Thursday, 15 November 2007

Muhidin Issa Michuzi: Bongo Celebrity?

Juzi, nilikuwa naongea na marafiki hapa Boston. Tukawa tunajadili habari za Tanzania kama serikali kuongeza mishahara ya wafanyakazi na madhara yake. Watu wameachishwa kazi shauri ya waajiri kushindwa kulipa mishahara mikubwa. Tuliongea kuhusu wasichana wanaopata mimba shuleni Bongo na kasi ya UKIMWI. Tuliongea kuhusu kuingiza magari Bongo na barabara zilivyojaa magari mpaka yanashindwa kutembea.

Ajabu tulijadili kwa kirefu zaidi kaka Michuzi na blogu yake maarufu ambayo karibu kila MTanzania nje ya nchi ana habari nayo. Tulisema amekuwa kama Oprah hapa Marekani, mtu ambaye watu wanamwamini na wanamtegemea kwa mambo kadhaa. Kuna watu ambao hawana raha mpaka wameona blogu ya Michuzi kama vile watu hawaoni raha mpaka wameona show ya Oprah.

Watu wakitaka habari za Bongo hawaendi kwanza ippmedia.com au site ya Daily News wanakimbilia blogu ya Michuzi. Na sasa kwa vile watu wengi wanasoma blogu ya Michuzi basi watu wanataka habari zao zionekane pale maana wanajua wengi wataziona.

Michuzi akibandika kitu watu wanakimbilia kwenye blogu yake kutoa maoni yao maana wanajua wengi watasoma. Kama kuna msiba watu wanatoa habari pale, pia kama kuna haja ya mchango watu wanatoa habari pale. Juzi tuliona habari ya mtoto mdogo aliyehitaji msaada wa kutengeneza uso. Watu walitoa pesa na ushauri mara moja. Pia Michuzi kaanzisha lugha ya 'Michuzi talk' yaani kuandika kiingereza kwa kiswahili. Wabongo wanaipenda kweli.

Na Michuzi akitoa maoni yake watu wanaona kama ndo sheria. "Michuzi kasema!" Lakini hasa navyoona waBongo wa nje ya nchi wanampenda kwa sababu anatoa picha za nyumbani na kufanya watu wajisikie hawako mbali na nchi yao.

Tulibishana kuhusu habari ya kuwa eti anatoza watu kubandika habari zao kwenye blogu. Ilibidi nimpigie Michuzi kumwuliza. Alisema hiyo habari si kweli. Hatozi hata senti tano kubandika kitu kwenye blogu yake. Alisema wakati mwingine anaweza kupewa kitu kama shukurani lakini hatozi.

Kwa kifupi uhusiano wangu na Michuzi ulianza zamani hata kabla hajawa mpiga picha wa Daily News. Alikuwa ni kijana tu mwenye kamera aliyekuwa anapiga picha za watu wakiwa disko. Msemo wake ulikuwa, " Natafuta michuzi!" Ndo kapewa jina la Michuzi. Tukamshauri awe mpiga picha wa kujitegemea Daily News, yaani freelance. Akawa analeta picha nzuri kuliko hata wapiga picha walioajiriwa pale.

Nakumbuka alivyoajiriwa Daily News mwanzoni wahariri waligoma kumwita Michuzi, wakasema atumie jina la Muhidini Issa. Lakini kila mtu alikuwa anamwita Michuzi na watu wa nje wakawa wanamwita Michuzi, mwisho walikubali aitwe Michuzi. Kwanza ilikuwa kwenye brackets, 'Michuzi'. Mwisho waliachia vizuizi na Michuzi ndo ilikuwa jina lake.

Michuzi ana moyo ya kazi anayofanya. Na kwa wasiojua Michuzi ni mwigizaji mzuri sana.


Kutoka: blog ya Chemi

No comments: