Friday, 8 February 2008

Richmondgate: Ripoti yasomwa Bungeni

Kamati yawahusisha Waziri Mkuu, mawaziri Kashfa ya Richmond
* Richmond ni ujasiri wa kifisadi
* Zabuni ilitolewa kwa shinizo
* Uongozi wa Takukuru kitanzini

Na Waandishi Wetu, Dar na Dodoma
Mwananchi
KAMATI Teule ya Bunge ya Kuchunguza Mchakato wa Zabuni ya Uzalishaji Umeme wa Dharura imependekeza kuwa viongozi wote waliosimamia na kuhakikisha kuwa Kampuni ya Richmond Development LLC inashinda zabuni hiyo wawajibishwe.

Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo bungeni jana, Mwenyekiti wake, Dk Harrison Mwakyembe, alisema wamebaini na kuridhika ukiukaji mkubwa wa taratibu na sheria za nchi.

Dk Mwakyembe alisema, kamati imeona mawasiliano ya karibu kati ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Waziri wa Nishati na Madini wa zamani, Dk Ibrahim Msabaha na wa sasa, Nazir Karamag, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Arthur Mwakapungi katika hatua mbalimbali za zabuni hiyo, lakini hawakukiri kutumwa au kuagizwa kubeba kampuni hiyo ya Marekani na kwamba, kwa mfumo wa uongozi na utawala bora wanawajibika wenyewe.

Baada ya uchunguzi wake na kubaini mianya inayoashiria rushwa, kamati imependekeza wahusika kuwajibishwa na mamlaka husika, huku Waziri Mkuu akitakiwa kupima uzito wa suala hilo kwa kuamua kuwajibika mwenyewe au bunge kumwajibisha.

Alisema uhuru mkubwa ambao viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini waliutumia bila wasiwasi kuhakikisha kampuni waliyotaka inapewa zabuni ya umeme unoanyesha kuwa ulitokana na maelekezo ya mara kwa mara waliyopata kutoka kwa Waziri Mkuu katika kila hatua ya mchakato huo.

Aliendelea kuwa, upendeleo wa dhahiri ambao Richmond ilipata kutoka taasisi mbalimbali za serikali ni kama Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambacho kilifikia hatua ya kufumbia macho baadhi ya taratibu zake za msingi ili kuipa kampuni tanzu ya Richmond Development Company LLC cheti cha uwekezaji haraka iwezekanavyo bila kutimiza masharti ya Bodi za Makandarasi na Wahandisi na Wizara ya Nishati na Madini kuikingia kifua kampuni hiyo isichukuliwe hatua za kisheria.

Lowassa amehusishwa na upendeleo wa kampuni hiyo kutokana na barua yake Juni 21, 2006 akiagiza kuwa Richmond ipewe zabuni hiyo na kwamba.

Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema, Ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inatamka wazi kuwa Waziri Mkuu ndiye mwenye madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za serikali na ndiye kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni.

Alisema kamati haikufurahishwa na taarifa zinazomgusa moja kwa moja Lowassa katika kupendelea Kampuni ya Richmond Development na kwamba, kamati imetimiza wajibu wake kwa uwazi na ukweli kama ilivyoagizwa na Bunge.

"Kwa kuzingatia umuhimu wa nafasi aliyonayo Waziri Mkuu katika uendeshaji wa shughuli za serikali na uongozi wa nchi kwa ujumla, ni wajibu wake yeye mwenyewe kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi huu na wajibu wake kikatiba ndani na nje ya Bunge," alisema na kuongeza:

"Vile vile ni wajibu wa Bunge ambalo linathibitisha uteuzi wake kwa mujibu wa Ibara ya 51 inayothibitisha uteuzi wake kuangalia ikiwa matokeo ya uchunguzi huu hayajaathiri hadhi na uzito wake ndani ya Bunge."

Wengine waliopendekezwa kuwajibishwa ni Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, aliyeshabikia na kuingilia uhuishaji wa mkataba huo ambao ulikuwa tayari umekoma, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Msabaha ambaye alikuwa waziri katika wizara hiyo kabla ya kuhamishwa.

Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema, Dk Msabaha akiwa nje ya kiapo alieleza kamati kwamba, yeye ni mbuzi wa kafara kwa sababu biashara hiyo ilikuwa ya Lowassa na mshirika wake, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Viongozi wengine ambao wamehusihwa na tuhuma hizo za kuingiza taifa kwenye mkataba na kampuni ya mfukoni na kusababisha hasara kwa nchi.

Maafisa wa wizara hiyo waliopendekezwa kuwajibishwa ni Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi na Kamishna wa Nishati, Bashir Mrindoko.

Mrindoko anadaiwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu mpya wa Wizara kuhusu udhaifu wa Richmond Development ambao ulijulikana na wizara hiyo tangu mwaka 2004 kwenye Mkataba wa bomba la mafuta.

Rungu la uwajibika ambalo linashikiliwa na Rais Jakaya Kikwete pia, limeelekezwa kuangukia Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kutokana na taarifa yake kuwa taifa halikupata hasara kutokana na mkataba huo.

"Taarifa hiyo imemong’oa kwa kiasi kikubwa hadhi na heshima ya chombo hiki muhimu cha kitaifa kilichopewa dhamana na rushwa na sio kuipamba, ili kurejesha heshima ya umma katika taasisi hiyo, Kamati teule inapendekeza yafanyike mabadiliko ya haraka ya uongozi wa taasisi hiyo," alisema.

Wengine wanatatakiwa kuwajibishwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika ambaye katika majadiliano yake na Kamati Teule alionyesha kutoelewa kabisa kilichokuwa kinatendeka na wasaidizi wake na mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Wakili wa Serikali, Donald Chidowu ambaye ushiriki wake katika GNT haukuwa na tija yeyote, hivyo kuchangia kuingiza nchi katika mkataba wa aibu.

Kamati Teule imeanisha katika taarifa hiyo vitendo vya ubabe, ujeuri na kiburi vilivyofanywa na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini alimradi kampuni waliyotaka iteuliwe kiasi cha kupindisha hata maamuzi ya Baraza la Mawaziri bila wasiwasi wowote.

Dk Mwakyembe alisema, wengine wanaotakiwa kuwajibishwa ni wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco ambao walishindwa kuzuia shinikizo kutoka uongozi wa juu.

Naye Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu, ametakiwa kuendesha uchunguzi na kubaini wakurugenzi waliohusika kwenye malipo ya kampuni hiyo na kuwachukulia hatua za nidhamu.

source: jambo-forum(jf)

No comments: