Yanga yatinga fainali Tusker
09 Aug 2007By Somoe Ng’itu, Mwanza
Timu ya soka ya Yanga jana ilitinga fainali ya michuano ya Tusker baada ya kuisukumiza nje Tusker ya Kenya kwa kuichapa kwa penati 4-2, baada ya kutoka sare ya 1-1 katika muda wa dakika 90. Yanga ikicheza kwa kujiamini zaidi ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 37 kupitia kwa mchezaji wake wa kimataifa Wisdom Ndlovu kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Amir Maftaha. Pamoja na kupachikwa bao hilo wachezaji wa Tusker hawakukata tamaa, ambapo katika dakika ya 60 waliongeza mashambulizi langoni mwa Yanga na kusawazisha katika dakika ya 69 baada ya mshambuliaji mwenye kasi wa Tusker Adam Hassan kuwazidi ujanja mabeki wa Yanga na kufanikiwa kuachia shuti kali lililotinga wavuni. Timu hizo zilimaliza dakika 90 zikiwa zimefungana 1-1 na ndipo sheria ya penati tano tano ilipotumika, ambapo Yanga ndio ilifanikiwa kupenya. Katika penati hizo Yanga ilikuwa ya kwanza kupiga kupitia kwa mchezaji wake Thomas Mourice akifuatiwa na Amri Kiemba, Fred Mbuna na Wisdom Ndlovu ambao wote walifunga isipokuwa Credo Mwaipopo alipiga pembeni penati hiyo. Kwa upande wa Tusker ni James Mlinga na Abuu Yusuph walipiga nje penati zao, huku Edward Kanga na Allan Wanga wao walifanikiwa kuzizamisha penati zao. Kwa matokeo hayo Yanga sasa itakutana na timu ya Mtibwa Sugar ya Turiani katika mchezo wa fainali utakaochezwa keshokutwa, ambapo Mtibwa imefanikiwa kuingia hatua hiyo baada ya kuichapa timu ya Prisons ya Mbeya kwa 2-1.
* SOURCE: Nipashe
Thursday, 9 August 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment