Muda wa kuanzisha shirikisho bado - Wabunge
03 Aug 2007By Lucy Lyatuu, Dodoma
Wabunge wamesema muda wa Tanzania kukubali kuunda Shirikisho haujafika hadi hapo matatizo yanayozikabili nchi hizo kiuchumi na kisiasa yatakapopatiwa ufumbuzi. Aidha, wamesema uamuzi wa kuwepo shirikisho aachiwe mwananchi pekee kwani ndiye atakayeamua baada ya kuelimika. Hayo yalisemwa jana bungeni katika mawasilisho ya bajeti ya fedha kwa mwaka 2007/8 ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Msemaji Mkuu wa kambi ya Upinzani, Bw. Abubakar Khamis Bakary, alisema muda wa kukubali kuingia katika shirikisho kwa Tanzania haujafika. Alisema mambo ya kuzingatiwa ni pamoja na tofauti za nchi wanachama ambapo uchumi wa Kenya uko juu pamoja na maendeleo ya viwanda ukilinganisha na nchi nyingine za Uganda na Tanzania. Alisema Tanzania haijafikia uwezo wa kushindana na Kenya katika sekta hiyo na hivyo basi hofu inaweza kugeuzwa soko la bidhaa za Kenya ni ya msingi. `Je Tanzania imejiandaaje kuingia katika ushindani huu wa kibepari? Je, muda wa matayarisho wa miaka mitano utatosheleza kwa Tanzania na Uganda kufikia hatua ya Kenya?` Alihoji. Alisema ipo hofu kwa vijana wa Kitanzani kukosa ajira rasmi kutokana na ushindani wa soko la ajira. `Hili pia linachangiwa na mfumo wetu wa elimu na udhaifu wa lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi wa kitanzania. Madhara yake ni kuongezeka kwa umaskini na vijana wetu watakuwa na kazi duni nchini mwao. Hilo ndio lengo la kujitawala?` Alizidi kuhoji Bw. Abubakar. Alisema tatizo lingine ni kwamba kila nchi hadi sasa inatumia sarafu yake ambazo zinatofautiana sana kithamani ambapo sarafu ya Kenya ni zaidi ya mara kumi na tano ukilinganisha na ya Tanzania. Hata hivyo, alisema hali ya demokrasia ya nchi hizo ni mbovu na kwamba zingeboreshwa kwanza kabla ya kufikia hitimisho wasije kuangukia katika mfumo mbovu zaidi wa kisiasa na kuzidisha matatizo. Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Bw. Peter Serukamba, alisema wananchi waelimishwe kwanza umuhimu wa Shirikisho la Afrika Mashariki kabla ya kuingia. Aidha, alisema wanaohitajika katika shirikisho hilo ni nchi ya Burundi na Rwanda kutokana na kununua bidhaa nyingi za Tanzania. `Kwa mfano mauzo ya Tanzania kwenda nchini Burundi ni Sh. bilioni 46 wakati wao wananunua Sh. milioni 44, sasa inaonekana kuwa wanahitajika katika shirikisho hilo,` alisema Bw. Serukamba. Hata hivyo, alishauri kutowafuata Wakenya na pia akataka nchi hiyo isiwaburuze Watanzania katika shirikisho na badala yake waingizwe Demokrasia ya Kongo (DRC) kwani wana manufaa kwa Tanzania. Naye Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Wilbrod Slaa, alisema suala la kukamilika kwa Urais wa Shirikisho wa Afrika Mashariki mwaka 2013 lisitishwe hadi hapo wananchi watakapokuwa wameelewa manufaa yake. Alisema uamuzi wa kuwepo kwa shirikisho na rais wake aachiwe mwananchi ambaye ndiye mwenye dhamana na nchi yake. Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Bw. Zitto Kabwe alisema wasiotaka shirikisho wana hofu. Hata hivyo, alisema lazima serikali ijiandae na kuelimisha wananchi wake nini hasa ajenda ya shirikisho kama ilivyo kwa nchi nyingine.
* SOURCE: Nipashe
Friday, 3 August 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment