Waitara astaafu
23 Aug 2007By Frank Mbunda
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini, Jenerali George Waitara, anatarajiwa kustaafu kazi na kuagwa rasmi Septemba 17, mwaka huu. Habari za uhakika zilizopatikana jijini Dar es Salaam, zimesema kuwa maandalizi ya sherehe ya kumuaga kiongozi huyo yameanza katika kambi zote nchini. Aidha, imefahamika kwamba Septemba 4, Jenerali Waitara, atazungumza na askari wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani katika kambi ya Lugalo, ikiwa ni sehemu ya kuwaaga. Sherehe rasmi za kumuaga zinatarajiwa kufanyika katika kambi maarufu ya Abdallah Twalipo, Mgulani, jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete. Nipashe imeshuhudia baadhi ya maeneo yakiendelea kufanyiwa marekebisho kwa ajili ya shughuli hiyo muhimu. Aidha, baadhi ya askari wa vikosi vya Dar es Salaam na Pwani wameanza kukusanywa kwa ajili ya mazoezi ya gwaride maalum la pamoja. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Profesa Juma Kapuya, hakuweza kupatikana kuthibitisha taarifa hizo. Jenerali Waitara anakuwa kiongozi wa sita kuliongoza jeshi hilo tangu lilipoanzishwa rasmi Septemba 1 mwaka 1964. Jenerali Mirisho Sarakikya, alikuwa wa kwanza kuliongoza Jeshi hilo, akifuatiwa na Jenerali Abdallah Twalipo, Jenerali David Msuguri, Jenerali Kiaro, Robert Mboma na Jenerali Waitara anachukua nafasi ya sita.
* SOURCE: Nipashe
Thursday, 23 August 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment