Baraza: Wapya sita, 14 waenda na maji
RAIS Jakaya Kikwete jana Jumanne, alitangaza Baraza lake jipya la Mawazili akisema limezingatia muundo mpya wa Serikali ambao umefanywa, ikiwa ni pamoja na kuunganisha wizara, kuzipunguza na kuunda nyingine mpya.
Akitangaza Baraza lake hilo kwenye Ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema wizara iliyokuwa ikishughulikia mahusiano ya jamii, chini ya Kingunge Ngombale-Mwiru, ambaye ameamua kustaafu, imefutwa.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, majukumu ya wizara hiyo mengine yamehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na mengine yanasalia kwa washauri wa Rais wa mambo ya siasa.
Wizara ya Fedha imeunganishwa na ile ya Mipango na Uwezeshaji, ili kufanya wizara mmoja ya Fedha. Tume ya Mipango iliyokuwa chini ya Mipango na Uwezeshaji, sasa itafanyiwa mabadiliko na kisha itakuwa chini ya Ofisi ya Rais.
Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Raia zimeunganishwa, na kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Wizara nyingine zilizounganishwa ni ile ya Elimu na Ufundi na ile ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.
Rais alisema kutokana na uwingi wa shule za sekondari zilizofunguliwa, uendeshaji wa shule hizo pamoja na zile za shule za msingi sasa utakuwa chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), huku kukiwa na maofisa wa elimu wawili, moja wa sekondari na mwingine wa msingi.
Kwa upande wa sayansi na teknolojia, na teknolojia ya mawasiliano (ICT), Rais alisema kwamba zitaundiwa wizara ambayo sasa inaitwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Kitengo cha uwamwagiliaji maji kimehamishiwa kwenye Wizara ya Maji kutoka Wizara ya Kilimo, wakati kitengo cha uvuvi kimehamishwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na kupelekwa Wizara ya Mifugo.
Wizara ya Sheria nayo imefanyiwa mabadiliko, ambapo Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye ndiye alikuwa akibeba pia majukumu ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, sasa nafasi hizo zimetenganishwa. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali atabakia kama msaidizi mkuu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa wizara atakuwa mtu mwingine.
Kwa kuzingatia mabadiliko hayo, Rais alitangaza kwamba sasa Serikali yake itakuwa na mawaziri 26 na manaibu 21, na kufanya jumla 47, tofauti na Baraza lililovunjwa lililokuwa na jumla yao 60.
Akitangaza Baraza la Mawaziri hilo jipya, alisema kuwa Ofisi ya Rais (Utawala Bora) itakuwa chini ya Sophia Simba na ile ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma itaendelea kuwa chini ya Hawa Ghasia.
Kwa upande wa Ofisi ya Makamu wa Rais alisema kwamba masuala ya Muungano yatashughulikiwa na Waziri Muhammed Seif Khatib, wakati masuala ya mazingira yatakuwa chini ya Dk. Batilda Burian.
Ofisi ya Waziri Mkuu itakuwa na Waziri wa Nchi (Sera), na ambaye atashughulikia Uratibu na Bunge ambaye ni Philip Marmo, wakati Waziri wa Nchi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI) atakuwa Steven Wassira. Naibu Waziri wa TAMISEMI atakuwa Celina Kombani.
Wizara ya Mipango na Fedha itakuwa chini ya Mustafa Mkullo na manaibu waziri wake watakuwa Jeremia Sumari na Omar Yusuf Mzee.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii bado itashikiliwa na Profesa David Mwakyusa na Naibu Waziri pia atabakia kuwa Dk Aisha Kigoda.
John Chiligati ataongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliyokuwa chini ya John Magufuli ambaye sasa anakwenda Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi akiwa na Naibu Waziri Dk. James Wanyancha.
Profesa Jumanne Maghembe ataongoza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, akiwa na Naibu Waziri, Gaudensia Kabaka na Naibu Waziri, Mwantumu Mahiza.
Wizara mpya ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia itaongozwa na Waziri Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu Waziri, Dk Maua Daftari.
Wizara ya mindombinu ambayo umebadilishwa kuwa ikijihusisha na barabara zaidi itaendelea kuwa chini ya Waziri Andrew Chenge na Naibu wake Dk. Milton Makongoro Mahanga.
Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo imepeta Waziri mpya ambaye ni George Huruma Mkuchika na Naibu wake atabaki kuwa Joel Bendera.
Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana itakuwa chini ya Profesa Juma Kapuya na Naibu wake atakuwa Hezekiah Chibulunje.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji sasa atakuwa Profesa Mark Mwandosya na Naibu wake atakuwa Injinia Christopher Chiza.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika atakuwa Profesa Peter Msolla na Naibu wake akiwa Dk. Matayo David Matayo.
Margaret Sitta atakuwa ndiye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Naibu wake atakuwa Dk. Lucy Nkya.
Waziri wa Maliasili na Utalii anakuwa Shamsa Mwangunga na Naibu Waziri anakuwa Ezekiel Maige.
Wizara ya Mambo ya Ndani itakuwa chini ya Lawrence Masha na naibu wake, Hamisi Kagasheki.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itaendelea kuongozwa na Bernard Membe na Naibu wake, Seif Ali Iddi.
William Ngeleja anakuwa Waziri kamili wa Nishati na Madini akiwa na Naibu Waziri, Adamu Malima, huku Wizara ya Katiba na Sheria ikiongozwa na Mathias Chikawe.
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itakuwa chini ya Dk. Hussein Mwinyi na Naibu Waziri, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaongozwa na Dk. Deodorius Kamala na Naibu wake anakuwa Mohamed Aboud.
Wizara ya Viwanda Biashara na Masoko sasa itakuwa chini ya Waziri Dk Mary Nagu na Naibu Waziri, Dk Steven Chami.
kutoka: www.raiamwema.co.tz,
Mwandishi Wetu Februari 13, 2008
Friday, 15 February 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment