Thursday, 30 August 2007

Wivu ktk Mapenzi!!!

Mara nyingi tunasikia habari ya mtu kumpiga mpenzi wake kwa ajili ya wivu. Mwanamke kasalimiwa na mwanaume mwingine, kibao! Mwanamke anapiga simu nyumbani kumwulizia mtu, mke anampiga na sufuria na mengine.
Lakini wakati mwingine wivu unazidi mpaka watu wanafanya maajabu.
Nimesikitika sana kusikia habari ya jamaa kujinyonga Gesti huko Tandika eti kwa vile mpenzi wake wa miaka 19 alikuwa na wapenzi wengi. Kitu gani kilimwingia marehemu Said Libonge mpaka kaamua kumchoma mpenzi wake kisu na yeye mwenyewe kujinyonga. Ni wivu au ugonjwa wa akili?Mimi sikuwepo bali nimesoma tu hiyo habari ya kusikitisha. Na huyo dada lazima atajiuliza mara mbili tatu kabla ya kuingia gesti na mwanaume au kuwa na mpenzi mwingine.Lakini nikikumbuka vituko wanavyofanya wapenzi kwa jina la wivu, nasikitika na nacheka.
Haya tuchukue kesi ya mama fulani aliyemkuta mume wake yuko kwenye shughuli ndani ya gari eneo ya Mbuyuni Dar es Salaam miaka ya tisini. Yule mama alidai kuwa alifungua mlango wa gari kamkuta mume wake yuko juu ya howara wake anapampu na alidai kuwa mambo yao yalikolea kiasi kuwa alikuwa anampiga mume wake aliyekuwa ameshusha suruali matakoni na hakusikia kitu. Kwanza mtu wa kawaida angebakia anashangaa mdomo wazi, au angekimbia kwa aibu. Lakini hapa huyo mama na wivu zake kaweza kufungua mlango wa gari na kuanza kumpiga mtu shughulini.
Haya nakumbuka kisa cha mama mwingine miaka ya themanini. Mume wake alienda na howara wake kwenye gesti Manzese. Yule mama alijua yuko chumba gani. Kitanda kilikuwa chini ya dirisha. Basi yule mama alikesha pale kwenye dirisha na walipoanza mambo yao, yule mama kafungua dirisha na kuwamwagia chupa ya tindi kali. Kwa vile walikuwa uchi wote waliungua vibaya!
Wivu jamani!
Nilivyokuwa nasoma Tabora Girls kuna dada fulani aliuliwa na mume wake. Sitamsahau yule dada. Alikuwa anakaa National Housing na mume wake, ndoa yao bado changa. Dada mwenyewe alikuwa mzuri kweli kweli. Mume wake alikuwa ni mwanajeshi mwenye cheo cha Kepiteni. Alikuwa mwembamba mwenye kipara. Kuna wenzangu walimuwa wanamvizia yule baba. Basi kuna siku yule baba alishikwa na wivu, kamfunga kamba mke wake na kumtia matambara mdomoni mwake kusudi asiweze kupiga kelele. Wanasema kuwa yule baba alimpiga raundi ya kwanza, kampiga raundi ya pili, kampiga raundi ya tatu mpaka yule dada kafa. Eti kapusuliwa bandama! Kisa cha kumpiga mke wake mpaka kafa kilikuwa eti alimwona anaongea na mwanume mwingine. Yule baba alihukumiwa kifo.
Niendelee?
Kuna visa vingi, vya watu kuua au kuumiza wapenzi wao kwa jina la wivu.
Mimi mwenyewe nimeshikwa na wivu mara kadhaa lakini siyo kiasi cha kuua au kumwumiza mtu! Niwasimulimie kisa kimoja. Kuna jamaa nilikuwa nampenda sana. Lakini yeye hakunijali wala nini zaidi ya kusalimiana. Basi kuna siku nilimwona anakwenda kwenye deti mjini DSM na dada fulani! DUH! Nilijikuta naona kizunguzungu, Siwezi kusema, hasira zimejaa na nikaanza kulia! Watu waliniuliza nalia nini, nikashindwa kusema! Baadaye nikasema basi Mungu hakupanga niwe naye. Yaani nikikumbuka nacheka.

source: chemi's blog

2 comments:

Anonymous said...

Mosonga,

Asante kwa majibu yako katika blogu yangu.

MOSONGA RAPHAEL said...

Chemi nafurahia sana makala zako. Si hii peke yake bali nyingi sana ulizoandika ktk blog hii. Ya kwanza ambayo ilinisisimua sana ilikuwa ile ya Matako Makubwa ikifuatiwa na ile ya maisha ya JKT Masange (ambapo mimi pia nilipitia kama miaka 6 baada yako).

Yaani unaonyesha ukomavu wako katika 'open-ness of mind and freedom of expression!'

Kuna vitu ambavyo watu wengi wanaona haya kuvisema wazi, lakini ktk giza wanavisema au kuvifanya. Lakini wewe umeonyesha ukomavu wako ... na sasa wengi wetu tunaweza kuona na kujifunza.

Nadhani wapo wengi pia ambao mambo kama haya yamewagusa kimaisha na walikuwa wanapata shida kimawazo. Na kwa bahati nzuri sasa wataona kuwa kumbe hili sio tatizo lililowapata wao pekee bali ni kwa mwanadamu yeyote linaweza kumpata au limeshamsibu!

I really find your blog very entertainig and a place to socialize with everybody, because you have shown the way!!!

Thank You Chemi.