Friday, 15 February 2008

'mkataba ufutwe, watuhumiwa washughulikiwe'

'Watuhumiwa Richmond wanyang'anywe pasipoti'
*Wabunge: Mkataba ufutwe, malipo yasimame

WABUNGE wamewachachamalia watuhumiwa wa Richmond na kusema kujiuzulu kwao hakutoshi na wameitaka Serikali iwachukulie hatua pamoja na kuwanyang'anya pasipoti ili wasitoroke.

Pia wameitaka Serikali kusimamisha mara moja malipo ya Sh. milioni 152 zinazolipwa kwa kampuni ya Richmond, kufilisi mali za watuhumiwa wakiwamo waliojiuzulu na mkataba huo usitishwe kama ilivyofanywa kwa kampuni ya kusambaza maji Dar es Salaam ya City Water.

“Serikali ikamate pasi za watuhumiwa wote wa Richmond wasitoroke nchi, kujiuzulu tu hakutoshi, lazima wachukuliwe hatua kali zaidi,” alisema Mbunge wa Viti Maalumu, Bi Grace Kiwelu (CHADEMA).

Naye Mbunge wa Iramba Mashariki, Bw. Mgana Msindai alisema: “Wenzetu (Kamati), walikwenda mpaka Marekani hakuna kampuni ya Richmond, sasa hizi fedha zililipwa kwa nani?.

“Tunataka haya malipo yasimamishwe mara moja, kama hakuna kampuni tunamlipa nani wakati haipo? Kama ni watu fulani ndio wanalipwa fedha za walipa kodi wafilisiwe,” alisema Bw. Msindai.

Aliendelea: “TAKUKURU wametajwa katika ripoti hii nao wawajibishwe, nirudie kuiomba Serikali kusiwe na mchezo, mawaziri walioteuliwa wamejifunza kwamba ukilegea kidogo mambo yanaharibika,” alisema.

Naye Mbunge wa Igalula, Bibi Tatu Ntimizi (CCM), aliitaka Serikali kuwachukulia hatua kali waliotajwa katika ripoti hiyo hata kama si wanasiasa na kusisitiza, kwamba ni lazima mali za waliohusika moja kwa moja zifilisiwe kwa manufaa ya umma, ili liwe fundisho kwa watu wengine.

“Kila mwezi TANESCO inakusanya sh. bilioni 30, lakini sh. bilioni 21 wanalipa madeni za Richmond, IPTL, Songas na Aggreko, kupe wamejaa TANESCO ndiyo maana iko ICU, kama tulivunja mkataba na City Water, kwa nini tusivunje na Richmond? Au City Water hakukuwa na mtu ndiyo maana tulivunja mkataba?.

“Tusiogope kushitakiwa, hakuna mkataba ambao hauwezi kujinasua, kutokana na hayo yaliyojitokeza ni wakati muafaka sasa Serikali kukubali kuleta mikataba bungeni, hizi ni enzi za ukweli na uwazi, urasimu huu ndio umetufikisha huku, mtu kama umetajwa umehusika kwa nini hawakukutaja Spika au kunitaja Mbunge wa Igalula?,” alihoji Bibi Ntimizi.

Naye Mbunge wa Sikonge, Bw. Said Nkumba (CCM), alisema hakuna sababu ya kuendelea kujiuliza kampuni ya Richmond kwa maelezo kuwa waliotajwa kuhusika kuhakikisha mkataba huo wa hewa unasainiwa ndio Richmond wenyewe.

“Waliohakikisha kwamba mkataba huo unasainiwa ndio Richmond, maana kila mahali kule Marekani na hapa nchini hakuna hiyo kampuni, Mheshimiwa Mbunge mwenzetu, ndiye anapokea sh. milioni 152 kila siku, ni lazima wawajibishwe kinidhamu pia, tumeibiwa, badala ya fedha hizi kulipa malimbikizo ya walimu, suala la kujiuzulu haliwezi kuwa ndio suluhisho,” alisisitiza Bw. Nkumba.

Alisema ni lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya walioitwa na kukataa kujitokeza, kwani walilidharau Bunge zima lililounda Kamati hiyo Teule na kuipa majukumu ya kisheria ya kuhoji kila mtu ambaye angeweza kutoa taarifa za kusaidia kujua ukweli.

“Wapo wafanyabiashara ambao wameingia katika siasa kama kinga kufanya mambo yasiyofaa, wapo wafanyabiashara wengi wanaotoa misaada bila kuwa hata na mawazo ya kuwa wanasiasa ... wanatoa misaada kila siku, lakini hawaoneshi nia ya kuwa wanasiasa, si lazima uwe mbunge au diwani ndio usaidie watu," alisema Bw. Nkumba.

Aliitaka Serikali kuangalia upya suala la TAKUKURU na baadhi ya taasisi zake muhimu na kuziweka chini ya Mamlaka ya Bunge moja kwa moja, ili ufuatilie uwe rahisi kwa maelelezo kuwa taasisi hizo zikiwajibika kwa Bunge, ni lazima zitekeleze majukumu yake ipasavyo kila wakati.

Naye Mbunge wa Kilindi, Bibi Beatrice Shellukindo alisema, “wananchi walio wengi wanachotaka ni fedha zirudishwe, kujiuzulu hakuna uhusiano na fedha, wengi wanajiuliza wabunge wa CCM walikuwa wapi, lakini unajua unaweza kuvumilia, lakini imefika sasa ni lazima tuseme.

“Kwa kile kilichotokea, TAKUKURU tubuni chombo kingine kinachoshughulikia rushwa lakini si kile, pia nidhamu ya woga ni kubwa sana Serikali, ni lazima watumishi wa umma waondokane na nidhamu ya woga,” alisema Bibi Shellukindo.

Alisema kutokana na suala la Richmond yeye na mume wake tayari wameandika wosia kwa Mwanasheria kwa kuwa wamepokea vitisho vingi na kwamba hawezi kuogopa kutetea maslahi ya Taifa kwa kuwa anaamini mlinzi mkuu ni Mungu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo, Bw. Charles Keenja (CCM), alisema kilichotokea katika mkataba wa Richmond si bahati mbaya, bali ni jambo lililopangwa kwa makusudi, hivyo lazima hatua kali zichukuliwe bila kuangalia suala la kujiuzulu.

“Hivi sasa wananchi na sisi tunachangishwa fedha kulipia uchafu huu, lazima hatua kali zaidi zichukuliwe, fedha hizi zinalipwa Watanzania tu na si watu wa Marekani, Serikali lazima itueleze fedha hizi zinalipwa kwa akina nani,” alisema Bw. Keenja.

Naye Mbunge wa Busanda, Bw. Kabuzi Rwilomba (CCM), alitoa mwito kwa Bunge kuhakikisha Kamati Teule haiishi tu kwa Richmond bali iende mpaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambako pia kuna 'madudu' ya EPA na mengine mengi.

“Tusingependa kusikia ‘kasungura kadogo tukagawane’ kumbe wenzetu wanakula sungura nzima sisi tunapewa manyoya, wote waliohusika wachukuliwe hatua kali, siasa isiwe kichaka cha wafanyabiashara kuficha maovu,” alionya Bw. Rwilomba.

Wabunge wote waliochangia walimsifu Mwenyekiti wa Kamati Teule, Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe na kueleza kwamba licha ya vitisho na kila aina ya maneno, lakini wamesaidia Taifa kwa kufanya kazi kwa uaminifu bila hofu.

Walimtaka Dkt. Mwakyembe kuwasilisha maoni ya Kamati yake leo kuhusu hatua zinazostahili kuchukuliwa, dhidi ya wahusika bila hofu na kwamba watakuwa nyuma yao kuhakikisha mapendekezo yao yanatekelezwa na na katika Mkutano wa 11 wa Bunge wapewe majibu ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kulingana na mapendekezo hayo.

kutoka: majira, 15.02.2008 0235 EAT
Na John Daniel, Dodoma

No comments: