PART I
Ukatili majumbani: Jinamizi linalowatafuna wanawake kimyakimya
Ukatili wa majumbani unaendelea kumkandamiza mwanamke wa Kitanzania na yule wa Afrika kutokana na mila potofu, tamaduni au desturi zilizopitwa na wakati kuendelezwa na baadhi ya makabila.
"Mtoto wangu niliyezaa na aliyekuwa mume wangu wa kwanza anashikiliwa na aliyekuwa mume wangu wa pili mpaka pale familia yangu itakapomlipa ng’ombe wanane aliotoa kama mahari wakati nikiolewa”.
Haya ni maneno ya Bi. Ester Masiaga, binti mdogo mwenye umri wa miaka 20 ambaye katika umri wake huo, amekwishaolewa mara mbili na kuachika.
Kwa sasa angelikuwa na watoto wawili, lakini kwa bahati mbaya mimba aliyobeba akiwa kwa mume wake wa pili, iliharibika kutokana na kipigo kikali alichopata toka kwa aliyekuwa mume wake wa pili.
Akizungumza kwa huzuni kubwa na machozi yakimtoka, Bi. Ester anasema anakumbuka kuwa akiwa na umri wa miaka 16 baba yake mzazi alimchukua toka mikononi mwa mama yake mkoani Mwanza na kwenda kumuozesha kwa mwanaume mmoja, aliyemtaja kwa jina moja la Emmanuel katika kijiji cha Mwananchi.
Anasema mwanaume huyo alikuwa ni mtu mzima kushinda yeye ila hakumbuki alikuwa na miaka mingapi, ila kwa kumwangalia katika sura yake alijua ni mtu mzima.
`` Sikuwahi kwenda shule kwa kuwa wazazi wangu hawakunisomesha,`` anaongea binti huyo mwenye rangi ya chungwa, mrefu na anayeonyesha kukata tamaa ya maisha.
Anasema kuwa kutokana na kuwa na umri mdogo kazi nyingine za nyumbani zilimpa shida kuzifanya na hiyo ilisababisha kupigwa kila siku na mumewe huyo, hadi aliporudishwa kijijini kwao akiwa na mimba ya miezi sita.
Anaongeza kuwa shangazi yake alichukua jukumu la kumtunza hadi alipojifungua mtoto wake wa kwanza.
Anasema mtoto wake huyo alipofikisha miaka miwili alitafutiwa mwanamume mwingine na kuozeshwa huko Musoma, mkoani Mara.
Anasema kuwa kama ilivyokuwa kwa mume wake wa kwanza kuwa na umri mkubwa, vivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mume wake wa pili anayemtaja kwa jina la Chacha Range.
“Mateso yalikuwa ni kila siku, lakini haya yalizidi maana hata mwanangu niliyekwenda naye huko alikuwa akiteswa na wakati mwingine alilazwa katika majani yenye umande asubuhi,” anasema Bi. Ester huku machozi yakimtoka.
Anasema manyanyaso hayo yalizidi na siku moja asubuhi, alikutana na mwanawe huyo akiwa amelazwa katika majani na alipohoji kulikoni, hapo ndipo amani ikatoweka ndani ya nyumba.
Anasema mumewe alimjia juu na kuanza kumwangushia kipigo kikali, na kumtaka kuondoka ndani ya nyumba hiyo haraka iwezekanavyo.
* SOURCE: Nipashe, By Usu-Emma Sindila, 20 Nov 2007.
PART II
Unamfukuza mkeo wa ndoa, unalundika vimada ndani!
Vurugu ndani ya familia zetu wakati mwingine ni za kujitakia. Yapo matatizo ambayo yangeweza kutatuliwa mapema ili hali ya amani na utulivu nyumbani irejee, lakini kwa kuyapuuza, yakazua matatizo mengine makubwa zaidi.
Niliwahi kuchambua kituko kimoja ambapo baba mwenye ndoa yake aliamua pia kumuweka kinyumba shemeji yake(mdogo wa mkewe), kisha hausigeli ndani ya nyumba yake.
Shemeji pamoja na hausigeli baada ya kutambulishwa rasmi kwa bi-mkubwa walijengewa nyumba zao jirani na bi-mkubwa huyo. Bila shaka vurugu zile ulizisoma.
Leo sikiliza vurugu zinazokaribia kufanana na hizo ujionee namna nyumba zetu zinavyobomoka kutokana na sababu mbalimbali, moja ikiwa na kutoridhika na kile ulichokitafuta mwenyewe kwa utashi wako.
Yupo baba mmoja mwenye kazi nzuri tu inayomuingizia kipato. Anaye mkewe wa ndoa ambaye wamebahatika kuzaa watoto watatu.
Wamejenga nyumba yao nzuri kubwa ya kifahari na kwa ujumla maisha yao yalikuwa mazuri.
Miaka miwili hivi iliyopita, baba huyu akaletewa nyumbani mtoto ambaye alimzaa nje ya ndoa.
Inasemekana mtoto huyo aliletwa na mama yake mzazi baada ya baba kukwepa malezi. Mama kumfikisha tu kwa babake akatimua zake. Bi-mkubwa ilibidi akae kimya, hali iliyoashiria kumkubali mtoto yule. Hakuona sababu ya kulumbana na mumewe.
Baba huyu anaye dada yake ambaye inavyoonekana alikuwa haelewani na wifi yake(mke wa kaka yake). Mara kwa mara walikuwa wakizozana kwa masuala yasiyoeleweka.
Wakati kutokuelewana huko kukiendelea, baba mwenye nyumba akawa naye hawaelewani na mkewe. Kila siku mzozo wakati mwingine bila sababu.
Ikafikia wakati mume huyu akawa anamwambia mkewe iko siku nitamchinja kwa kisu. Mama akadhani ni utani, hawezi. Kwani kwa kisa gani kikubwa hata kufikia uamuzi huo.
Kama utani, mume huyu akamwambia bi-mkubwa nikirudi nyumbani leo nisikukute, la, nitakuchinja kweli. Akaondoka zake.
Bi-mkubwa akadhani ni masihara, aliporejea akashangaa kumkuta. Alichofanya mzee aliingia jikoni kuchukua kisu. Mama kuona vile akamnyakua mwanaye mdogo wa miaka mitatu hivi na kukimbia naye.
Akapeleka malalamiko yake kwa ndugu zake, mshenga wa ndoa na hata kufikisha mahakamani akiomba talaka na mgawanyo wa mali walizochuma na mumewe.
Siku ile bi-mkubwa alipotimka nyumbani, jioni yule wifi yake akamleta mwanamke ambaye alikuwa hawara wa kaka yake ili azibe nafasi iliyoachwa.
Kaka yake kuona vile akafurahi na moja kwa moja akamkabidhi bed-room aliyokuwa akilala na bi-mkubwa. Hata dada yake alishangilia kwani hakumpenda katu bi-mkubwa kama hawara huyu.
Haukupita muda, yupo mwanamke mwingine ambaye alikuwa amewekwa kinyumba na baba huyu na tayari alikuwa amezaa mtoto.
Nyumba aliyokuwa amepangishwa kodi ikawa imeisha. Na aliposikia kuwa bi-mkubwa ameondoka, naye mbio na mwanae wakatinga kwa mzee.
Kufika pale baba akawa anashangaa lakini ikatumika busara ambapo yule hawara wa kwanza alipewa chumba kingine na yule aliyekuja na mtoto akaruhusiwa kulala chumbani alikokuwa akilala bi-mkubwa kabla ya kutimua.
Sasa katika nyumba ile kukawa na wanawake wawili walioziba pengo la bi-mkubwa baada ya kuondoka.
Katika kushughulikia mzozo baina yake na mumewe, bi-mkubwa akaamuriwa na vyombo vya usuluhishi kwamba arejee kwa mumewe wakati shauri lile likipatia ufumbuzi.
Bi-mkubwa alikubali kurudi katika mji wake. Hata hivyo, kutokana na vitisho vya awali vya mumewe kwamba angemchinja, hakuthubutu kulala katika chumba chake na mumewe bali alilala chumba kingine.
Chumba kikubwa aliendelea kuishi yule bibie aliyekuja na mtoto mchanga. Bi-mkubwa kwa sasa ametulia akisubiri maamuzi ya kudai talaka. Lakini hawa vimada wawili, ni purukshani tupu.
Inapotokea bwana mzee anataka kumtoa outing mmoja wao, inabidi afanye mahesabu makubwa. Anafanya kama mwizi yaani atampa kideti huyu akidhani mwenzake hatajua.
Lakini kwa jinsi wanawake hawa wawili walivyojiwekea mtandao wa kumfuatilia mwanaume huyu, mwenyewe anawavulia kofia.
Anaweza kumwambia mmoja amfuate mahali fulani wakati fulani.
Huku akiamini kuwa inakuwa ni siri. Lakini anapokuwa akijiburudisha, ghafla anatokea mwenzake, anavuta kiti na kutaka ahudumiwe sawia.
Bwana hana la kufanya, kwani wote ni wanawake zake, hivyo anatulia kama zumbukuku.
Si unajua mtu aliyetekwa nyara anavyokuwa mjinga. Anapelekeshwa tu hajui hili wala lile.
Yote haya ni ya kujitakia. Bwana huyu hivi ana raha gani katika maisha haya ya kuzungukwa na wanawake wasio na tija kwake?
Wao nyumbani ni kula kulala na kumtafuta leo anakunywa baa gani. Hivi baba huyu biashara ziyeyuke, arudi pale nyumbani watakuwa wanatizamana vipi?
Binafsi, matatizo mengine wanadamu tunajitakia.
Mke mkubwa alikuwa nyota ya bahati kwa baba yule. Alikuwa mtulivu na mvumilivu. Ona pale alipoletewa mtoto wa nje kwa mara ya kwanza, alitulia, hakuona sababu ya kuzua rabsha kwani alitambua Maisha Ndivyo Yalivyo na hata kama angebisha, mtoto kashazaliwa na ameletwa kwa baba yake, kumbe angefanya nini zaidi? Namsifu mama huyu kwa hili, ni mvumilivu na aliyekomaa.
Huyu ndiye aliyekuwa mke anayeweza kubeba mambo. Hofu yake kubwa ni ile hatua ya mumewe kumtishia kumchinja, vinginevyo asingeondoka nyumbani kwake. Alipenda mji wake, alipenda familia yake, hata majirani wameeleza hayo.
Sasa baba huyu hana amani. Kila kukicha wanawake hawa wanamvizia yuko wapi. Je, ana raha gani huyu? Baba ni kiongozi wa nyumba, kiongozi wa familia, anapoyumbishwa na tamaa za nje ya ndoa, familia nayo ni kama vile imetoweka.
Watoto kamwe hawawezi kuishi katika misingi ya maadili mema, tulivu na endelevu.
Huu ni wakati wa kutunza familia zetu, tuheshimiane, tuvumiliane, tusameheane. Na zaidi ya yote, tuachane na tamaa za mwili zisizo na tija.
Wasalaam
SOURCE: Nipashe
Na Anti Flora Wingia, 2007-11-18
Email:
fwingia@yahoo.com
Tuesday, 20 November 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment