu
mitambo ya kuzalisha umeme, siku hiyo hiyo Wizara ya Nishati na
Madini ilituma ujumbe unaopingana na agizo la Baraza la Mawaziri
kwenda kampuni mama ya Songas ya CDC Globeleg.
Pamoja na kufanya na kufikia hatua ambayo baadhi ya watu walilazimika
kuhojiwa zaidi ya mara moja, Dkt. Mwakyembe alisema baadhi ya maswali
hayajapata majibu.
Maswali ambayo majibu yake yalitarajiwa kupatikana kutoka kwa Dkt.
Msabaha na Bw. Mwakapugi bila mafanikio ni:
"Je, kulikuwa na kikao kingine cha Baraza la Mawaziri siku hiyo hiyo
ya Februari 10, mwaka juzi, kilichotengua uamuzi wake wa awali wa siku
hiyo?"
"Ikiwa jibu ni hapana, kwa nini wizara ilipeleka ujumbe kwenda CDC
Globeleq, ujumbe tofauti na ule ilioagizwa na Baraza la Mawaziri?"
kutoka: majira, 07.02.2008 0157 EAT
Na Waandishi Wetu, Dodoma
Friday, 8 February 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment