Friday, 8 February 2008

Richmondgate: ...Wabunge wachachamaa

Wabunge wametaka Baraza la Mawaziri lijiuzulu na viongozi waliohusika katika kashfa ya kampuni ya Richmond wafikishwa mahakamani na kufilisiwa mali walizojipatia kwa njia ya rushwa na ufisadi.

Waliyasema hayo bungeni jana wakati wakichangia ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la mkataba bomu wa Richmond ambayo ilipewa zabuni ya kuzalisha umeme.

Ripoti ya kamati hiyo ilisomwa bungeni juzi na Mwenyekiti wake, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), ambapo ilipendekeza mambo kadhaa ikiwataka mawaziri wa Nishati na Madini, Nazir Kamaragi na Waziri wa Afrika Mashariki Dk. Ibrahim Msabaha kujiuzulu nyadhifa zao.

Aidha kamati hiyo ilipendekeza kuwa Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa atumie busara kuamua jambo la kufanya. Wote hao jana walitangaza kujiuzulu baada ya kumwandikia Rais Jakaya Kikwete kusudio hilo.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Bw. Christopher ole Sendeka (CCM) aliwataka viongozi waliohusika katika tuhuma hiyo kujiuzulu nyadhifa zao na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

``Tusiishie hapa tu wachunguzwe na kufilisiwa viongozi wote waliohusika kuanzia Mwanasheria Mkuu wa Serikali na uongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).``

Alisema inasikitisha TAKUKURU ilipotangaza kwamba mkataba wa Richmond uko safi na haukuwa na dalili yo yote ya rushwa wakati si kweli.

Alisema uandaliwe mpango wa mikataba kutokuwa siri ya Mawaziri na Makatibu Wakuu, bali ifikishwe bungeni na kujadiliwa ili kuwakwepa mafisadi kutumia dhamana waliyopewa kujinufaisha na kulitwisha taifa mzigo.

Aidha, aliwataka wote waliohusika katika kashfa hiyo kunyang`anywa kadi za uanachama wa CCM ili kukiondolea sifa mbaya chama hicho alichodai kinaaminiwa duniani.

Naye Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Bi. Anne Kilango Malecela alisema viongozi wa serikali waliokabidhiwa dhamana na heshima kubwa lakini wakafanya madudu, wameitia aibu serikali.

``Mheshimiwa spika, naomba nizungumzie hoja hii hata kama itanigharimu: Wenzetu wa serikali wanatutia aibu, yote yaliyozungumzwa na Kamati yana vithibitisho kuanzia Waziri Mkuu, Bw. Nazir Karamagi, Msabaha na hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali,`` alisema.

Alisema gharama kubwa inayolipwa na Tanesco kwa kampuni ya Richmond ndiyo inayopandisha gharama za umeme na kusababisha mzigo kwa wananchi.

``Waliotajwa kwenye kamati hii hawafai kabisa kuwa viongozi na wote wanatakiwa kujiuzulu kwa maslahi ya taifa kwa sababu ndiyo wanaosababisha maisha magumu kwa wananchi,`` alisema.

Alisema mambo yote yaliyoandikwa katika ripoti hiyo hayana utata na kwamba yana vielelezo vya kutosha vinavyowatia hatiani watuhumiwa.

Alilitaka bunge kubadilika na kutowaachia na kufanya kazi kwa pamoja bila kujali vyama.

``Tusiwaachie akina Kabwe tu kuwakosoa viongozi wabovu serikalini, bali tuungane bila kujali vyama na kulifanya bunge kuwa mtetezi mkubwa wa wananchi,`` alisema.

Aliwakumbusha wabunge kwamba wapo viongozi wa aina mbili; wale wanaokufa na kusahauliwa na wale ambao wakifa huendelea kuishi vichwani mwa watu.

Alisema viongozi wanaoendelea kuishi baada ya kufa ni wale wanaowatumikia wananchi na hivyo akawataka viongozi wote wajitahidi kuishi baada ya vifo vyao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa (CHADEMA), alitaka Baraza zima la Mawaziri kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo kwa sababu ya uwajibikaji wa pamoja.

Aidha alitaka Mwanasheria Mkuu awajibishwe kutokana na tuhuma hizo.

``Nataka Baraza la Mawaziri lijiuzulu kwa kuwa maagizo, maelezo na majadiliano ya baraza hilo hayawezi kuvunjwa na agizo la waziri mmoja au wawili,`` alisema.

Alisema katika mkataba huo kuna wingu kubwa la rushwa na akataka uchunguzi wa tuhuma hizo ufanywe na Jeshi la Polisi.

Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Bi. Anna Komu alisema kinachosababisha mfumko wa bei kila siku kunatokana na kupanda kwa gharama za mafuta na umeme.

``Maisha magumu yanayolalamikiwa na Watanzania hivi sasa yanasababishwa na viongozi hawa ambao siyo waaminifu, ``alisema kwa uchungu.

* SOURCE: Nipashe, 08 Feb 2008
By Waandishi Wetu

No comments: