Wakongwe wa Yanga kuiongoza SPUTANZA
29 Nov 2007
By Badru Kimwaga, Jijini
Wachezaji watatu wa zamani wa timu ya Yanga, Ramadhani Kampira, Sekilojo Chambua na Mohammed Husseni `Mmachinga` wameteuliwa kukiongoza Chama cha Wachezaji wa Soka wa Tanzania, SPUTANZA, ambapo moja ya majukumu waliyopewa ni kuhakikisha wanawaandikisha wanachama wapya na kuunganisha nguvu za wachezaji wote wa mkoa huo.
Uteuzi wa viongozi hao wapya wa chama hicho waliteuliwa hivi karibuni baada ya kufanyika kikao cha uongozi wa taifa wa SPUTANZA uliokutana jijini na tayari wameshapelekewa barua za kufahamishwa juu ya uteuzi huo.
Mmoja wa viongozi hao aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti, Ramadhan Kampira amesema yeye na wenzake waliletewa barua iliyotiwa saini ya Mwenyekiti, Venance Mwamoto kuwa watakiongoza chama cha mkoa wa Dar es Salaam ili kuhakikisha chama kinakuwa na nguvu na kuwaunganisha wachezaji wote wa zamani na wale wa sasa wanaoendelea kucheza mpira.
Kampira amesema mbali na jukumu la kusaka kwa kuhamasisha wachezaji wote kujiunga na chama cha mkoa pamoja na kile cha taifa, pia watakuwa na kazi ya kuwaunganisha wachezaji hao hususani wale wa zamani ambao wamesahauliwa na taifa licha ya michango yao mpaka leo kuwepo katika kumbukumbu za Tanzania.
Kampira aliwashukuru wale wote waliofanikisha kuteuliwa kwao na kuahidi kutekeleza kwa hali na mali majukumu yote waliyopewa huku akisisitiza kitu cha msingi ni kupewa ushirikiano wa kutosha.
* SOURCE: Alasiri
Friday, 30 November 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment