Monday, 18 February 2008

Mama Salma Kikwete, Mama Raula Bush

Laura Bush, mke wa Rais George Bush wa Marekani, amekemea vitendo vya unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watoto wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

Alisema vitendo vya aina hiyo, vinachangia kuwafanya watoto hao, kukosa matumaini, licha ya kuwa na ndoto za maisha bora ya baadaye.

Bi. Laura aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipoungana na mke wa Rais Jakaya Kikwete, Salma Kikwete, kuzindua Mpango Kazi wa Huduma za Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kipindi cha mwaka huu hadi 2010.

Hafla hiyo ilifanyika katika ofisi za makao makuu ya taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), inayoongozwa na Mama Salma.

Ilihudhuriwa na watu mbalimbali akiwamo mke wa Waziri Mkuu, Bi. Tunu Pinda, baadhi ya mawaziri wanawake, wake za marais wastaafu, Mama Maria Nyerere, Sitti Mwinyi, Anna Mkapa na mke wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Bi. Regina Lowassa.

Awali, Bi. Laura alimkabidhi Bi. Salma funguo za gari la wagonjwa, lililotolewa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kwa WAMA.

Kabla ya kukabidhi funguo hizo, Bi. Laura, alimpongeza Rais Kikwete na mkewe kwa jitihada na ushiriki wao katika vita dhidi ya virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Alisema gari hilo litasaidia kupunguza kadhia zinazowapata wagonjwa hususani waliopo maeneo ya vijijini ambapo WAMA inaratibu miradi ya afya.

Kwa upande wake Bi. Salma, alisema tatifi mbalimbali zinaonyesha kuwapo ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu, inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2010, idadi hiyo itafikia milioni nne.

Bi. Salma, alisema jamii imekuwa na utamaduni wa kuwalinda na kuwahudumia watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.

``Ukoo, udugu wa karibu umekuwa nguzo imara kwenye jamii katika kulinda, kutunza na kutoa mahitaji ya lazima kwa watoto hao,`` alisema.

Hata hivyo, alisema utamaduni huo wenye usalama umeanza kudhoofika kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo ongezeko la vifo vya wazazi kutokana na Ukimwi, umasikini uliokithiri unaokwaza jamii kuendelea kutoa huduma bora kwa watoto na ndugu zao.

* SOURCE: Nipashe, 18 Feb 2008
By Mashaka Mgeta


Mke wa Rais Bush Mama Laura Bush ameeleza kuridhishwa kwake na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na ongezeko maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI.

Mama Laura aliyasema hayo Dar es Salaam jana, wakati akizindua Mpango Kazi wa Taifa wa Huduma kwa Watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Alisema Tanzania ni kati ya nchi za kwanza kuandaa Mpango Kazi wa aina hiyo ambao hivi sasa unaonesha mafanikio makubwa kwa kundi la watoto husika ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

"Serikali ya Marekani, itaendeleza mpango wake wa kusaidia mpango huo wa dharura wakati nchi inapoingia katika utekelezwaji wa mpango wa pili," alisema.

Mama Laura alisema ni wazi kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Rais Kikwete na Mkewe Mama Salma ni mfano wa kuigwa kwa kuonesha moyo wa kulea yatima na kuwaongoza Watanzania katika uzinduzi wa kampeni ya upimaji wa virusi vya UKIMWI kwa hiari.

Alisema ili mpango huo uweze kufanikiwa, ni jukumu la Serikali kuhakikisha unakuwa endelevu kuanzia shule za msingi nchi nzima ili uweze kukidhi mahitaji ya jamii inayolengwa kufikishiwa ujumbe wa kupiga vita na kukomesha unyanyapaa dhidi ya ugonjwa huo.

Naye Mama Salma, alisema tafiti mbalimbali zilizowahi kufanyika, zinaonesha kwamba idadi ya watoto walio katika mazingira hatarishi inaongezeka mwaka hadi mwaka.

Alisema kwa mujibu wa ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002, asilimia 10-12 ya watoto walio na umri wa miaka 18, wamo katika mazingira hatarishi ikiwa ni idadi inayokadiriwa kufikia watoto milioni mbili ambapo kati ya hao, asilimia 42 ni yatima wanaotokana na UKIMWI.

Alisema zaidi ya nusu ya walezi wa watoto hao ni bibi au babu wenye umri wa miaka 65 na kuendelea wakati asilimia 12 ya watoto hao, ni wale wanaojilea wenyewe na kulea wadogo zao na kwamba ifikapo mwaka 2010, idadi ya watoto hao itakuwa imefikia milioni 4.

"Natambua na kuthamini mchango wako katika kuhamasisha upatikanaji wa huduma za jamii kwa wanaohitaji na pia nakupongeza kwa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za kudhibiti UKIMWI na kuhamasisha upatikanaji wa misaada mbalimbali kwa nchi zinazoendelea hususan kwa watoto na wanawake," alisema Mama Salma.

Aidha Mama Salma alimshukuru Mama Laura kwa niaba ya Shirika la Misaada la Marekani (USAID), kwa msaada wa gari la huduma ya kwanza lilitolewa kwa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) inayojihusisha na masuala ya kijamii.

Rais Bush na mkewe wapo katika ziara ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika ambapo kabla ya kuja nchi ziara yao ilianzia Benin, baada ya kumaliza ziara yake ya siku nne nchini, Rais Bush atatembelea pia Rwanda, Ghana na Liberia kabla ya kurejea Marekani.

Naye Magesa Magesa kutoka Arusha anaripoti kuwa
Rais Bush leo anatarajiwa kuwasili mjini hapo kwa ziara ya siku moja

Akiwa Arusha atatembelea Hospitali ya Wilaya ya Meru,iliyopo Tengeru mjini hapa na baadaye atatembelea kiwanda cha kutengeneza vyandarua vya Olyset, cha A to Z,kilichopo Kisongo mjini hapa.

Lengo lake kutembelea kiwanda hicho na hospitali hiyo ni kukagua na kujionea namna utekelezaji wa miradi ya kupambambana na malaria na UKIMWI unavyotekelezwa.

(www.majira.co.tz, 18/02/2008)

No comments: