Monday, 26 November 2007

Ajali ya MUSS: Leo ni miaka 21

Mnamo tarehe 26/11/1986, miaka 21 iliyopita Shule ya Sekondari Musoma (MUSS) ilipata pigo kubwa ktk historia yake chini ya Mkuu wa Shule Nashon Otieno.

Gari la shule ambalo wanafunzi walilibatiza jina la FOKKER (Isuzu Tipper tani 7) likiwa njiani toka Shule ya Ualimu Bweri, Manispaa ya Musoma, ilipata ajali ktk kona jirani na machinjioni. Katika ajali hiyo wanafunzi kadhaa walipoteza maisha yao (ingawa sikumbuki idadi yao kwa uhakika ila ni kati ya 8 na 10 hivi!).

Timu ya mpira wa miguu ya Shule ilialikwa kucheza mechi ya kirafiki na wenzao wa Chuo cha Bweri.
Katika msafara huo wa Bweri nami ilikuwa niwemo. Mimi pamoja na rafiki yangu Amon Herman Kafugugu tulikuwepo na tulipania kupanda FOKKA la shule ili kwenda kushuhudia mpambano. Lakini kutokana na wingi wa wanafunzi ndani ya gari (washangiliaji na wachezaji)nafasi haikuwa inatosha kwa wote waliokuwepo kuondoka kwa FOKKA. Ilibidi mwalimu wa michezo Ndugu Maningu apunguze idadi. Mimi na Kafugugu ni miongoni mwa waliopunguzwa na hivyo hatukuondoka. Wapo walioenda kwa miguu maana pale na Bweri sio mbali na wakati wa kurudi walidandia gari.

Jioni ile wakati wa kurejea shuleni ktk kona, huenda kutokana na mwendo wa kasi FOKKA ilipiduka na kuua hapo hapo. Habari za ajali zilipofika shuleni, wanafunzi karibia wote tulikimbia kuelekea eneo la ajali. Tulipofika pale tulianza kutoa msaada pale tulipoweza na kusimamisha baadhi ya magari ili kutoa msaada wa usafiri hadi hospitali ya mkoa. Kwa kweli barabara ilifungika kwa muda ktk kipindi chote cha kuhudumia majeruhi na kuwanasua majeruhi na waliopoteza maisha, maana wengine walikuwa wamebanwa na vyuma vya gari!

Mwanafunzi mwingine aliuwawa ktk ajali ya pili (ajali ndani ya ajali). Lori moja likitokea Bweri, wakati giza lilishaanza, lilipita katikati ya wanafunzi waliokuwa wamezunguka eneo la ajali bila tahadhali wala kupunguza mwendo; na lilitokomea bila kusimama. Rafiki yangu Kafugugu nae alinusurika ajali ya pili ingawa alikanyagwa mguu (foot) ambao aliuuguza (jeraha) kwa zaidi ya mwezi hospitalini!

Ukumbi wa MUBIG ulitumika katika kutoa salaam za mwisho kwa marehemu.

Ingawa majina yao yamenitoka lakini bado nawakumbuka wanafunzi wenzangu waliopoteza maisha yao ktk umri mdogo. Natoa pole kwa wote walioguswa ktk ajali na misiba hasa ndugu na marafiki wa marehemu.

No comments: