Tuesday, 13 November 2007

Kunradhi, Mheshimiwa Malecela!

Nimesoma juzi ktk gazeti Nipashe ushauri wa Mheshimiwa John Cygwiyemis Malecela kwa CCM, kuwa ibadili utaratibu wake wa kutafuta viongozi/wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa. Mhe Malecela alisema kuwa alishawahi kuongea na makamu mwenyekiti/rais wa ANC cha Afrika Kusini Ndugu Jacob Zuma juu ya utaratibu wanaoutumia na kuuona ni mzuri kuliko wa CCM. Pia Mhe Malecela amesema kuwa zipo nchi nyingi kusini mwa Afrika mfano Msumbiji (FRELIMO?) ambazo taratibu zao kutafuta viongozi zinafaa kuigwa na hazina malalamiko kutoka kwa wagombea hasa wanaoshindwa ktk chaguzi ndani ya chama.
Mawazo na ushauri huu wa Mheshimiwa Malecela aliyoyatoa huko nyumbani kwake Mvumi Mission, ktk sherehe ya kumpongeza kung'atuka umakamu m/kiti, ni mazuri na hayapaswi kufumbiwa macho na kuyazibia masikio. Yanafaa kuigwa na CCM na hata vyama vya upinzani kwani lengo ni maelewano ndani ya vyama na ushindani sawia.

Pamoja na kuridhishwa na mchango huu wa mawazo ya Mheshimiwa Malecela, bado mimi nina swali la nyongeza nalielekeza kwake.

Mhe Malecela amekuwa makamu wa mwenyekiti CCM Taifa kwa miaka 15, amekuwa ndani ya chama tangu enzi za TANU na sasa ni mjumbe wa kudumu kamati kuu ya CCM.
Hivi kweli Mheshimiwa ulishindwa kuyapeleka mapendekezo/mawazo yako ktk vikao halali vya CCM ili viyafanyie kazi?
Ni kwanini unayasema haya baada ya wewe kung'atuka na uko nje?
Kama ulijua haya mapungufu ulitumiaje nafasi yako kama makamu wa mwenyekiti wa chama (tena ngazi ya Taifa) kuyatafutia ufumbuzi.
Ulikuwa na nafasi ya kuonana na kuongea na wenyeviti wote wa CCM enzi za uongozi wako: wahesimiwa Rais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin W Mkapa na mhe Rais wa sasa Jakaya Kikwete, na makatibu wakuu wao Ndugu Gama, Philip Mangula na wa sasa Yusuf Makamba.
Ulikuwa na uwezo kabisa kusaidia kivitendo, je ulifanya hivyo?
Kama ulishindwa wewe, Makamu Mwenyekiti, mtu wa ngazi za juu kabisa kicheo - unamwambia nani aifanye hiyo kazi?

No comments: